KUTOKA BONDE LA MZEE MAFKO HADI KERO ZA UDIKTETA!

 



Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Nilipokuwa nikisoma katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi, nilikuwa natembea umbali wa takribani kilomita 20 kila siku, yaani kilomita 10 kwenda shuleni na kilomita 10 kurudi nyumbani. Hata hivyo, kwangu mimi, umbali huo haukuwa mrefu sana, hasa ukizingatia kuwa nilikuwa kijana mwenye nguvu na ari ya kutafuta elimu. Huyu ndiye Mwanakwetu!

 

Safari yangu ya kila siku ilianzia nyumbani kwetu, Mbagala Kizinga, nyumba namba 7. Kutoka hapo nilipita Sokoni Kizinga, nikavuka Barabara ya Kilwa na kushuka katika Bonde la Mzee Mafko. Baada ya hapo nilipita kando ya Shamba la Maua la Kadozo (GOA), nikapita karibu na Kituo cha Kiroho Mbagala, kisha nikapanda Mlima wa Mtoni Kijichi na hatimaye kufika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi. Hii ndiyo ilikuwa safari yangu ya kila siku katika kipindi chote cha masomo yangu ya shule ya msingi.

 

Safari hii ya kilomita 20, yenye milima, mabonde na mikunjo kadhaa ya njia, ilikuwa na changamoto mbalimbali. Leo nataka nikusimulie changamoto moja ambayo ilikuwa kero kubwa wakati huo, si kwa Mwanakwetu pekee, bali pia kwa wanafunzi wengi waliokuwa wakitumia njia hiyo.

Tukiwa tunapita katika Bonde la Mzee Mafko na maeneo ya Shamba la Maua la Kadozo, tulikumbana na mmea mmoja maarufu kwa jina la MMAVIMAVI (Alsodeiopsis schumannii), pia unafahamika kama Mkaranga mwitu.

 

Mmea huu ulikuwa na majani yaliyotoa harufu mbaya inayofanana na kinyesi. Juu ya mmea huo kulikuwa na nzi wengi, hasa ulipokomaa na kutoa maua mengi ya rangi ya njano.

 

Nakumbuka vizuri kero iliyokuwa ikitukabili. Unapokuwa unapita katika njia iliyozungukwa na mmavimavi uliokomaa, ukaukanyaga vibaya au hata kujifutia katika majani yake, basi nguo zako zote zilikuwa zikijaa harufu mbaya kana kwamba umetoka chooni na kujipaka kinyesi mwili mzima!

 

Sasa, ili kuondokana na adha hiyo, ikiwa ungeukanyaga mmavimavi katika Bonde la Mzee Mafko, ulipofika eneo la Shamba la Maua la Kadozo, ilikulazimu kuvua nguo zako zote, ukabaki na chupi, kisha uzifue kwa kutumia sabuni maalumu tuliyokuwa tumeibeba katika mabegi yetu ya shule kando ya maji ya Mto Mzinga.

 

Baada ya kuzifua, ulizivaa zikiwa bado mbichi na kuendelea na safari huku zikikauka mwilini.

Wenzako wakikuuliza, "Mbona leo umevaa nguo mbichi?" unawajibu tu, "Nimeukanyaga mmavimavi!" Nao walikuwa wanaelewa vizuri sana shida yenyewe kwa sababu walikuwa wanaifahamu kero hiyo.

 

Lakini vipi ikiwa umekanyaga mmavimavi ukiwa tayari umepanda Mlima wa Mtoni Kijichi? Ni vigumu kurudi Mto Mzinga.

Hapo ilikuwa kazi nyingine! Ulibeba harufu hiyo hadi shuleni. Ulipofika, ulilazimika kupitia kwa Mama Ntilie ambaye tulikuwa tukinunua kwake chakula wakati wa mchana. Ungeomba maji na sabuni, naye angekupa ili ufue nguo zako. Baada ya kufua, ulizivaa zikiwa bado mbichi na kuingia darasani.

 

Wakati mwingine, hata kwenye mstari wa asubuhi hukuweza kusimama pamoja na wenzako. Na mwalimu alipokuuliza kwa nini umechelewa, ulimjibu kuwa ulikuwa ukifua nguo zako baada ya kuchafuliwa na mmea wa mmavimavi njiani. Walimu wa wakati huo walikuwa wanaifahamu vizuri changamoto hiyo.

 

Mwanakwetu hana hakika kama walimu wa leo katika maeneo ya Mbagala na Ikangao bado wanakumbana kero hii ya mmavimavi kutoka kwa wanafunzi wao.

Swali la kujiuliza ni hili: Kwa nini leo Mwanakwetu amekumbuka kisa hiki cha mmavimavi?

Mwanakwetu analinganisha kero ya mmea wa mmavimavi na hoja ya utawala wa kiimla.

 

Kwanza, usumbufu katika maisha ya kila siku. Mmavimavi uliwasababishia wanafunzi waliotumia njia ya Bonde la Mzee Mafko na Shamba la Maua la Kadozo usumbufu mkubwa. Mwanafunzi aliyeukanyaga alilazimika kuvumilia harufu mbaya, kufua nguo na kubadili utaratibu wake wa safari. Vivyo hivyo, udikteta huwasababishia wananchi usumbufu katika maisha yao kwa kuwanyima haki, uhuru na nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

 

Pili, upotevu wa muda na kudorora kwa shughuli za maendeleo. Wanafunzi waliokanyaga mmavimavi walipoteza muda wa masomo kwa kulazimika kutafuta maji na sabuni, kufua nguo na kuendelea na safari. Hali hii inafanana na udikteta, ambapo wananchi hutumia muda na nguvu nyingi kukabiliana na urasimu, vikwazo na mifumo isiyozingatia haki badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo.

 

Tatu, hofu na kukosekana kwa uhuru. Wanafunzi waliokuwa wakipita katika njia hiyo waliishi kwa wasiwasi wa kuukanyaga mmavimavi kutokana na madhara yake. Hali hii inafanana na maisha ya wananchi katika utawala wa kidikteta, ambapo baadhi yao huogopa kutoa maoni, kuikosoa serikali au kudai haki zao kwa kuhofia vitisho na hatua za kikatili kutoka kwa mamlaka.

 

Nne, kuvurugika kwa utaratibu wa maisha. Mmavimavi uliwalazimisha wanafunzi kubadili utaratibu wao wa kawaida wa kwenda shuleni na wakati mwingine kuchelewa kuingia darasani. Vivyo hivyo, udikteta unaweza kuzuia wananchi kutekeleza shughuli zao za kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa uhuru, hivyo kudhoofisha uzalishaji na maendeleo ya jamii.

Tano, wananchi kulazimika kutafuta msaada na kudai haki zao huku na kule. Mwanafunzi aliyeukanyaga mmavimavi alilazimika kuwaeleza wenzake sababu ya kuvaa nguo mbichi. Cha kusikitisha ni kwamba, licha ya walimu na wazazi kufahamu kero hiyo, hakuna aliyeonekana kuwajibika kuitafutia suluhisho la kudumu. Hali hii inaweza kulinganishwa na mazingira ya kidikteta, ambapo wananchi hulazimika kutafuta msaada na kupeleka malalamiko yao katika maeneo mbalimbali, hata nje ya mipaka ya nchi yao, ili haki zao zisikilizwe. Badala ya mamlaka kuwajibika na kushughulikia matatizo ya wananchi, wananchi hujikuta wakitumia nguvu nyingi kudai haki zao.

 

Sita, mmavimavi kama kikwazo kinachosambaa. Kadiri mmavimavi ulivyosambaa katika njia, ndivyo ulivyozidi kuwa kikwazo kwa wanafunzi. Hali hii inafanana na udikteta unapozikumba taasisi mbalimbali za nchi, kama vyombo vya habari, mahakama na mifumo ya uwajibikaji. Udhibiti wa taasisi hizo hudhoofisha demokrasia na kuwanyima wananchi nafasi ya kushiriki katika uongozi wa nchi yao.

Saba, umuhimu wa kutokata tamaa katika kukabiliana na changamoto. Licha ya usumbufu wa mmavimavi, wanafunzi hawakuacha kwenda shuleni. Walibuni mbinu za kukabiliana na tatizo hilo, ikiwemo kubeba sabuni na kutafuta maji ya kufulia. Hali hii inatukumbusha umuhimu wa wananchi kutumia njia za amani na za kisheria kudai haki, uhuru, uwajibikaji na utawala bora.

 

Kwa hiyo, kisa cha mmavimavi si kumbukumbu ya kawaida tu ya maisha ya Mwanakwetu alipokuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mtoni Kijichi, bali ni mfano unaoweza kutusaidia kuelewa madhara ya udikteta katika jamii.

Jamii haipaswi kuzoea mifumo inayozuia watu kustawi. Kama wanafunzi walivyotafuta njia za kukabiliana na mmavimavi ili waendelee na safari yao ya kutafuta elimu, ndivyo wananchi wanavyopaswa kuendelea kudai haki, uhuru, uwajibikaji na demokrasia kwa njia za amani na za kisheria.

 

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“KUTOKA BONDE LA MZEE MAFKO HADI KERO ZA UDIKTETA!”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments