HONGERA KWA MAHAFALI

 




Lucas Masunzu – MAKOLE

KATIKATI ya mwaka 2022 ndugu yetu alikutana na watu wengi ukanda wa katikati ya nchi yetu. Kwa bahati akiwa katika ibada ya pamoja iliyofanyika katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma alikutana na ndugu Tryphone Mwinuka kipindi akiwa Rais wa serikali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dodoma. Nduguyetu alikutana na Mwinuka kipindi akijiandaa kukabidhi kijiti cha uongozi maana awamu yake ilikuwa ikimalizika. Kukabidhi uongozi kwa wafuasi wa demokrasia ni jambo ambalo halikwepeki, huyu anashuka yule anapanda kushika usukani. Siku hiyo Mwinuka alikuwa nadhifu alivalia suti nyeusi iliyomkaa sawasawa, nywele zake zilinyolewa mtindo mzuri kama ule wanaopenda kunyoa wanamuziki wengi wa muziki wa rumba.

 

Kipindi cha matangazo kilimnyanyua Mwinuka siku hiyo, akashika maikrofoni akasalimia mamia ya watu waliofurika akaeleza mambo mengi yaliyosindikizwa na neno la kumbukumbu kuhusu kuishi kwa wema kwa kumbukumbu ya kesho. Msisitizo ulikuwa;

 

“Hakipo kitu cha milele duniani kila kitu kina mwisho lakini matendo yetu yawe mazuri au mabaya ndiyo yatakumbukwa daima. Inapendeza zaidi binadamu anapokumbukwa kwa mambo mazuri aliyowatendea nduguze, jamii yake na taifa lake”.

 

Katika ukimya huo watu walikuwa wakisikiliza sauti ya Mwinuka iliyosikika vizuri kupitia spika kubwa zilizokuwa kulia na kushoto upande wa mbele ukumbini hapo. Binti mmoja aliyekuwa ameketi karibu na nduguyetu upande wa kulia nyuma ya huo ukumbi alinyanyua simu yake ya mkononi akaelekeza kamera kwa Mwinuka akapiga picha kadhaa baadaye alisogeza mdomo wake karibu na sikio la Nduguyetu akanong’oneza kwa sauti laini ya chini;

 

Mwinuka ameongoza vizuri licha ya umri wake kuwa mdogo ukizingatia chuo kikuu cha Dodoma kina maelfu ya wanafunzi wakiwamo wa umahiri na uzamivu lakini ameweza.

 

Nduguyetu alimnong’oneza binti huyo ni kweli amejitahidi sana tunamtakia kila lililo jema anapojiandaa kukabidhi uongozi. Mwenyezi Mungu amsaidie ahitimu vizuri masomo yake, atimize malengo yake, kama ana ndoto za kuwa kiongozi hapo baadaye tunamtakia heri”.

 

Kunong’onezana huko kulipamba moto, nduguyetu akamtuliza binti huyo kwa kumkumbusha kuwa wapo katika ibada.

 

Nduguyetu anasema nini leo?

 

Hongera Tryphone Mwinuka kwa kuhitimu na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Hongera kwa wanafunzi wote wanaohitimu shahada katika fani mbalimbali mwaka 2023 katika mahafali ya 14 Chuo Kikuu cha Dodoma. Hongera pia kwa wahadhiri wote Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kufanya kazi nzuri ya kuwaandaa wahitimu.

 

Hongera Tryphone Mwinuka, Kwa heri.

 

theheroluke23@gmail.com

0762665595

@ 2023



 

1/Post a Comment/Comments

Post a Comment