UHURU WA KIDIJITALI: ENEO LINALOIBUA MASWALI MAGUMU KWA TANZANIA

 

Na: Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Mwanakwetu alipokutana na ripoti ya Ibrahim Index of African Governance (IIAG) 2026, aliamua kuichunguza kwa makini ili kubaini Tanzania imeelezwa vipi katika tathmini ya utawala bora barani Afrika.

Alipoanza kuisoma, alikutana na taarifa inayoweza kumpa Mtanzania sababu ya kujivunia na kuwa na matumaini. Ati, Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizo juu ya wastani wa Afrika katika utawala bora!

 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotumika katika ripoti hiyo, Tanzania imepata alama 58.2 kati ya 100, huku ikishika nafasi ya 15 kati ya mataifa 54 ya Afrika.

 

Hata hivyo, Mwanakwetu hakutaka kuishia kwenye alama hizo za jumla. Aliendelea kupekua kurasa za ripoti akitaka kufahamu ni maeneo gani hasa Tanzania imefanya vizuri na ni yapi bado yanahitaji maboresho.

 

Alipofika kwenye sekta ya afya, akakutana na taarifa nyingine yenye matumaini. Ati, Tanzania imepata nafasi ya nane kati ya nchi 54 za Afrika katika kipengele cha afya, ikiwa na alama 68.9 kati ya 100. Hii ni ongezeko la alama 9.6 ikilinganishwa na mwaka 2016.

 

Hapa Mwanakwetu aliona kuna jambo la kutambua. Katika eneo la afya, Tanzania imeonesha maendeleo yanayostahili kuangaliwa na kujadiliwa. Ni ishara kwamba katika baadhi ya viashiria vya huduma za kijamii, kuna hatua zilizopigwa.

Hata hivyo, Mwanakwetu alijiuliza swali moja muhimu:

 

“Juzi kwangu alikuja kijana kuomba msaada wa michango ya matibabu. Je, ni kweli Mo Ibrahim imefanya tathmini yake vizuri, au kuna uhalisia wa maisha ya wananchi ambao takwimu hizi haziuelezi kikamilifu?”

 

Swali hili halimaanishi kwamba kisa cha mtu mmoja kinaweza kupima ubora wa sekta nzima ya afya. Bali linatukumbusha kuwa takwimu za kitaifa zinapaswa kutazamwa sambamba na uzoefu halisi wa wananchi katika kupata huduma.

 

Nusu ya furaha ya Mwanakwetu haikudumu kwa muda mrefu alipogeukia kurasa zinazohusu demokrasia, haki za wananchi na uhuru wa kidijitali.

Hapa ndipo uso mwingine wa Tanzania ulipojitokeza!

 

Mwanakwetu alikutana na takwimu zinazoonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 46 kati ya nchi 54 za Afrika katika kipengele cha uhuru wa kidijitali, ikiwa na alama 27.3 kati ya 100.

 

Alama hizi zinaibua maswali mazito kuhusu mazingira ya matumizi ya intaneti, upatikanaji wa taarifa, uhuru wa kujieleza na nafasi ya wananchi kushiriki katika mijadala mbalimbali kupitia majukwaa ya kidijitali.

 

Kwa hesabu rahisi, Tanzania iko chini kwa alama 22.7 kufikia kiwango cha alama 50 kati ya 100. Ingawa alama 50 si lazima ziwe kigezo rasmi cha kupima mafanikio katika kiashiria hicho, tofauti hii inasaidia kuonesha ukubwa wa changamoto iliyopo.

Mwanakwetu alijiuliza: Je, uhuru wa kidijitali una maana gani katika maisha ya kawaida ya Mtanzania?

 

Kwa hakika, uhuru wa kidijitali si suala la kuwa na simu janja, kununua kifurushi cha intaneti au kuwa na akaunti katika mitandao ya kijamii pekee. Ni mazingira yanayomwezesha mwananchi kupata taarifa, kutoa maoni, kujadili sera za umma, kukosoa pale anapoona kuna mapungufu na kushiriki katika mijadala ya kijamii na kisiasa kwa uhuru na kwa kuzingatia sheria.

 

Ni katika mazingira haya ambapo uhuru wa kujieleza kupitia mitandao unakuwa muhimu. Mwananchi anapaswa kuwa na nafasi ya kutumia majukwaa ya kidijitali kutoa maoni kuhusu masuala yanayogusa maisha yake, jamii na taifa kwa ujumla.

Mwanakwetu akasema:

 

“TCRA, Polisi, mamlaka za uchunguzi na wenye dhamana katika serikali wasiwe hodari wa kuweka mpira kwapani linapokuja suala la haki za wananchi. Kuna simu, vifaa vya kielektroniki, kompyuta, laini za simu na diski kuu zinazochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na kubaki katika ofisi za vyombo vya uchunguzi kwa muda mrefu.Hali hii inawaweka baadhi ya wananchi katika gharama zisizotarajiwa za kununua vifaa vingine ili waendelee na shughuli zao. Wengine wanashindwa hata kuuliza, ‘Simu yangu mtanipa lini?’ kwa kuhofia namna swali hilo litakavyopokelewa na pia kuwakumbusha wachunguzi kukushugulikia.”

 

Hoja ya Mwanakwetu hapa ni kwamba vyombo vya uchunguzi vina wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, wajibu huo unapaswa kwenda sambamba na uwazi, uwajibikaji na kuheshimu haki za watu ambao vifaa vyao vinachukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.

 

Mwanakwetu bado ana maswali kuhusu namna takwimu za Mo Ibrahim zinavyoakisi hali halisi ya uhuru wa wananchi katika mazingira ya kidijitali.

 

Katika uchambuzi wa Tanzania, kipengele cha uhuru wa kujieleza na imani kwa ujumla kimepata alama 48.5, kikiwa katika nafasi ya 32. Hii ni takwimu nyingine inayostahili kuangaliwa kwa makini kwa sababu inahusiana na nafasi ya wananchi kujieleza na kushiriki katika maisha ya umma.

Mwanakwetu aliendelea kujiuliza kuhusu namna maudhui yanavyodhibitiwa katika mazingira ya mtandaoni.

Je, wananchi wana mazingira yanayowawezesha kupata na kusambaza taarifa? Je, wanayo nafasi ya kujadili masuala ya kitaifa kupitia mitandao ya kijamii? Je, mifumo iliyopo inahakikisha kuwa udhibiti wowote unaofanyika unazingatia haki za msingi za wananchi?

 

Maswali haya yana uzito kwa sababu intaneti imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Inatumika katika biashara, elimu, mawasiliano, upatikanaji wa habari na mijadala kuhusu maendeleo ya taifa.

 

Pia, suala la kuzimwa kwa intaneti au mitandao ya kijamii ni eneo muhimu katika mjadala wa uhuru wa kidijitali. Hatua za aina hiyo zinapochukuliwa zinaweza kuathiri mawasiliano, shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa taarifa na ushiriki wa wananchi katika masuala ya umma.

 

Jambo jingine lililomvutia Mwanakwetu ni suala la faragha na usalama wa taarifa za watumiaji wa intaneti.

Katika dunia ambayo taarifa nyingi za watu zinahifadhiwa na kusambazwa kwa njia za kidijitali, ulinzi wa taarifa binafsi ni jambo muhimu. Wananchi wanahitaji mazingira yanayoheshimu faragha zao, yanayolinda taarifa zao binafsi na kuweka mifumo madhubuti ya usalama katika matumizi ya huduma za kidijitali.

Lakini huenda jambo linalostahili kupewa uzito zaidi katika takwimu hizi ni mwenendo wa Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi.

 

Kwa mujibu wa takwimu za ripoti, alama za Tanzania katika kipengele cha uhuru wa kidijitali zimepungua kwa pointi 16.4 kati ya mwaka 2016 na 2025.

Hii ina maana kwamba mjadala haupaswi kujikita kwenye nafasi ya 46 pekee, bali pia katika kutafuta majibu ya kwa nini alama za Tanzania zimeonesha mwelekeo wa kushuka katika kipindi hicho.

 

Ni wakati wa kujiuliza kama mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayohusu matumizi ya teknolojia yamekuwa yakipanua au kupunguza nafasi ya wananchi kutumia uhuru wao wa kidijitali.

 

Kwa ujumla, baada ya kuichunguza ripoti hii, Mwanakwetu anaona picha mbili tofauti kuhusu Tanzania.

 

Upande mmoja kuna matokeo yanayotia matumaini katika baadhi ya viashiria vya huduma za kijamii, hususan afya, ambako nchi imepata nafasi ya nane barani Afrika. Matokeo haya yanastahili kutambuliwa, lakini hayapaswi kutafsiriwa kuwa kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa urahisi au kwamba changamoto za sekta hiyo zimekwisha.

 

Upande mwingine kuna changamoto zinazohusu uhuru wa kidijitali, haki za wananchi, uwajibikaji, usalama na utawala wa sheria. Haya ni maeneo yanayohitaji kutazamwa kwa kina kwa sababu yanaathiri namna wananchi wanavyopata taarifa, kujieleza na kushiriki katika shughuli za kijamii na kitaifa.

 

Hapa ndipo tunapaswa kuelewa kwamba kuwa juu ya wastani wa Afrika katika tathmini ya jumla hakumaanishi kuwa kila eneo la utawala linafanya vizuri. Nafasi ya 15 ya Tanzania ni nafasi ya jumla katika tathmini ya utawala bora, si nafasi ya demokrasia pekee wala kipimo cha mafanikio katika kila sekta.

 

Kwa hiyo, ujumbe muhimu wa Mwanakwetu unaotokana na uchambuzi huu ni kwamba Tanzania inapaswa kujitafakari na kuangalia kwa kina maeneo ambayo bado yanaonesha mapungufu.

 

Mwanakwetu anabaki na swali moja muhimu:

“Tunawezaje kujenga Tanzania yenye maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi huku tukihakikisha kuwa uhuru wa wananchi kupata taarifa, kujieleza na kushiriki katika mijadala ya maendeleo ya taifa unalindwa?”

 

Inawezekana TCRA, Polisi na vyombo vya uchunguzi vikaona vinatimiza wajibu wao vizuri. Lakini tathmini ya Mo Ibrahim, kupitia ripoti hii, inaonesha maeneo ambayo Tanzania inapaswa kuyatafakari na kuyaboresha.

Maana, kama kuna changamoto katika uhuru wa habari na uhuru wa kidijitali, athari zake hazimuishii mwandishi wa habari pekee. Zinamhusu pia mwananchi wa kawaida anayehitaji kupata taarifa, kutoa maoni na kushiriki katika masuala yanayogusa maisha yake na maendeleo ya taifa.

Ni muhimu kuelewa kwamba maendeleo ya taifa hayapimwi kwa uwezo wa kujenga miundombinu ya kiteknolojia pekee, bali pia kwa namna teknolojia hiyo inavyomwezesha mwananchi kupata taarifa, kutumia haki zake na kushiriki katika kujenga mustakabali wa nchi yake.

Kwa taasisi ya Mo Ibrahimu natambua na kuheshimu kazi nzuri mnayofanya kila mwaka lakini mjitahidi muingie ndani zaidi,  kwa kifupi naona ripoti hii ya mwaka 2026 haikufikia kiwango chenu cha miaka ya nyuma.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“UHURU WA KIDIJITALI: ENEO LINALOIBUA MASWALI MAGUMU KWA TANZANIA.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments