
Adeladius Makwega – DODOMA
Asubuhi ya Novemba 13, 2026, Mwanakwetu alitaka kufahamu kama eneo alilokuwapo lilikuwa na parokia ya jirani.
Swali hilo lilijibiwa na kijana mmoja wa bodaboda aliyesema:
“Japokuwa mimi ni mgeni katika eneo la Ilazo, ninajua kuwa hapa kuna Parokia ya Ilazo, Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.”
Mwanakwetu akasema moyoni: Kumbe vijana wetu wa bodaboda nao wanajua mambo ya Kanisa na parokia!
Mwanakwetu akamuuliza kijana huyo,
“Ni kiasi gani cha fedha hadi kwenye Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili?”
Kijana huyo akajibu kuwa ni shilingi 1,000.
Mwanakwetu akapanda bodaboda hiyo na kuanza safari. Wakiwa njiani, akamuuliza kijana huyo kama anasali katika jumuiya gani hapo Ilazo.
Kijana huyo akajibu kuwa bado hakuwa ameanza kusali katika jumuiya yoyote.
Mwanakwetu akamshauri akumbuke kushiriki katika maisha ya jumuiya na afuatilie kujua eneo analoishi ni jumuiya gani ili aweze kuanza kushiriki katika shughuli za kiimani.
Baada ya muda, Mwanakwetu alifika katika parokia hiyo. Aliona eneo lililokuwa na mwonekano wa shule. Aliingia kupitia mlango mdogo na kuelekea katika duka la parokia, ambako alinunua msalaba mmoja, rozari tatu na shajara moja ya jumuiya ya mwaka 2027.
Akiwa dukani, Mwanakwetu alimtania mama aliyekuwa akihudumu kwa kumuuliza:
“Vipi, vitenge vyetu vya WAWATA mnaviuza hapa?”
Mama huyo akajibu kuwa ndiyo, vinapatikana.
Mwanakwetu akauliza,
“Je, vina pande ngapi?”
Mama huyo akajibu kuwa vitenge hivyo vina pande tatu.
Mwanakwetu akasema,
“Si vina pande mbili?”
Mama huyo akasisitiza kuwa ni kweli vitenge vyao vina pande tatu.
Mwanakwetu akaendelea kumuuliza mama huyo:
“Je, hapa parokiani yupo padri anayeweza kunibarikia visakramenti vyangu?”
Mama huyo akapiga simu kuulizia kama Padri Kerra alikuwapo. Alipopata jibu kuwa padri huyo alikuwapo, Mwanakwetu alipewa mtu wa kumwelekeza hadi alipokuwa.
Mwanakwetu anasimulia:
“Tulifika katika jengo lingine lililokuwa limezungushiwa mabati. Tulibisha hodi na kuingia katika ofisi ya Padri Kerra. Nilimkuta padri mmoja mrefu sana na mweupe sana, ambaye hakuwa mtu wa maneno mengi. Nilimsalimu alijibu na nilimwambia, ‘Padri, naomba unibarikie visakramenti vyangu.’ Padri Kerra alisimama, akaanza sala fupi na kuvibariki visakramenti vyangu. Baada ya hapo, tuliagana.”
Mwanakwetu alitoka na kurudi kwa kijana wa bodaboda aliyekuwa amemfikisha parokiani. Kijana huyo alimrudisha katika eneo jingine kabisa kwa gharama ya shilingi 2,000.
Hii ilikuwa ni safari ya Mwanakwetu kufika katika Parokia ya Ilazo.
Msomaji wangu, naamini ni vizuri kuifahamu kwa ufupi Parokia ya Ilazo.
Parokia hii inajulikana kwa jina la Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili. Mtakatifu huyu alitangazwa kuwa mtakatifu na Papa Francisko Aprili 27, 2014.
Hivyo, jina hilo linaashiria kuwa parokia hii ilianzishwa baada ya kutangazwa kwa utakatifu wa Yohane Paulo wa Pili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kuhusu historia yake, Parokia ya Ilazo ilitokana na maendeleo ya shughuli za kichungaji na ongezeko la waamini katika eneo hilo, likiwa sehemu ya upanuzi wa huduma za Kanisa katika Jiji la Dodoma.Parokia hii wanapatikana kwa simu namba 0759084188.
Swali la Mwanakwetu kutaka kujua parokia ya jirani lilikuwa na sababu kadhaa. Mojawapo ilikuwa kutambua mahali ambapo muumini Mkatoliki anaweza kupata huduma za kiroho anapokuwa mbali na parokia yake ya kawaida.
Katika maisha ya Kanisa, muumini anaweza kupata huduma za kiroho katika parokia nyingine. Si lazima kila wakati arudi katika parokia anayoishi ili kupata huduma hiyo.
Mwanakwetu alikuwa na swali hili akilini: “Kama ningetaka kuungama, je, hapa Ilazo ningeweza kupata huduma hiyo kwa urahisi?”
Kwa mujibu wa Sheria za Kanisa Katoliki (Code of Canon Law), Kanuni ya 991, muumini ana uhuru wa kuchagua padri aliyeidhinishwa na Kanisa kwa ajili ya kuungama dhambi zake, hata kama padri huyo anatoka katika parokia nyingine au Kanisa la ibada nyingine linalotambuliwa na Kanisa Katoliki.
Kanuni hiyo inasema:
“Every member of the Christian faithful is free to confess sins to a legitimately approved confessor of his or her choice, even to one of another rite.”
Kwa tafsiri ya Kiswahili:
“Kila muumini ana uhuru wa kuungama dhambi zake kwa padre aliyeidhinishwa kihalali na Kanisa, kwa chaguo lake mwenyewe, hata kama ni wa ibada nyingine.”
Mambo muhimu ya kuzingatia ni haya:
Muumini halazimiki kuungama katika parokia yake pekee.Anaweza kuchagua padre wa parokia nyingine. Padri anayesikiliza maungamo lazima awe na ruhusa halali ya Kanisa ya kusikiliza maungamo na kutoa ondoleo la dhambi (facultas). Muumini hapaswi kujiona kuwa amefanya kosa la kikanisa kwa kwenda kuungama katika parokia nyingine.
Kwa hiyo, Mwanakwetu alipoitembelea Parokia ya Ilazo na kupata huduma ya kubarikiwa visakramenti vyake, alitambua umuhimu wa kuifahamu parokia hiyo kwa ajili ya huduma nyingine za kiroho, ikiwamo Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho kwa siku zijazo.
Kwa ndugu zangu ambao wakati mwingine mnahitaji kuungama nje ya parokia zenu, ni vizuri kufahamu kuwa mna uhuru wa kwenda katika parokia nyingine na kuomba huduma hiyo.
Unachotakiwa kufanya ni kufika katika parokia husika na kuulizia mahali unapoweza kumpata padri.
Unaweza pia kuulizia katika ofisi au duka la parokia kama kuna padri anayepatikana kwa ajili ya huduma hiyo.
Si lazima ununue rozari, msalaba au kitu kingine ili upate haki ya kuungama. Unaweza kueleza tu hitaji lako kwa wahudumu wa parokia na kuomba kuonana na padri.
Unapokutana na padri, mweleze kuwa unahitaji kupokea Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Ikiwa hayupo tayari wakati huo, anaweza kukuelekeza kuhusu muda unaofaa wa kurudi au namna ya kupata huduma hiyo.
Jambo la msingi ni kutambua kuwa Kanisa ni mama wa waamini wote, na huduma zake za kiroho zinapaswa kuwafikia waamini kulingana na taratibu zake.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka:
“UNAIIJUA PAROKIA YA ILAZO?”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com-0717649257

.gif)
.gif)
Post a Comment