PAULINE GEKUL WA MWAKA 2010

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Siku ya leo, Mwanakwetu anaamua kulifunga suala la Mheshimiwa Pauline Gekul, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa akiwa Mbunge wa Babati na awali akiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Hata hivyo, naweka wazi kwamba endapo mtu yeyote atakuja na hoja kuhusu suala hili, nitasimama hadharani na kujibu hoja hizo bila mashaka yoyote.

 

Awali ya yote, naomba niweke wazi kwamba miongoni mwa wadau ambao wamekuwa wakiwasiliana nami kila ninapoandika makala kuhusu Pauline Gekul ni Wakili Tadey Lister Mlemeta. Amekuwa akitoa hoja zake, na miongoni mwa hoja hizo ni hii:

 

“Huyu dada amenifanyia mabaya sana nikiwa mgombea wa CHADEMA.”

 

Mwanakwetu anapokea maoni haya kwa mikono miwili. Ninaamini kwamba hata Mheshimiwa Gekul mwenyewe ameyasoma. Ikiwa kuna ukweli katika maelezo hayo, naamini Mheshimiwa Gekul anatambua jambo la kufanya, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ndugu Mlemeta ili wazungumze na kuweka mambo sawa.

 

Mwanakwetu anaamini kwamba hakuna binadamu aliyekamilika; kila mmoja ana mapungufu yake.

 

“Inawezekana Pauline Gekul akawa na hili, na mimi Mwanakwetu wa Mbagala nikawa na lile, huku mdogo wangu Tadey Lister Mlemeta naye akiwa na lake. Huo ndiyo ubinadamu.”

 

Kupitia makala haya, Mwanakwetu anamuomba ndugu Tadey Lister Mlemeta kwamba itakuwa vizuri yeye na Pauline Gekul kusameheana kwa yaliyopita.

 

Uhusiano wangu na Wakili Tadey Lister Mlemeta

Ili kuweka bayana jambo hili, naomba ifahamike kwamba Wakili Tadey Lister Mlemeta ni mdogo wangu wa damu. Yeye ni mtoto wa mjomba wangu mkubwa, anayefahamika kwa jina la Lister Samweli Mlemeta, ambaye ni mfamasia mstaafu.

 

Babu yake Wakili Tadey Mlemeta, Muwaha Samweli Tadey Mlemeta, alizaliwa tumbo moja na babu yangu, Hezron Tadey Mlemeta. Babu yangu Hezron alimzaa mama yangu, Doroth Hezron Tadey Mlemeta.

 

Kwa faida ya msomaji wangu, fahamu kwamba jina Tadey, analotumia Wakili Tadey, ni jina la baba wa babu yake, Muwaha Samweli Tadey Mlemeta.

Pauline Gekul ni dada wa watu wa Babati

 

Kwa watu wa Babati, ni muhimu kutambua kwamba Bi. Pauline Gekul ni dada yenu na mama yetu. Alipokuwa Naibu Waziri, alikuwa akitumikia umma wa Watanzania.

 

Ni katika utumishi huo wa umma ndipo akina Mwanakwetu tulipopata nafasi ya kumfahamu. Jambo hili ni muhimu kulielewa.

 

Pauline Gekul, kama dada wa wana wa Babati, ana mapungufu ya kibinadamu kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Kwa hakika, hata mimi Mwanakwetu wa Mbagala, pamoja na ndugu zangu wa Ikangao Ketaketa, nina dada wengi ambao nimekua nao na ninafahamu mapungufu yao. Hata hivyo, siwezi kutumia mapungufu ya dada zangu kuwaangamiza.

 

Badala yake, tutumie mapungufu ya ndugu zetu kama fursa ya kuwasaidia kujirekebisha, kujenga maeneo yetu na kuijenga Tanzania kwa ujumla.

 

Mazuri aliyoyafanya Pauline Gekul kama kiongozi wa kitaifa ni mengi. Wazee wa Babati wana wajibu wa kutambua mchango huo na kutafuta namna ya kutatua changamoto zinazomkabili mwanasiasa huyu.

 

Hivi ndivyo wazee wa Mbagala na wa Ikangao Mahenge wanavyokaa pamoja na ndugu yao Mwanakwetu.

 

“Rais anapofanya uteuzi au kumwondoa mmoja wetu katika nafasi ya uongozi, maana yake ni kwamba fursa ya ndugu yenu kuwawakilisha inapotea, na hakuna uhakika kwamba fursa hiyo itarudi tena kwenu. Hapo mmekula wa chuya.”

 

Kwa wanaonitukana kila ninapoandika kuhusu Pauline Gekul

Neno langu la mwisho kwa leo ni kwa wale wanaonitukana kila ninapoandika makala kuhusu Pauline Gekul. Najua mnasema mengi, yakiwemo haya:

 

“Oh, Mwanakwetu anapenda wanawake weupe!”

“Oh, yule Mwanakwetu, Pauline ni mpenzi wake!”

“Oh, Mwanakwetu kapewa pesa nyingi za hongo ili amsafishe!”

Jamani, niseme wazi kwamba Pauline nimefanya naye kazi, lakini hata namba yake ya simu sina.

 

Niseme wazi kwamba Pauline hajawahi kunipa chochote. Vilevile, sijawahi hata kumtamani , jamani angaliene hata namna mnayonisingizia.

Kwa hakika, Bi. Pauline Gekul namfahamu kwa karibu tangu alipokuwa Mbunge wa CHADEMA mwaka 2015. Nilipata kumwona kwa karibu katika vipindi vya Bunge, hasa kipindi cha “Lile Lililoleta Mjadala” kilichokuwa kikirushwa na TBC Taifa, kabla ya Bunge kuiondolea TBC haki hiyo.

 

Wakati huo, Pauline Gekul alikuwa binti mrembo na kijana kabisa.

 

“Kama sikutia neno la mapenzi wakati huo, jamani, nitie neno hilo leo hii? Natambua kwamba Pauline Gekul ameolewa, na hata mimi nina mke.”

 

Wana Babati, mlindeni dada yenu

Mwanakwetu nasema wazi kwamba kwa wana Babati, ni vizuri kuhakikisha kuwa dada yenu Pauline Gekul anafanya siasa kwa njia nzuri huku mkimlinda na kumsaidia kukabiliana na changamoto zinazomkabili.

Endapo mtashindwa kufanya hivyo, Mwanakwetu ninatoa kauli yangu hadharani:

 

“Pauline Gekul nitamuhamishia kwetu Mbagala, Dar es Salaam, akale kamba kochi, au nimhamishie kwetu Ikangao Mahenge, Morogoro, akale kambale wa Mto Luhombero. Nina hakika kwamba kamba kochi wa Mbagala na kambale wa Mto Luhombero wakimfikia Binti Gekul, akala tu atapendeza zaidi, maana samaki hawa wana protini nyingi. Akila samaki hao, Pauline Gekul atakuwa kama alivyokuwa mwaka 2010. Nawaombeni, msimkondeshe Bi. Pauline Gekul.”

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

PAULINE GEKUL WA MWAKA 2010.

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com 0717649257

 







































 

 

0/Post a Comment/Comments