Adeladius Makwega — MBAGALA
Jicho la Mwanakwetu lilipotua kwenye barua ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ya Oktoba 23, 2026, lilikutana na ujumbe unaogusa mambo nyeti katika maisha ya Kanisa na jamii. Barua hii inawaalika viongozi wa Kanisa kuadhimisha Misa Takatifu kwa nia ya kuwaombea marehemu na waathirika wa matukio ya ukatili yaliyohusishwa na siku ya uchaguzi ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.
Kwa Mwanakwetu, huu si mwaliko wa ibada pekee, bali pia ni nafasi ya kutafakari thamani ya uhai wa binadamu, nafasi ya sala na wajibu wa Kanisa katika nyakati mbalimbali za maisha ya mwanadamu duniani.
Katika mafundisho ya Kanisa Katoliki, Misa Takatifu ni kiini cha maisha ya Kikristo na tendo kuu la ibada. Kanisa linapowaalika waamini kuungana katika Misa kwa ajili ya marehemu, linawakumbusha kwamba kuwaombea waliofariki ni sehemu muhimu ya imani ya Kikristo.
Kanuni ya 901 ya Sheria za Kanisa Katoliki, maarufu kama Canon Law, inatambua uwezekano wa kuhani kuadhimisha Misa kwa nia ya walio hai au waliofariki. Hivyo, wito huu una msingi unaoeleweka ndani ya mafundisho na utaratibu wa Kanisa.
Lakini jicho la Mwanakwetu linaona kwamba ujumbe wa barua hii hauishii kwa wale waliofariki. Unawagusa pia waliofiwa, waliojeruhiwa, walioshuhudia na wote ambao huenda bado wanaishi na maumivu ya matukio hayo.
Katika mazingira kama haya, Kanisa lina nafasi ya kutoa faraja ya kiroho, kuimarisha matumaini na kuwakumbusha watu kwamba utu wa binadamu unapaswa kuheshimiwa bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi. Kwa mtazamo huo, maombi yanakuwa njia ya kuwakutanisha watu katika huzuni na kuwasaidia kutafakari namna ya kujenga maisha yenye amani.
Hata hivyo, Mwanakwetu anajiuliza: Je, barua hii ni mwito wa kichungaji au ni agizo lenye nguvu ya kisheria ndani ya Kanisa?
Sheria za Kanisa zinatoa mwongozo kuhusu mamlaka ya viongozi na vyombo vya Kanisa. Kanuni ya 447 inaeleza nafasi ya Baraza la Maaskofu katika kutekeleza kwa pamoja baadhi ya majukumu ya kichungaji, huku Kanuni ya 455 ikiweka masharti kuhusu utoaji wa amri za jumla zenye nguvu ya kisheria.
Kwa upande mwingine, barua hii inafungua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Kanisa katika kujenga amani na maridhiano nchini. Kanisa linapowaalika waamini kuungana katika sala, linatoa nafasi ya kutafakari namna ya kuponya majeraha ya kijamii, kuwafariji walioteseka na kuhimiza heshima kwa maisha ya binadamu.
Hii haimaanishi kwamba kuadhimisha Misa pekee kunamaliza matatizo yote yaliyosababisha majonzi. Badala yake, sala inaweza kwenda sambamba na wajibu wa jamii kutafuta ukweli, kusikilizana, kutenda haki na kuchukua hatua zinazofaa kuzuia madhara kama hayo yasijirudie.
Mwanakwetu anaona pia umuhimu wa kutofautisha kati ya maombi ya Kanisa na hukumu dhidi ya watu au makundi fulani. Kuwaombea marehemu na waathirika hakumaanishi moja kwa moja kwamba Kanisa limetoa hukumu ya kisheria dhidi ya mtu fulani, wala si lazima iwe tamko la kuunga mkono upande wa kisiasa. Ujumbe wake unaweza kueleweka kama mwito wa kiroho unaoweka mbele utu wa binadamu, faraja kwa wanaoteseka na matumaini ya amani.
“Taifa linapopitia majonzi, swali si tu namna ya kuwaombea waliofariki, bali pia namna ya kuishi kwa kuheshimiana ili amani iwe sehemu ya maisha ya kila siku.”
Kwa heshima ya barua hii, Mwanakwetu anaomba kusimulia kwa kifupi namna hali ilivyokuwa kwa upande wake tangu Oktoba 29, 2025, hadi hali ya utulivu ilipoanza kurejea, kwa kuzingatia muktadha wa Kanisa Katoliki.
Siku ya Oktoba 29, 2025, Mwanakwetu hakupiga kura kwa sababu kadi yake ya mpiga kura ilimruhusu kupiga kura katika Jimbo la Mbagala, Mtaa wa Kizinga, jijini Dar es Salaam, wakati huo yeye alikuwa Musoma, mkoani Mara. Kwa hiyo, hakuweza kupiga kura siku hiyo.
Hata hivyo, akiwa Afisa Habari na mwanahabari, Mwanakwetu alikuwa karibu na vituo kadhaa vya kupigia kura. Aliona watu wachache sana katika vituo hivyo. Baadaye, mvua kubwa ilinyesha Musoma Mjini, na hali ya hatari ilitangazwa huku matukio kadhaa yakifuata.
“Kwa wale wanaokumbuka, Oktoba 29, 2025, ilikuwa Jumatano. Oktoba 30 ilikuwa Alhamisi, Oktoba 31 ilikuwa Ijumaa, Novemba 1 ilikuwa Jumamosi, na Novemba 2 ilikuwa Jumapili. Katika siku hizo, matukio yaliyokuwa yakiendelea yaliathiri maisha ya watu na kuwafanya wengi kuendelea kufuatilia kwa makini hali ya usalama katika maeneo yao.”
Mwanakwetu nikiwa Musoma, Jumapili iliyoangukia matukio haya ya dominika ya 31 ya mwaka C wa Liturujia ya kanisa, nilisali katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma. Padri aliyesalisha Misa hiyo alikuwa paroko wa parokia hiyo, anayefahamika kwa jina la Julius Ogolla. Kwa hakika, kwa kadiri ninavyokumbuka, padri huyo hakuzungumzia hali iliyokuwa ikiendelea mitaani katika mahubiri yake siku hiyo.
Mwanakwetu anakumbuka kwamba tulipotoka kanisani, baadhi ya waamini nilioongozana nao walikuwa wakilalamika kwamba padri hakuwa amezungumzia chochote kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea mitaani.
Dada mmoja alisema kwa masikitiko kwamba viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa faraja yetu au kwa kuwa wao wanakaa ndani ya makazi yao na kukaa ndani ya kuta za kanisa, kana kwamba hawaoni yaliyokuwa yakitokea nje?
Kwa Mwanakwetu, mazungumzo hayo yalikuwa na maana kwa sababu yalionyesha namna baadhi ya waamini walivyohisi hali hii katika kipindi hicho. Lakini si nia yangu kutoa hukumu ya jumla kuhusu padri huyo au Kanisa, bali kueleza kumbukumbu yangu na hisia nilizozishuhudia miongoni mwa waamini siku hii
Unaweza pia kurejea makala hii: Ombeeni Marehemu Wetu. https://www.mwanakwetu.co.tz/2025/11/ombeeni-marehemu-wetu.html.
Mwanakwetu anakumbuka pia kwamba siku hiyo kufika kanisani haikuwa kazi rahisi. Kwa mujibu wa kumbukumbu yangu, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walikuwa wakizuia watu kutoka majumbani mwao.
Kwa kuwa nilikuwa nikiishi karibu na Makaburi ya Mwisenge, nilikwenda kanisani kupitia njia iliyokuwa kando ya makaburi.
Hali hiyo ilinifanya nitafakari kwa kina kuhusu mazingira ambayo waamini walikuwa wakiishi na namna walivyokuwa wakijaribu kuendelea na shughuli zao za kawaida, ikiwamo kwenda kwenye ibada. Katika mazingira yasiyoeleweka vizuri, taarifa sahihi, mawasiliano na faraja ya kiroho huwa na umuhimu mkubwa kwa watu.
Pia, Mwanakwetu nakumbuka nyumba niliyokuwa nikiishi wakati huo ilikuwa na mageti matatu imara: geti kubwa la nje, geti la katikati na geti la mwisho. Tulikubaliana kwamba mageti yote yafungwe vizuri kwa ajili ya usalama wetu.
Hata hivyo, kulikuwa na binti mmoja ambaye alitofautiana nasi kutokana na kitendo chake cha kufungua geti na kuliacha wazi. Tulimweleza kwamba angeweza kutumia geti lililokuwa karibu na vyumba vyake. Ikiwa angeamua kutumia geti la upande mwingine, tulimwomba awe na nidhamu ya kulifungua na kulifunga vizuri.
Nyumba hiyo ilikuwa na njia nyembamba ya ndani ambayo mgeni hangeweza kuitambua kwa urahisi na geti moja lilipofunguliwa, mkazi angeweza kufika karibu na mlango wa vyumba vya wakazi wengine. Kwa mgeni ambaye hakuifahamu nyumba hiyo, ilikuwa vigumu kutambua namna njia hiyo ilivyokuwa imepangwa.
Kwa Mwanakwetu, kumbukumbu hizi zinaonyesha jinsi hali ya kutokuwa na uhakika inavyoweza kuathiri maisha ya kawaida ya watu, hata katika sehemu ambazo kwa kawaida mtu angeziona kuwa salama. Tulilazimika kufikiria zaidi kuhusu milango, njia za kuingia na kutoka, na namna ya kuhakikisha usalama wa familia na majirani.
Kuna tukio jingine ambalo Mwanakwetu analikumbuka kwa namna ya pekee. Siku moja ndani ya mwezi Novemba 2025, mtu alibisha hodi kwa nguvu na kuligonga geti mara kadhaa. Baadaye, simu ilipigwa na ndipo nikafahamu kwamba waliokuwa nje walikuwa viongozi wa Jumuiya ya Mtakatifu Antony wa Padua. Miongoni mwao alikuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, mzee mmoja Mkerewe, pamoja na katibu wake. Nilifungua mlango, wakaingia na kuniuliza:
“Jamani, kwema? Tunakuja mara nyingi, lakini tunakuta milango yenu imefungwa. Hatujui kinachoendelea.”
Niliwajibu kwamba ni kweli, milango ilikuwa ikifungwa kwa sababu hali yenyewe haikuwa inaeleweka vizuri.
Mwenyekiti wa jumuiya akaniuliza:
“Je, watu wa nyumba hii mpo salama?”
Nikajibu kwamba wote tuliokuwa upande huo wa nyumba tulikuwa salama.
Kisha mwenyekiti akauliza:
“Marietha Cossam yupo wapi?”
Nikajibu kwamba Mwalimu Marietha, kwa kadiri nilivyofahamu, alikuwa Mwanza kwa likizo ya kujifungua. Mwenyekiti wa jumuiya akaendelea kuuliza kuhusu wakazi wengine ambao hawakuwa Wakatoliki, kama nao walikuwa wazima.
Nikajibu kwamba wote walikuwa wazima. Ndipo mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Antony wa Padua akasema:
“Shida yetu ilikuwa kujua kama wanafamilia wa jumuiya yetu wapo salama. Kama mpo salama, basi kwaherini.”
Baada ya kuhakikisha hali ya wakazi, viongozi hao waliagana nasi na kuondoka.
Kwa Mwanakwetu, kitendo hicho kilikuwa na maana kubwa kuliko mazungumzo marefu. Kilionyesha kwamba jumuiya ya Kanisa inaweza kuwa sehemu ya uangalizi, mawasiliano na kujali maisha ya watu, hata pale ambapo hali ya nje inawafanya watu wajifungie ndani ya nyumba zao. Jambo lililonigusa zaidi ni kwamba viongozi hao hawakuishia kuwaulizia Wakatoliki pekee; waliulizia pia hali za wakazi ambao hawakuwa Wakatoliki.
Kwa hakika kila mmoja anawajibu wake katika kanisa, Kwa makala haya kila Mkristo ajiulize Je Oktoba 29, 2025 alifanya jambo gani? Huu ni wakati wa toba.
Mwanakwetu upo? Kumbuka.
“BARUA YA TEC: SALA, HURUMA NA WAJIBU WA KANISA.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com 0717649257
.gif)








.gif)
Post a Comment