Adeladius Makwega – MBAGALA
“Ati baba, mbona kwenye bega lako la kushoto na la kulia kuna alama? Je, uliumia?”
Hilo lilikuwa swali la Joshua, kijana mwenye umri wa miaka 11 mwaka 2026, akimuuliza baba yake wakati walipokuwa wamepumzika katika kibanda chao shambani. Baba na mwana walikuwa wamekwenda kupanda mahindi katika shamba lao dogo la nyumbani.
Baba alikuwa amevalia mabuti ya shambani, suruali nyeusi na jaketi jeusi. Aliposikia swali hilo, alitambua kuwa amepata fursa ya kumweleza mwanawe historia iliyojificha nyuma ya makovu yaliyokuwa kwenye mabega yake.
“Hizi ni alama za chanjo ya ndui, mwanangu. Ni makovu yanayoweza kubaki kwenye ngozi baada ya mtu kuchanjwa dhidi ya ugonjwa huo. Zamani, chanjo ya ndui ilikuwa ikitolewa kwa kuchanja ngozi kwa kutumia kifaa maalumu, na sehemu iliyochanjwa ingeweza kuacha kovu la kudumu.
Ndui ilikuwa ugonjwa hatari sana wa kuambukiza uliosababishwa na virusi vinavyojulikana kama Variola. Ugonjwa huo uliwahi kusababisha vifo vya mamilioni ya watu duniani. Inakadiriwa kuwa katika karne ya 20 pekee, ndui ilisababisha vifo vya takribani watu milioni 300. Takribani mtu mmoja kati ya watatu walioambukizwa aliweza kufariki dunia.
Hata hivyo, kutokana na juhudi kubwa za chanjo, ushirikiano wa kimataifa na hatua mbalimbali za afya ya umma, dunia hatimaye ilifanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo.”
Joshua, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne, aliendelea kumsikiliza baba yake kwa makini.
“Sasa baba, kama usingepata chanjo hii, pengine hata sisi tusingezaliwa?”
Baba yake, Mwanakwetu, akamjibu:
“Ndiyo mwanangu. Chanjo ilikuwa moja ya silaha muhimu katika kulinda maisha ya watu dhidi ya ugonjwa huo. Watu wengi waliokuwepo katika kizazi cha babu na bibi zetu walishuhudia athari za ndui. Kwa hiyo, mafanikio ya chanjo yalikuwa na umuhimu mkubwa kwa maisha ya vizazi vilivyofuata.”
Joshua akauliza tena:
“Nikiumwa malaria natapika, nasikia baridi na ninakosa hamu ya kula. Sasa dalili za ugonjwa wa ndui zilikuwa zipi?”
Mwanakwetu akamjibu:
“Mwanangu, ndui ilikuwa na dalili mbalimbali. Kwa kawaida, dalili zilianza kuonekana kati ya siku 7 na 17 baada ya mtu kuambukizwa virusi vya Variola.
Katika hatua ya awali, mgonjwa alipata homa kali ghafla, uchovu mwingi, maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo na wakati mwingine kutapika.
Baadaye, vidonda vilianza kujitokeza ndani ya mdomo na kooni. Upele ulianza kuonekana usoni na kisha kusambaa sehemu nyingine za mwili, ikiwemo mikono, miguu, viganja na nyayo.
Kadiri siku zilivyopita, vipele vilibadilika na kuwa na majimaji, baadaye vikakauka na kuacha makovu kwa baadhi ya wagonjwa waliopona.
Huo ndio ulikuwa miongoni mwa upekee wa ugonjwa huo. Mtu aliyepona angeweza kubaki na makovu yaliyokuwa ushahidi wa historia ya ugonjwa aliowahi kuugua.”
Joshua Makwega alikuwa msikivu sana. Baada ya maelezo hayo, akauliza:
“Sasa baba, mbona sisi hatuna makovu haya? Maana na sisi tunapenda kuishi. Je, tutakuwa salama?”
Mwanakwetu akamjibu:
“Mwanangu, duniani kwa sasa ndui ya binadamu imetokomezwa rasmi. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kutokomezwa kwake mwaka 1980, baada ya kisa cha mwisho cha maambukizi ya kawaida kuripotiwa nchini Somalia mwaka 1977.
Hata hivyo, usichanganye kovu la chanjo ya ndui na kovu la chanjo ya BCG inayotolewa kwa ajili ya kinga dhidi ya kifua kikuu. Chanjo ya BCG pia inaweza kuacha kovu kwenye sehemu ya juu ya mkono. Kwa hiyo, mtu mwenye kovu hilo si lazima awe amechanjwa dhidi ya ndui.”
Baba aliendelea kumweleza mwanawe:
“Mwanangu, katika mapambano haya Tanzania haikujitenga na dunia. Nchi yetu ilishiriki katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa ndui kupitia kampeni za chanjo, ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na uhamasishaji wa wananchi.
Baada ya uhuru, mapambano haya yaliendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha afya za wananchi. Mwaka 1967, WHO iliongeza kasi ya mpango wa kimataifa wa kutokomeza ndui. Tanzania nayo ilishiriki katika kampeni za chanjo zilizolenga kuwafikia wananchi wengi, zikiwemo kampeni zilizoanza mwaka 1968 katika Tanzania Bara.
Katika kampeni hizo, zilitumika chanjo maalumu zilizohifadhiwa katika hali ya kugandishwa (freeze-dried vaccine) pamoja na sindano maalumu zilizojulikana kama bifurcated needles.
Mafanikio hayo yalihitaji zaidi ya wataalamu wa afya. Yalihitaji ushirikiano wa viongozi, watumishi wa serikali na wananchi wenyewe. Elimu ya afya kwa umma, uhamasishaji wa jamii na mifumo ya kiutawala, ikiwemo mfumo wa nyumba kumi kumi, vilikuwa muhimu katika kuwafikia wananchi wengi.
Katika kipindi hicho, viongozi mbalimbali wa serikali na sekta ya afya walishiriki katika kusimamia na kuendeleza huduma za afya nchini. Miongoni mwa majina yanayostahili kukumbukwa katika historia ya uongozi wa taifa katika kipindi hicho ni Profesa Abdulrahman Mohammed Babu, Austin Kapere Edward Shaba na Bi. Lucy Lameck.
“Wanawake nao hawakuwa nyuma katika maendeleo ya taifa. Bi. Lucy Lameck alikuwa miongoni mwa wanawake waliopata nafasi za uongozi katika serikali ya Tanganyika na baadaye Tanzania. Uzoefu wake katika taaluma ya uuguzi ni sehemu muhimu ya historia yake ya utumishi wa umma.
Pamoja na hayo, mapambano dhidi ya ndui yalihusisha wauguzi, matabibu, wakaguzi wa afya na watumishi wengine waliokuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi.
Mamlaka za afya zilitumia hatua mbalimbali, zikiwemo kutenga wagonjwa, kufuatilia maeneo yaliyokuwa na milipuko na kutoa elimu ya kuzuia maambukizi. Hata hivyo, kulikuwa na changamoto za usafiri, kufikia maeneo ya mbali, masuala ya kiutawala na baadhi ya mitazamo ya kitamaduni iliyohitaji kuelimishwa.”
Hapo ndipo Joshua alipogundua kuwa alama alizokuwa akiziona kwenye mabega ya baba yake hazikuwa makovu ya kawaida tu. Zilibeba historia ya mapambano ya binadamu dhidi ya ugonjwa uliowahi kuitikisa dunia.
Mwanakwetu naye alitambua kuwa mazungumzo hayo yalikuwa zaidi ya kumjibu mtoto swali kuhusu kovu. Yalikuwa nafasi ya kumfundisha mwanawe historia ya afya ya binadamu na umuhimu wa kutambua mchango wa vizazi vilivyotangulia.
Wakiwa bado shambani, radi kubwa ilisikika angani na muda mfupi baadaye mvua ilianza kunyesha. Ugali uliletwa, baba na mwana wakala, kisha wakarejea shambani kuendelea na shughuli yao ya kupanda mahindi.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika, haya ni mazungumzo baina ya baba na mwana kuhusu ugonjwa wa ndui. Joshua Makwega, aliyezaliwa mwaka 2015, hakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu ugonjwa huo ambao uliwahi kuwa tishio kubwa kwa maisha ya binadamu duniani.
Mazungumzo hayo yanatoa taswira ya namna dunia ilivyopambana na ugonjwa huo kwa kutumia elimu, chanjo, ushirikiano wa kimataifa na mifumo ya afya ya umma.
Kovu la chanjo ya ndui kwenye bega la baadhi ya watu walio hai hadi leo ni kumbukumbu ya kipindi ambacho dunia ilipambana na ugonjwa huo na hatimaye kuushinda.
Lakini Mwanakwetu anaamini kuwa historia hiyo haipaswi kubaki kwenye mabega ya wazazi na babu zetu pekee. Inapaswa kufika pia kwa watoto na vijana ambao hawakushuhudia kipindi hicho.
Katika mazungumzo yake na Joshua, Mwanakwetu alieleza umuhimu wa viongozi, wataalamu wa afya, wauguzi, matabibu, wakaguzi wa afya na watumishi wengine wa umma waliokuwa sehemu ya mapambano dhidi ya magonjwa nchini.
Hata hivyo, historia hii haipaswi kusimuliwa kwa maneno pekee. Inahitaji pia ushahidi wa nyaraka.
Miongoni mwa ushahidi huo ni nyaraka ya Novemba 9, 1961 kutoka Mvumi, Wilaya ya Dodoma. Nyaraka hiyo, yenye muhuri wa Mahakama ya Mitaa ya Mvumi (Local Court, Mvumi), inaonyesha taarifa iliyotumwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuhusu kutokea kwa ugonjwa wa ndui katika eneo hilo.
Mwandishi wa barua hiyo alieleza kuwa ugonjwa wa ndui ulikuwa umetokea katika eneo lao na kuwasilisha taarifa hiyo kwa mamlaka ya wilaya. Pia kuna maandishi yanayoonyesha kuwa Mkaguzi wa Afya (Health Inspector) alitakiwa kufahamishwa.
Hii ni nyaraka yenye umuhimu wa kihistoria kwa sababu inatupa taswira ya namna taarifa za milipuko ya magonjwa zilivyokuwa zikifikishwa kwa mamlaka za serikali katika kipindi cha Tanganyika.
Kwa Mwanakwetu, karatasi hiyo si karatasi ya zamani tu. Ni ushahidi unaotukumbusha kuwa mapambano dhidi ya magonjwa yana historia yake, yana wahusika wake na yana kumbukumbu zinazopaswa kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Nyaraka za aina hii zinapaswa kutunzwa kwa umakini kwa sababu zinaweza kusaidia watafiti, wanahistoria, wanafunzi na wananchi kuelewa namna serikali na jamii zilivyokabiliana na changamoto mbalimbali za afya katika vipindi tofauti.
Tunapoadhimisha miaka 65 tangu uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, ni muhimu pia kuikumbuka historia ya mapambano ya kulinda afya za wananchi. Uhuru haukuwa tu mwanzo wa safari ya kisiasa na kiutawala; ulikuwa pia mwanzo wa safari ya kujenga taifa lenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii, kiuchumi na kiafya.
Na pengine, moja ya masomo makubwa tunayoweza kujifunza kutokana na historia ya ndui ni kwamba matatizo makubwa yanayolikabili taifa yanaweza kushindwa pale kunapokuwa na maarifa, uongozi, ushirikiano na dhamira ya pamoja.
Kovu lililo kwenye bega la baba linaweza kuwa somo kwa mwana. Nyaraka iliyohifadhiwa kwa zaidi ya miongo sita inaweza kuwa somo kwa taifa zima.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka:
ALAMA YA CHANJO YA NDUI KATIKA BEGA LA BABA
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
TANBIHI: Makala haya ni maalumu kwa heshima ya miaka 65 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, yakikumbusha historia ya mapambano ya kulinda afya za binadamu na umuhimu wa kuhifadhi nyaraka za taifa.
.gif)















.gif)
.gif)


Post a Comment