KIPANDE CHA KARATASI CHENYE HISTORIA KUBWA

 

Adeladius Makwega


Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma

Miaka 65 iliyopita, kijana mmoja alikuwa na ndoto gani kuhusu maisha yake ya baadaye? Ni nini kilimfanya aandike barua kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma? Je, alikuwa akiomba msaada wa aina gani, na ndoto yake ilitimia?

Haya si maswali ya kubuni, bali ni maswali yanayopata majibu kupitia kipande kimoja cha karatasi kilichohifadhiwa katika kumbukumbu za Taifa. Barua hiyo, iliyoandikwa Oktoba 4, 1961 na kijana aliyejitambulisha kwa jina la E. Kivira, inatufungulia ukurasa wa historia ya kijana aliyekuwa na matumaini ya kupata mafunzo ya kuwa Msaidizi wa Tiba Vijijini.

 

Haya ni maswali kwako ya mapema Novemba 18, 2026, nikiwa katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma, nilikutana na Bi. Onesta Sendeya, Afisa Kumbukumbu katika Idara hiyo. Katika mazungumzo yetu, alinielekeza kwenye barua moja ya kihistoria iliyonifanya nisitishe kwa muda fikra zangu na kujiuliza maswali mengi kuhusu maisha ya vijana wa Tanganyika miaka ya 1960. Nilipoitazama barua hiyo, jambo la kwanza lililonivutia lilikuwa ya Oktoba 4, 1961. Ilikuwa imeandikwa kwa mkono, katika kipindi ambacho Tanganyika ilikuwa imebakiza miezi michache tu kabla ya kupata uhuru wake, Desemba 9, 1961. Lakini zaidi ya tarehe hiyo, kilichonivutia ni maudhui yake. Ilikuwa barua ya kijana mwenye umri wa miaka 20 aliyekuwa akitafuta nafasi ya kujenga maisha yake kupitia elimu na taaluma ya afya.

 

Bi. Onesta Sendeya alifafanua kuwa barua hiyo iliandikwa na kijana aliyejitambulisha kwa jina la E. Kivira, akimwandikia Mkuu wa Wilaya wa Dodoma (District Commissioner). Lengo lake lilikuwa kuomba nafasi ya kupata mafunzo ya kuwa Rural Medical Aid, yaani Msaidizi wa Tiba Vijijini.

 

Nilipoendelea kuisoma, niligundua kuwa kijana huyu hakuwa amekaa tu na kuandika ombi bila sababu. Alikuwa na historia ya elimu na alikuwa tayari amechukua hatua kadhaa katika kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.

 

Katika barua yake, Kivira alieleza kuwa alikuwa ameshauriwa na Mganga Mkuu wa Mkoa (Provincial Medical Officer), kupitia barua yenye kumbukumbu DA/61/37 ya Septemba 8, 1961 kutoka Arusha, kuwasilisha maombi yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.

 

Alieleza pia kuwa alimaliza masomo ya Standard VIII katika Kidia Middle School. Baadaye alisafiri kwenda Uganda, ambako aliendelea na masomo katika shule aliyoitaja kama Kabale Busoga Secondary School. Huko alikamilisha kiwango cha masomo alichokitaja kama Senior (S.4), na akaeleza kuwa alifaulu mitihani ya Uganda Senior Secondary Entrance Examination pamoja na Junior Secondary Leaving Examination.

 

Katika kujitambulisha kwake, alieleza kuwa alikuwa Mchagga mwenye umri wa miaka 20. Baada ya kuweka wazi historia yake ya elimu, alieleza nia yake ya kupata nafasi ya mafunzo ya kuwa Msaidizi wa Tiba Vijijini katika mwaka uliofuata.

 

Hapo ndipo nilipojiuliza: Kijana huyu alikuwa na ndoto gani? Alikuwa akitazamia maisha gani baada ya kupata mafunzo hayo? Je, alikuwa akifikiria namna ambavyo angeweza kutumia taaluma hiyo kusaidia watu wa vijijini ambao huenda walikuwa na changamoto ya kupata huduma za afya?

 

Hakika, hatuwezi kujibu maswali hayo kwa kutegemea barua hii pekee. Wala hatujui kama alipata nafasi aliyoomba, kama alihitimu mafunzo au maisha yake yaliendeleaje. Hayo yanahitaji kumbukumbu nyingine za kihistoria. Hata hivyo, jambo moja liko wazi: kijana huyu alikuwa na lengo, alitafuta taarifa, alifuata ushauri na akachukua hatua ili kufikia ndoto yake.

 

Mwanakwetu, unapoangalia barua hii baada ya miaka 65, ni vigumu kutokujifunza jambo. Kwanza, inatukumbusha thamani ya elimu. Kivira hakuridhika na elimu ya msingi; aliendelea na masomo hadi Uganda ili kuongeza maarifa yake. Hii inatufundisha kuwa elimu si suala la kutafuta cheti pekee, bali ni safari ya kujenga uwezo, kupanua upeo wa fikra na kujiandaa kukabiliana na changamoto za maisha.

 

Pili, barua hii inatukumbusha kuwa fursa hazipaswi kusubiriwa tu, bali zinapaswa kutafutwa. Kijana huyu hakukaa akisubiri maisha yajipange yenyewe. Alipopata ushauri kutoka kwa mamlaka ya afya, aliufanyia kazi na kuandika maombi yake. Huu ni mfano unaopaswa kuwafikirisha vijana wa leo ambao wakati mwingine hukata tamaa wanapokosa ajira au nafasi za kujiendeleza. Kutafuta taarifa, kujenga mahusiano ya kitaaluma, kufuata taratibu na kuomba nafasi ni sehemu ya safari ya maendeleo.

 

Jambo jingine linalovutia ni namna alivyoandika barua yake. Alieleza sababu ya kuandika, akataja rejea ya barua aliyokuwa ameipokea, akaweka historia yake ya elimu na kuwasilisha ombi lake kwa lugha ya heshima. Hii inatukumbusha umuhimu wa mawasiliano rasmi na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha. Katika kipindi hiki ambacho teknolojia imerahisisha mawasiliano, bado tunahitaji kuzingatia weledi, mpangilio na heshima katika kuwasiliana.

 

Pia, safari ya Kivira kwenda Uganda kutafuta elimu inatufundisha kuwa maarifa hayana mipaka ya kijiografia. Miaka hiyo, kijana kutoka Tanganyika aliweza kuvuka mpaka kutafuta elimu na baadaye kurejea kutafuta nafasi ya mafunzo ya taaluma ya afya nyumbani. Huu ni mfano unaotukumbusha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, kubadilishana maarifa na kutumia fursa zinazopatikana katika nchi nyingine.

Zaidi ya yote, ombi lake la mafunzo ya afya linatufanya tutafakari kuhusu nafasi ya vijana katika maendeleo ya jamii. Taaluma ya afya ina umuhimu mkubwa kwa maisha ya wananchi, hasa wale wanaoishi vijijini. Kwa hiyo, kutafuta mafunzo katika eneo hilo ni jambo linalotupa nafasi ya kutafakari namna elimu na taaluma vinavyoweza kuwa nyenzo ya kuwahudumia wengine. Vijana wa leo wanapaswa kutambua kuwa mafanikio ya kweli hayapimwi kwa mafanikio binafsi pekee, bali pia kwa mchango unaotolewa kwa jamii.

 

Lakini kuna jambo jingine ambalo huenda wengi wasilione kwa haraka. Barua hii yenyewe ni ushahidi wa umuhimu wa kutunza kumbukumbu. Fikiria kama barua hii isingehifadhiwa. Je, tungekuwa na nafasi ya kujua kuwa mwaka 1961 kulikuwa na kijana wa miaka 20 aliyekuwa akitafuta nafasi ya mafunzo ya afya kwa kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma? Huenda simulizi hii isingefika kwetu.

Ndiyo maana nyaraka za kihistoria zina thamani kubwa. Barua, picha, vyeti na kumbukumbu nyingine ambazo wakati mwingine huonekana kuwa vitu vya kawaida, baadaye hugeuka kuwa hazina kwa watafiti, wanahistoria na vizazi vijavyo. Kupitia nyaraka hizi tunaweza kuelewa mifumo ya elimu, utawala, ajira, mawasiliano na maendeleo ya taaluma katika nyakati zilizopita.

 

Sasa hebu tujiulize: Miaka 65 iliyopita, kijana wa miaka 20 alikuwa akitumia kalamu na karatasi kuomba nafasi ya mafunzo ya afya. Leo, mwaka 2026, vijana wana teknolojia, intaneti, vyuo vingi, taarifa za haraka na fursa nyingi zaidi za kujifunza ndani na nje ya nchi. Lakini je, tunatumia fursa hizi kwa kiwango kinachostahili?

 

Je, vijana wetu wana bidii ya kutafuta maarifa kama walivyokuwa wakifanya vijana wa zamani? Je, tunaandaa vijana wenye dhamira ya kutumia taaluma zao kutatua changamoto za jamii? Je, tunathamini elimu tuliyo nayo na nafasi tunazozipata? Na zaidi ya yote, je, tunatambua wajibu wetu katika kuandika historia ambayo vizazi vijavyo vitaisoma?

 

 

Kwa mtazamo wangu, barua ya E. Kivira ya Oktoba 4, 1961 si karatasi ya zamani tu. Ni kioo kinachoturudisha kwenye kipindi muhimu cha historia ya Tanganyika na kutufanya tutafakari kuhusu safari ya maendeleo ya taifa letu. Ni ushahidi kuwa nyuma ya kila nyaraka kunaweza kuwa na ndoto, juhudi, matarajio na simulizi inayostahili kusimuliwa.

Mwanakwetu, historia si kumbukumbu ya yaliyopita pekee; ni mwalimu wa kutuongoza katika maamuzi ya leo na kesho. Maendeleo ya taifa hayajengwi na viongozi pekee. Yanajengwa pia na vijana wenye maono, wataalamu wenye uadilifu, watumishi wenye moyo wa kujitolea na wananchi wanaotumia maarifa yao kwa manufaa ya jamii.

Ikiwa kijana wa miaka 20 mwaka 1961 aliona umuhimu wa kutafuta elimu na kuomba nafasi ya mafunzo ya afya, sisi wa mwaka 2026 tunafanya nini kwa kutumia fursa nyingi tulizonazo?

Mwanakwetu, upo? Kumbuka,

“KIPANDE CHA KARATASI CHENYE HISTORIA KUBWA.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
-0717649257


















s



 




0/Post a Comment/Comments