.gif)
Adeladius Makwega – Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, DODOMA.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lina mpango wa kuanzisha makavazi katika baadhi ya Dayosisi zake ili kuweza kuhifadhi vizuri kumbukumbu zake.
Hayo yamebainika Novemba 17, 2026, katika ziara maalumu ya wataalamu wa kumbukumbu, maafisa TEHAMA, wakutubi, mchungaji na mwanateolojia kutoka kanisa hilo walipotembelea Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Wakizungumza katika viunga vya Makao Makuu ya Nyaraka na Kumbukumbu Dodoma, wataalamu hao walisema:
“Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, kila Dayosisi yake ina utajiri mkubwa wa Nyaraka na Kumbukumbu, hivyo sasa tumeamua kujikita katika kuboresha utendaji wetu kwa kiwango cha juu.”
Alisema Bi. Prisca Joachim, ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka Makao Makuu ya KKKT.
“Kanisa lina historia kubwa ya kutunza nyaraka zake tangu enzi na ndiyo maana Biblia imeweza kuwepo kwa miaka kadhaa sasa. Hata hivyo, sasa ni lazima tuwe na mazingira mazuri ya kuhifadhi nyaraka zetu kwa ajili ya wale wanaofanya kazi hii ya kueneza Neno.”
Alisema Mchungaji Avitius Momo.
Kwa upande wake, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliwapokea na kutoa ushirikiano kwa wageni hao. Aidha, wageni hao walifanya mazungumzo mafupi na wakurugenzi kadhaa, akiwamo Athanas Kolokota, Mkurugenzi wa Huduma za Nyaraka, pamoja na Ndugu Gaspari Kileo, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu.
Kutokana na ziara hiyo, yapo maswali kadhaa yanayobaki. Mosi, makavazi ni nini?
Mwanakwetu aliwasiliana na Bujo Boniface Ngwale, ambaye ni Afisa Kumbukumbu kutoka Ofis ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, na alisema:
“Makavazi ni nyaraka muhimu zinazohifadhiwa milele kwa ajili ya marejeo, tafiti na ushahidi wa baadaye. Pia, neno makavazi linamaanisha jengo au chumba chenye hadhi maalumu kinachotumika kuhifadhi nyaraka zenye thamani ya kuhifadhiwa milele.”
Je, ili uwe na makavazi unatakiwa kuwa na nini?
Bi Ngwale alisema:
“Unatakiwa kuwa na kumbukumbu, jengo, vifaa, mfumo na wataalamu. Kisha unafanya tathmini ili kubaini thamani ya kumbukumbu zinazopaswa kuharibiwa na zile zinazopaswa kuhifadhiwa milele. Zile zinazostahili kuhifadhiwa milele ndizo zinazohifadhiwa katika makavazi.”
Bi. Ngwale alitoa mifano ya nyaraka za kanisa zinazopaswa kuhifadhiwa katika makavazi:
“Katiba ya Dayosisi au Jimbo, hati za majengo yote ya kanisa, Biblia, vitabu vya mwongozo wa liturujia, ramani na michoro ya majengo, rejea za washirika kama vyeti vya ubatizo, kipaimara na ndoa, ripoti za kimisionari, ripoti za mikutano ya kanisa, magazeti na majarida ya kanisa.”
Jambo la kuzingatia ni kwamba nyaraka ni kumbukumbu, lakini si kila kumbukumbu ni nyaraka.
makwadeladius@gmail.com-0717649257

%20-%20Copy.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
.jpg)
%20-%20Copy.jpg)
.gif)
Post a Comment