Adeladius Makwega
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma
Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, wamehimizwa kuwa makini katika kulinda taarifa zao binafsi ili kuepuka matumizi yasiyoruhusiwa ya taarifa hizo yanayoweza kuwasababishia matatizo.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo maalumu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyofanyika jijini Dodoma, yakilenga kuongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu umuhimu wa usalama wa taarifa na matumizi sahihi ya teknolojia.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Afisa Utumishi Mkuu, Bi. Happiness Masija, alisema kuwa si salama kwa taarifa binafsi za mtu kuwekwa wazi kwa kila mtu, kwa kuwa zinaweza kutumiwa vibaya na watu wenye nia ovu.
“Haiwezekani kila mtu ajue namba yako ya hundi ya mshahara, kila mtu ajue hata kundi lako la damu. Hii ni hatari; jamani, tuwe makini,” alisisitiza Bi. Masija.
Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi, Bi. Masija alitoa mfano wa mama mmoja aliyejifungua mtoto na kumnunulia nguo nzuri. Baada ya kumvisha mtoto nguo hizo, mama huyo alipiga picha na kuisambaza katika mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa mfano huo, mfanyabiashara aliyeuza nguo hizo aliona picha ya mtoto huyo, akaamua kuitumia na kuisambaza zaidi kwa ajili ya kutangaza biashara yake. Picha hiyo ilipata umaarufu mkubwa na kumsaidia mfanyabiashara huyo kupata wateja wengi.
Hata hivyo, mama wa mtoto alipoona picha ya mtoto wake ikitumika katika tangazo la biashara bila ridhaa yake, alikasirika na kulalamika kuhusu matumizi hayo.
Kisa hicho kilitumika kuonesha umuhimu wa kuzingatia faragha na kupata ridhaa inayofaa kabla ya kutumia picha au taarifa binafsi za watu kwa madhumuni mengine, hususan katika shughuli za kibiashara.
Bi. Masija alisisitiza kuwa wafanyakazi wanapaswa kuwa waangalifu wanaposhiriki taarifa zao au za watu wengine katika mitandao ya kijamii.
Awali, katika mafunzo hayo, mwezeshaji Ally Ally alieleza maana ya ulinzi wa taarifa binafsi (Personal Data Protection au Data Privacy), akibainisha kuwa ni hatua na taratibu zinazolenga kulinda taarifa zinazoweza kumtambulisha mtu dhidi ya matumizi yasiyoruhusiwa, wizi, uharibifu au ufikiaji usioidhinishwa.
Alifafanua kuwa taarifa hizo zinaweza kuhifadhiwa katika mifumo ya kidijitali, kama vile kompyuta na mitandao, au katika nyaraka za karatasi.
Miongoni mwa taarifa binafsi alizozitaja ni: Majina na taarifa za kuzaliwa: Jina kamili na tarehe ya kuzaliwa. Namba za utambulisho: Namba ya NIDA, pasipoti au leseni ya udereva.
Taarifa za mawasiliano: Namba ya simu, barua pepe na anwani ya makazi.Taarifa za kifedha: Namba za akaunti za benki na taarifa za kadi za malipo.Taarifa za afya: Rekodi za matibabu na taarifa nyingine za kiafya.Taarifa za kibayometria: Alama za vidole na taarifa zinazotokana na sifa za kipekee za mwili, kama vile sura.
Mafunzo hayo yalieleza kuwa ukusanyaji na matumizi ya taarifa binafsi vinapaswa kuwa na msingi halali na kuzingatia masharti ya sheria husika. Taarifa zinapaswa kukusanywa kwa madhumuni maalumu na kutumiwa kwa namna inayolingana na madhumuni hayo.
Aidha, taasisi zinazokusanya na kuhifadhi taarifa za watu, zikiwemo benki, kampuni za simu na hospitali, zinapaswa kuweka mifumo na hatua stahiki za kiusalama ili kuzuia ufikiaji usioidhinishwa, udukuzi na uvujaji wa taarifa.
Washiriki pia walielezwa kuhusu umuhimu wa haki za watu kuhusiana na taarifa zao, ikiwemo kuomba taarifa zenye makosa zirekebishwe na kuwasilisha maombi ya kufutwa kwa taarifa pale ambapo sheria inaruhusu.
Mwandishi wa makala haya, akitafakari maudhui ya mafunzo hayo, alikumbuka kisa cha mtumishi mmoja wa kike aliyekuwa ameachana na mume wake. Baada ya talaka, mtumishi huyo aliamua kuwasilisha nyaraka zinazohusiana na talaka hiyo kwa mwajiri wake ili kusasisha taarifa zake za hali ya ndoa.
Alipoulizwa sababu ya kumjulisha mwajiri wake kuhusu mabadiliko hayo, alieleza kuwa alifanya hivyo kwa nia njema, akiamini kuwa ni muhimu taarifa zake binafsi ziwe sahihi na za sasa.
“Ninamjulisha mwajiri kwa nia njema, maana hali yangu ya ndoa ikibaki kuonesha kuwa bado nina ndoa wakati tayari tumeachana, kunaweza kutokea kifo au jambo jingine baya na aliyekuwa mwenza wangu akanufaika kutokana na taarifa hizo. Hivyo, kuna umuhimu wa kumjulisha mwajiri na kuhuisha taarifa binafsi,” alieleza.
Kisa hicho kinaonesha umuhimu wa kuhakikisha kuwa taarifa zilizopo katika kumbukumbu za waajiri ni sahihi na zinasasishwa kunapotokea mabadiliko muhimu ya hali ya mtumishi.
Hata hivyo, taarifa zinazohitajika na taratibu za kuzisasisha zinapaswa kuzingatia sheria na kanuni za taasisi husika.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa kupitia Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yalihusisha mada mbalimbali zilizolenga kuongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu matumizi ya teknolojia, usalama wa taarifa na umuhimu wa kulinda taarifa binafsi katika mazingira ya kazi na maisha ya kila siku.
Nchini Tanzania, masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi yanasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Na. 11 ya mwaka 2022, kupitia Kamisheni ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC). Sheria hiyo inaweka mfumo wa kisheria wa kulinda taarifa binafsi na kusimamia namna zinavyokusanywa, kuchakatwa, kuhifadhiwa na kutumiwa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwasaidia wafanyakazi kuongeza umakini katika utunzaji wa taarifa zao binafsi na kutambua wajibu wa kulinda taarifa za watu wengine.
makwadeladius@gmail.com- 0717649257

Post a Comment