Adeladius Makwega-DODOMA
Ilikuwa ni Sikukuu ya Kristo Mfalme. Mwanakwetu alihudhuria Misa ya kwanza katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Mara baada ya Misa hiyo, yalipangwa maandamano ya sikukuu. Maagizo ya viongozi wa Parokia yalikuwa kwamba waamini wote waliosali Misa ya kwanza waungane na wale watakaohudhuria Misa ya pili katika maandamano hayo ya kusherehekea sikukuu.
Mwanakwetu alitoka nje, lakini hakukuwa na utaratibu wa haraka wa kuanza maandamano. Akiwa nje hapo, alikutana na mama mmoja aliyemuuliza:
“Wewe, Mzee Makwega, unaingia Misa ya pili au unatoka?”
Akajibu kwamba anatoka, lakini anasubiri maandamano, kama alivyoagiza msomaji wa matangazo.
Mama huyo akasema alikuwa akiwahi nyumbani ili awaandae vijana wake, ambao walikuwa wanakuja kusali Misa ya pili.
Baada ya takribani dakika 15 bila kuwepo kwa utaratibu wa haraka wa kuanza maandamano, Mwanakwetu aliamua kuondoka na kurudi nyumbani kwake bila kushiriki maandamano.
Alipokuwa akiondoka kwa mwendo wa haraka, alikutana tena na yule mama aliyekuwa amemuuliza awali anasali Misa ya ngapi.
Mama huyo akamuuliza swali lingine hapo njiani:
“Umeamua kuondoka?”
Mwanakwetu akajibu:
“Ndiyo. Utaratibu wa maandamano hauko vizuri, wala haujapangwa vizuri. Nimeamua kuondoka.”
Mazungumzo yakaendelea:
“Parokia nyingine, katika misa kubwa za sikukuu kama hizi , huwa na ibada moja. Huanzia saa tatu asubuhi kwa maandamano au huishia kwa maandamano. Huu utaratibu wa kuwa na Misa ya kwanza na ya pili, kisha waamini kuungana katika maandamano, haujawekwa vizuri.”
Wakaendelea na safari ya kurudi nyumbani, njiani walizungumza mambo mengi hasa kuhusu namna Mkristo anavyopaswa kuishi, pamoja na masuala mengine. Hata hivyo, miongoni mwa maneno ya mwanzo yaliyokuwa ufunguo wa mjadala wao yalikuwa haya:
“Hivi, Mzee Makwega, uliyasikiliza yale maombi ya ibada ya leo?”
Jibu lilikuwa ndiyo.
Kwa faida ya wasomaji wa Mwanakwetu, naomba niyarudie maombi hayo kama yalivyosomwa katika ibada ya misa:
“Tukuomba, tuseme: Ufalme wako ufike! Ufalme wako ufike!
Ee Bwana Yesu, ulitutangazia Ufalme wa Mungu. Utufanye tayari kupokea habari za Ufalme wako na kushika kanuni zake, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Mojawapo ya kanuni za Ufalme wako ni kuwapa chakula wenye njaa. Utupe moyo wa ukarimu kwa wote wenye njaa, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Moja ya kanuni za Ufalme wako ni kukaribisha wageni. Utuonyeshe njia ya kuwalisha na kuwakaribisha wale walionyimwa makao na mahali pa kuishi, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Kusaidia wajane na yatima ni mojawapo ya kanuni za Ufalme wa Mungu. Utupe hamasa ya kuwasaidia yatima, hasa waliofiwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Kuwatunza wagonjwa na wazee ni mojawapo ya kanuni za Ufalme wa Mungu. Utupe neema na saburi ya kuwatunza wale wasiopata huduma na matunzo kutoka katika jamii zao, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Kanuni ya Ufalme wa Mungu ni kuwajali wafungwa. Utupe ujasiri wa kuwatetea wale wanaodhulumiwa haki zao, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!
Uzitawale na kuziongoza familia na jumuiya zetu, Ee Bwana — Ufalme wako ufike!”
Ndugu hawa waliendelea kutembea kwa miguu huku wakiongea juu hali hii.
Bila shaka, msomaji wangu, umeyasoma maombi haya.
Mama huyo akauliza:
“Je, Makwega, tunaishi hivyo? Je, makatekista wetu wanaishi hivyo? Je, mapadri wetu wanaishi hivyo? Je, maaskofu wetu wanaishi hivyo?”
Ndugu hawa waliendelea kutembea kwa takribani dakika 15. Baadaye, mama huyo alichepuka na kuendelea na njia yake, huku Mwanakwetu akiendelea kutembea kwa muda mfupi na hatimaye kufika nyumbani kwake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Nina hakika, msomaji wangu, umeyasikia maombi haya ambayo, kwa kadiri ninavyofahamu, yalisomwa katika misa zote dominika hii katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Sina hakika kama katika majimbo mengine pia walisoma maombi haya kama yalivyo. Hata hivyo, jambo muhimu ni hili: Je, wewe na mimi tunaishi kama Kristo Mfalme anavyotuagiza?
Changamoto kubwa inayoukabili ulimwengu wa Kikristo kwa sasa, na hata ndani ya Kanisa, ni kwamba wengi wametekwa na mungu wa fedha.
Hata ndani ya nyumba za ibada na misa fedha hutajwa mara nyingi zaidi kuliko Yesu Kristo.
Msomaji wangu, nakuomba, ndugu yangu, tujitafakari kwa kina jambo hili na hata baada ya misa waamini badala ya kutafakari neno wanatafakari michango na fedha tu.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka:
“Tunaishi kama Kristo Mfalme anavyotuagiza?”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
– 0717649257
.gif)

.gif)
Post a Comment