MZEE WA KATIKATI NA MEMA YA HII NCHI

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Nimekuwa nikitafakari mambo kadhaa kwa namna tofauti juu ya maisha ya Watanzania mara baada ya ya Serikali ya Awamu ya Nne kwenda zake, changamoto za Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2015 na pia vuta nikuvute ya Tanzania chini ya Utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Marehemu John Pombe Magufuli ambaye amelala kaburini huko Chato Geita. Utawala wake ukiongozwa na yeye John Pombe na Makamu wake Samia Suluhu , ukikumbwa na kashfa ya shambulio la Tundu Lissu Septemba 17, 2017 ambalo mpaka kesho halina majibu, huku huyu huyu aliyeshambuliwa akiwa na kesi ya uhaini mahakamani.

Huku kwa jicho la mizani ya haki, hesabu hiyo inakataa kabisa, Watanzania wakipigiwa bashrafu ya Ijumaa na Jumapili kuwa taifa hili lina vyombo mahiri vya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai na Mahakama Huru.

Tafakari hii ilianza katika akili ya Mwanakwetu akiwa anatokea nyumba kwake majira asubuhi, akiwa amepanda bodaboda, tafakari hii iliongeza kasi na kumteka kabisa Mwanakwetu. 

 



Kumbuka Bodaboda ndiyo usafiri wa siye akina yakhe. aliposhuka bodaboda hii akawa hana chenji ya shilingi 10,000 hivyo basi kumuomba ampeleke mkahawani ili aywe chai na chenji apate ndipo ampe 2000 yake shilingi.

 Akiwa anaingia mkahawani Mwanakwetu mbele bodaboda nyuma, mama mmoja akawa anasema maneno haya;

“Mie yule ni ndugu yangu kabisa, akaungana na upande mwingine, wakapambana ili nishindwe kura za maoni. Kata ile ilikuwa haina shule ya Sekondari tumepambana na kupata eneo tukaanza na ujenzi

Wewe fikiria mwaka huu wa 2020 kata haina Shule ya Sekondari wakati kilimanjaro Kata moja ina Shule za Sekondarai hadi tatu mpaka nne. Za Serikali mbili na za madhehebu ya dini na shule za watu binafsi. Sisi tulikuwa hatuna lakini nilijitahidi kupambana na sasa shule imekamilika na imepokea kidato cha kwanza.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu mkahawani akatoa noti yake ya shilingi 10,000 akampa mhudumu na kumuomba 2000 ili ampa bodaboda. Hili likafanyika naye Mwanakwetu kuanza kunywa chai chapati moja na supu.

“Yule ndugu yangu alikuwa na kampuni ambayo ilipewa kandarasi ya kufanya usafi katika kituo cha afya na mara nilipoingia mimi kama Diwani 2020 haukupita muda mrefu ile kampuni muda wake wa mkataba ulikwisha hivyo zabuni ikatangazwa ikaomba tena na wazaauni kadhaa.

Wazabuni wenye sifa  kadhaa wakaomba. Zoezi la Zabuni likaipigwa mweleka kampuni ya huyu ndugu yangu na tamati hakushinda zabuni, hapa ilishinda kampuni nyingine. Hapo ndipo tabua zilianza, akilalamika kwa nini sikumtetea, lakini yeye huyu kumbuka ana cheo CCM wilaya.

Watu wapo CCM kimkakati wakizunguka kusaka tenda na makampuni yao kwenye mabegi ukiwanyima kosa na hata ukikosao utendaji wao kazi katika tenda hizo ni kesa Wakaungana na mahasimu wangu kuhakikisha nashindwa udiwani, hapa akiwamo mbunge wa jimbo letu ambapo anagombea sasa.

Wakati wa kura za maoni wakiwakuta wajumbe Waisilamu, wanasema mimi ni Mkristo, hivyo basi sipaswi kuongoza. Kweli walishinda na mimi kupigwa mueleka kura za maoni. Sasa wananipigia simu shiriki kampeni na mimi ninawauliza Hivi Sasa Kwani Mimi Nimesilimu?”

Hawa jamaa  mkahawani wakaamka zao na kutoka nje kuelekea waendao. 

Kwa kando walikuwepo jamaa wawili, hapo hapa akaja jamaa anauza makoti, jamaa hawa mmoja akajaribu koti  moja la rangi ya kijivu likawa limemkaa vizuri , muuzaji alipoulizwa bei akasema shilingi 15,000/- jamaa akalia lia kisha kukubaliwa kwa aheri ya shilingi 10,000/-  

Kizuri hawa  jamaa wapya wawili kumbe wanamfahamu Mwanakwetu wakamlipia Mwanakwetu ile chai yake, mmoja anatoka Tarime alidai alimuona Mwanakwetu katika kikao cha Wafanyabiashara ndogo ndogo na ameisoma makala hiyo. 

Jamaa akasema

“Asante sana ndugu  mwandishi.”

Huyu jamaa aliyemlipia Mwanakwetu yeye anatokea Butiama. 

Mwanakwetu akamuuliza huyu ndugu wa Mwalimu Julius Nyerere, inakuwaje watu Butiama mmemuangusha Jumanne Sagini?

“Ahhh yule yule Bwana kwanza amekula sana mema ya hii nchi, kawa Katibu Mkuu miaka mingi, pili alipokua mbunge yeye alikuwa anawasaidia watu wa Majita tu, sisi watu Butiama katuacha kabisa na ndiyo maana matajiri wenye asili ya Butiama wakaamua kuungana kuwaona wajumbe na kumuangusha, mwandishi hicho ndicho kilichotokea kwa rafiki yako Jumanne Sagini.

Unajua ukiwa na mambo ya Majita unaangusha huko huko na ukiwa mdini utaangusha katika udini, watu wanakuangalia tu tamati lazima uangukie pua. 

Mwandishi  kwaheri , sisi tunakwenda zetu Bunda Bwana, tunakutakia kazi njema. Msalimie ndugu yako Mzee wa Katikati (Butiama) Jumanne Sagini.”

 

Jumanne Sagini alipokuwa Mbunge wa Butiama alipenda kupaita Butima ni Kitovu cha Mkoa wa Mara na yeye  aliitwa Mzee wa Katikati Butiama.

Mwanakwetu hapa akawa anacheka huku akisema Jumanne Sagini siyo ndugu yake bali alikuwa bosi wake maana alikuwa Waziri Mdogo wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Wakati Mwanakwetu akiagana na ndugu hawa hapa mkahawani, mama mmoja wa makamo akamuuliza Mwanakwetu Baba huwa unasoma Biblia? Mwanakwetu akajibu NAAAAM  lakini kwa kujaribujaribu, mama mie najaribu najaribu tu.Mama huyu akasema Sasa mwanagu nakuomba leo nenda kasome Isaya 60, 22.

“My brother remember these words ‘when the time is right, I, the Lord, will make it happen’.:.”

Huyu mama alipomaliza kusema kimombo akasimama na kuondoka zake. 

Mwanakwetu akamaliza kunywa chai hii kisha kuamka kuelekea aendapo, alipofika huko aendapo tu aliitafuta aya ile ya Biblia ikiwa na maneno haya;

“Wakati utakapofika, Mimi Bwana nitalitimiza.”

Mwanakwetu alipouliza wataalamu wa Biblia walijibu kuwa mstari huu wa Biblia kutoka Isaya 60:22 unasema: “Wakati utakapofika, Mimi Bwana nitalitimiza.” Huu ni ukumbusho kwamba Mungu ana wakati kamili kwa mipango na ahadi Zake. Wakati tunaposubiri matokeo ya kiungu, tunapaswa kumtumainia Mungu katika ukuu Wake, tukijua kwamba Yeye anafanya kazi kwa siri ili kuunganisha hali na watu kwa mapenzi Yake kutimizwa.

Mwanakwetu akakumbuka tangu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na hali ya Tanzania ya mwaka 2025 kwa leo inatosha sana.

Mwanakwetu Upo?

Je Makala haya niyaitaje?Kwani Mimi Nimesilimu? Ndugu Sagiji Amekula Mema ya Hii Nchi, Mwanakwetu anachagua Ndugu Jumanne Sagini Amekula Sana Mema ya Hii Nchi

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257














1/Post a Comment/Comments

Post a Comment