UCHOKOZI WA MEYA WA ZAMANI WA DAR ES SALAAM

 

Adeladius Makwega – Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma.

 

Novemba 5, 2026, Mwanakwetu alipachika katika mitandao kadhaa ya kijamii nyaraka moja ya afya iliyohusu ugonjwa wa ndui. Nyaraka hiyo ilikuwa ya Novemba mwaka 1961, siku chache kabla ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika.

 

Mara baada ya nyaraka hiyo kupatikana, wadau mbalimbali walitoa maoni yao. Miongoni mwao alikuwa Ramadhan Zame, ambaye alisema maneno yafuatayo:

 

“Wewe Makwega, mwanangu, umepata wapi nyaraka hiyo? Nakumbuka mwaka 1961 kaka yangu mzee Francis Fidelis Makwega alikuwa darasa la pili, na mimi ndiyo nilikuwa naanza darasa la kwanza. Wakati huo wewe ulikuwa wapi?”

Msomaji wangu, kumbuka kuwa ndugu Zame aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Mbagala na pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

 

Kwa heshima ya Mheshimiwa Zame, vyeo vyote alivyowahi kushika na uenyeji wake wa Mbagala, Mwanakwetu anajibu maswali haya kama ifuatavyo:

 

“Kwanza kabisa, Mheshimiwa Ramadhani Zame, shikamoo! Naomba salamu nyingi zikufikie hapo ulipo, wewe pamoja na mkeo na familia nzima ya Zame hapo Mbagala Makuka, Mbagala kwa Mangaya, na nyumbani kwenu kwa asili Mikwemeni. Najua mlIhamia Mbagala Makuka kutokana na shughuli za biashara na Vijiji vya Ujamaa.

Kwa heshima na taadhima, na kwa hisani ya Ukoo wa Zame na Ukoo wa Makwega, naomba nijibu maswali yako kama ifuatavyo:

 

Ni kweli kabisa kwamba mwaka 1961 nilikuwa sijazaliwa. Pia ni kweli kabisa kwamba baba yangu, Francis Fidelis Makwega, alikuwa mwanafunzi mwenzako wakati huo. Kikubwa zaidi, nyaraka hii nimeipata Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma, ambayo ina jukumu la kutunza nyaraka hizi.”

 

Haya majibu ninayatoa kwa heshima ya mzee wangu Ramadhani Zame wa Mbagala Makuka.

 

Kwa heshima ya wasomaji wangu, naomba nitoe taarifa zaidi kuhusu Francis Fidelis Makwega (baba wa Mwanakwetu), aliyesoma pamoja na Ramadhani Zame enzi hizo huko Mbagala, jijini Dar es Salaam. Aidha, naomba kueleza jinsi mimi, Mwanakwetu, nilivyozaliwa kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.

 

Nikiwa katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma, Tanzania, nilikutana na Bi. Bujo Boniface Ngwale, Afisa Kumbukumbu, ambaye alisema yafuatayo:

 

“Hapa nina faili kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu lenye taarifa za walimu wa Mkoa wa Dodoma kwa mwaka 1977.

Katika orodha hii kuna jina la mwalimu Doroth Hezron Mlemeta, aliyeajiriwa Januari Mosi, 1974, katika Shule ya Msingi Tambi. Alikuwa na namba ya UTS K7974, cheki namba 2193627, alizaliwa mwaka 1956 na alikuwa akilipwa mshahara wa shilingi 575 kwa mwaka 1977.

 

Pia kuna mwalimu Francis Fidelis, mwenye namba ya UTS P321, cheki namba 2231871, aliyezaliwa mwaka 1950. Mshahara wake ulikuwa shilingi 795, akiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tambi kwa mwaka 1977.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtafiti Adeladius, Francis Fidelis Makwega ni baba yake mzazi, na Doroth Hezron Mlemeta ni mama yake mzazi.”

 

Bi. Bujo Ngwale alimaliza maelezo yake kwa namna hiyo.

 

Kwa hakika, kama alivyosema Afisa Kumbukumbu Bi. Bujo Ngwale, mwalimu Francis Fidelis Makwega ni baba yangu, huku mwalimu Doroth Hezron Mlemeta akiwa mama yangu mzazi.

Kwa pamoja, wazazi wangu waliajiriwa Januari 1, 1974. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, Septemba 19, 1974, baada ya wazazi wangu kukutana kazini, nilizaliwa mimi, Adeladius Francis Fidelis Makwega (Mwanakwetu), ambaye ndiye mwandishi wa makala haya.

 

Kwa heshima ya taarifa hizo, naomba tufanye hesabu kidogo. Je, kuanzia Januari Mosi, 1974, wazazi wangu walipoajiriwa, hadi siku nilipozaliwa, ilikuwa ni siku ngapi, majuma mangapi na saa ngapi?

Hesabu yake ni kama ifuatavyo:

 

Kuanzia Januari 1, 1974, hadi Septemba 19, 1974, ni:

  • Siku: 261.
  • Majuma: 37 na siku 2.
  • Masaa: 6,264.

Hesabu hii inazingatia tofauti ya tarehe hizo bila kujumuisha siku ya Januari 1.

Iwapo utahesabu siku ya mwanzo na siku ya mwisho, jumla inakuwa siku 262, sawa na majuma 37 na siku 3.

Hii ndiyo hesabu ya muda wa ujauzito hadi kuzaliwa kwangu lakini hesabu hizi si za kitabibu.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kikubwa ni kumshukuru ndugu Ramadhani Zame, ambaye ni miongoni mwa watu wanaotoka katika koo za zamani za Mbagala, zilizokuwepo miaka mingi kabla ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, wakiwemo Ukoo wa Makwega.

 

Pia, nimshukuru Bi. Bujo Ngwale wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa kufanikisha kuniongoza na kunisaidia kupata taarifa hizi.

Tatu, naomba niwaeleze Watanzania kuwa serikali huwa na taarifa za raia wake, na taarifa hizo zinapohifadhiwa vizuri huwa na umuhimu mkubwa katika kuthibitisha historia ya maisha ya watu na familia zao.

 

Ukizitazama taarifa zangu mimi, Adeladius, utaelewa kuwa nilizaliwa kutokana na mazingira yaliyotokana na harakati za kuanzishwa kwa Vijiji vya Ujamaa. Ni kupitia mazingira hayo ambapo baba yangu, Mpogoro wa Mbagala, alikutana na mama yangu, Mgogo wa Kilimatinde na Muharara, wakiwa kazini katika Kijiji cha Tambi, Wilaya ya Mpwapwa (Kongwa), na ndipo nilipozaliwa.

 

Ukitazama vizuri kisa hiki, jamii ina simulizi yake: “Baba yako mwaka 1961 alikuwa darasa la pili.”

Mimi binafsi ninajua kuwa nilizaliwa Septemba 19, 1974, katika Hospitali ya Mlali. Taarifa za serikali zinaunga mkono tarehe hiyo, na hata hesabu ya muda wa ujauzito inaonesha kipindi cha majuma 37 na siku 2.

Kwa hakika, ni lazima Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ipewe heshima inayostahili kutokana na kazi kubwa ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu za taifa na wananchi wake.

Mwanakwetu, upo? Kumbuka!

“Uchokozi wa Meya wa Zamani wa Dar es Salaam.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257







































 

 



0/Post a Comment/Comments