PROFESA JENGO UMEFARIKI NIKIWA SIJAMPATA MWANAHITI WA ULAYA

 


 Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Chuo cha Humanities, Idara ya Sanaa za Ubunifu (Department of Creative Arts), kimetangaza kifo cha Profesa Elias Eliezar Jengo.

 

Kwa mujibu wa tangazo la kumbukumbu ya marehemu lililotolewa na idara hiyo, Profesa Jengo amefariki dunia Novemba 21, 2026, akiwa na umri wa miaka 90. Alizaliwa Mei 27, 1936.

Idara hiyo imetoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo, huku ikieleza kuwa mchango na urithi aliouacha utaendelea kukumbukwa kupitia maisha ya watu wengi aliowagusa.

 

Maneno hayo yamenigusa sana, kwani mimi ni miongoni mwa watu walioguswa na taaluma na mchango wa Profesa Jengo.

Nimejikuta nikikumbuka tukio moja la mwaka 2012, nilipokuwa katika chumba cha habari cha Shirika la Utangazaji la Ujerumani, Deutsche Welle (DW Kiswahili), mjini Bonn, Ujerumani.

 

Wakati huo, nilikuwa nimepewa jukumu la kuandaa makala kuhusu utamaduni na sanaa. Baada ya kuelekezwa kuandaa muswada, nilikuja na wazo la makala yenye kichwa “Mwanahiti: Zawadi Uyango Uzaramoni.”

 

Mada hiyo ilijadiliwa katika kikao kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Othuman Miraji, na hatimaye ikakubaliwa kwa ajili ya kuandaliwa na kurushwa hewani.

 

Katika kikao hicho, watumishi walitaka kujua ni nani ambao ningewashirikisha katika kujenga makala hiyo. Nilitaja majina ya Bi. Mariam Seleiman Binti Kilemile, bibi wa Kizaramo kutoka Mbagala; Mwalimu Sisa Mwaluka, dada wa Kizaramo aliyepitia mafunzo ya unyago wa Kizaramo; na mwisho, Profesa Elias Jengo, mtafiti na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Kikao kilipokea majina hayo, nami nikaanza mawasiliano na wahusika ili kukamilisha maandalizi ya makala.

 

Katika makala hiyo iliyokuwa na urefu wa dakika 9 na sekunde 45, Bi. Kilemile alieleza:

“Mwanahiti au Mwananyang’iti ni kadude kadogo kama mwanasesere, ambapo binti akifundwa, anakabidhiwa na kuwa nacho katika maisha yake yote hadi anapokuwa mzee. Anapokuwa mtu mzima, naye humkabidhi bintiye.

Mama akiwa na watoto wengi wa kike, anaweza kuomba kuchongewa wanahiti wengine kutoka katika miti ya mkongo, mvule na mpingo ili awape watoto wake wanapokwenda unyagoni. Ndiyo maana majina mengine ya Mwanahiti ni Mwanamkongo, Mwanampingo au Mwanamvule, kutegemea aina ya mti uliochongwa.”

Kwa upande wake, Mwalimu Sisa Mwaluka alisema:

“Ndiyo, nimetoka kuolewa hivi karibuni na ninaye Mwanahiti wangu. Hii ni mila muhimu sana. Jamii nyingi zinashangaa kuniona na hiki kisanamu. Wakati nasoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwenzangu mmoja alikiona na kudhani ni ushirikina. Lakini alipoelezwa kuwa ni mila tu, alielewa. Hata Profesa Jengo alinisaidia kumweleza hadi akaelewa mila hii. Mara nyingi tunakiweka chini ya kitanda au chini ya mto.”

 

Katika kukamilisha makala hiyo, nilimtafuta Profesa Elias Jengo, ambaye naye alieleza:

“Mwanahiti ni mila kubwa sana kwa makabila ya pwani ya Tanzania, kama vile Wakwele, Wazaramo, Wadoe, Waluguru, Wazigua na wengineo. Hata binti akikosa Mwanahiti, wanaamini kuwa pengine akiolewa bila kuwa nacho atapata balaa, hata kuzaa hawezi, na akizaa watoto wake wanaweza kufariki.Mwanahiti kila picha ya maumbile ya uzazi na huku kikiwa na shanga nyeusi, nyeupe na nyekundu na kila rangi ya shanga ina maana yake”

 

Nilizungumza mengi na Profesa Jengo kuhusu mila hii, na katika mazungumzo yetu, aliongeza:

 

“Hata huko Ulaya zipo jamii zenye Mwanahiti wao, kama vile Ugiriki. Hii ni mila ya kutukuka sana.”

 

Nilimwambia Profesa Jengo kuwa nitasubiri kukamilisha makala hiyo, kisha nianze hekaheka za kumsaka Mwanahiti wa Ulaya. Nilimweleza kuwa, ili ujue mbuga ipi ina wanyama wakali, sharti uitembelee kwa kuwa nipi Ulaya nipo mbugani nitamsaka mwanahiti wa Ulaya.

 

Baada ya kukamilisha kazi hiyo, niliandaa makala iliyokuwa na sehemu mbili, ambazo zilirushwa hewani kwa mara ya kwanza Juni 5, 2012, kupitia DW Kiswahili.

 

Mwanakwetu, leo nimeyakumbuka haya kama sehemu ya heshima na kumbukumbu kwa Profesa Elias Jengo, ambaye alikuwa mdau mkubwa wa utamaduni na sanaa ya Mwafrika, pamoja na vyombo vya habari.

 

Nakumbuka hata nilipokupigia simu kwa mara ya kwanza kuhusu kuandaa makala haya, hukusita kunipa ushirikiano. Ulinipa maelezo kwa wakati huo huo na kunipatia namba ya simu ya Mwalimu Sisa Mwaluka, ambaye wakati huo alikuwa akiishi Pugu. Ushirikiano wako ulisaidia sana kukamilisha makala haya.

 

Kwa hakika, nasikitika sana kutokana na msiba huu. Ninatoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote wa Profesa Jengo, pamoja na wadau wa sanaa nchini Tanzania na wote waliopata nafasi ya kufundishwa, kufanya kazi au kushirikiana naye.

Profesa Jengo, umefariki miaka 14 tangu tulipoandaa makala ya Mwanahiti. Wakati huo nilikuahidi kuwa nitaendelea kumsaka Mwanahiti wa Ulaya.

 

Hadi leo, sijampata. Hata hivyo, bado sijakata tamaa. Nitaendelea na jitihada za kumsaka, na siku nitakapompata, nitawajulisha ndugu wa ukoo wa Jengo, nao watafikisha ujumbe huo kwako huko ulipolala.

Hakika, Profesa Jengo, umefariki nikiwa sijampata Mwanahiti wa Ulaya.

Mwanakwetu, upo? Kumbuka:

“Profesa Jengo, umefariki nikiwa sijampata Mwanahiti wa Ulaya.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257









 

 

0/Post a Comment/Comments