Adeladius Makwega — Mbagala
Katika siasa, kelele si hoja, picha si ushahidi, na kurudia jambo mara nyingi hakulifanyi kuwa kweli.
Siasa zinapokuwa na afya, mtu hapaswi kupimwa kwa idadi ya picha anazotengeneza dhidi ya mpinzani wake, bali kwa uzito wa hoja anazoweka mezani.
Hapo ndipo mjadala kuhusu Mwigulu Lameck Nchemba unapopaswa kuanzia.
Mwigulu si jina lililoibuka jana. Ni mwanasiasa mwenye historia katika Bunge na Serikali, hivyo kumkosoa ni haki. Na mimi, Mwanakwetu, nimemkosoa mara nyingi pale nilipoona sababu ya kufanya hivyo.
Kumtetea hakumaanishi kwamba hana makosa.
Mwigulu si malaika. Ni mwanadamu na kiongozi anayepaswa kuwajibika kwa maamuzi yake.
Historia ya uongozi wa Tanzania pia inaonyesha kuwa viongozi wamewahi kuwajibishwa kisiasa na kiutendaji. Kwa hiyo, kumtetea Mwigulu hakumaanishi kufuta kumbukumbu wala kufumba macho mbele ya makosa.
Lakini kama kuna hoja dhidi yake, iwe hoja.
Siyo vikaragosi. Siyo mwanasesere. Siyo picha za kutengenezwa. Siyo video za kumdhalilisha mtu.
“Huyu ni baba mwenye watoto, mwanamme mwenye mke, mtu mwenye mashemaji lakini pia ni kiongozi wa jamii ya watu zaidi mmoja na mpaka sasa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Kama kuna sera inayopingwa, itajwe. Kama kuna uamuzi unaohojiwa, utajwe. Kama kuna takwimu zinazopingwa, leta takwimu mbadala. Kama kuna kosa, leta ushahidi, siyo vikaragosi.
Hoja ipigane na hoja. Ushahidi ujibu ushahidi. Rekodi ijibu rekodi.
Mwigulu anatoka Singida, lakini anapokuwa katika uongozi wa kitaifa, anawajibika kwa Tanzania nzima. Kwa hiyo, mjadala wake usijengwe kwa ukanda, chuki au hisia; ujengwe kwa kazi, sera, maamuzi, matokeo na uwajibikaji.
Na kama unatoka kibakulini ukitaka kupambana na mtu wa sinia, usije na vitisho.
Njoo na hoja.
Kwa sababu sinia langu limejaa hoja.
Na nyikani kuna simba, chui, tembo na nyoka—lakini hata hao hawana nafasi kwenye meza kama hawana hoja.
Ndiyo maana tunaposema “Mizungu ya Mbagala”, tunamaanisha ujasiri wa kuuliza maswali magumu na uwezo wa kuyajibu kwa hoja, takwimu na ushahidi.
Kumkosoa Mwigulu ni haki. Kumtetea pia ni haki. Lakini hakuna upande unaopaswa kukimbia hoja na kuja na video, huko kukimbia hoja.
Historia ya Afrika ina mifano inayotufundisha madhara ya siasa zinapogeuka kuwa vita vya kuchafuana.
“Nchini Zimbabwe, Askofu Mkuu Pius Ncube alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Robert Mugabe, hasa kuhusu haki za binadamu na hali ya kisiasa nchini humo. Mvutano kati yake na serikali ya Mugabe ulikuwa mkubwa.
Mwaka 2007, vyombo vya habari vinavyohusishwa na serikali vilichapisha picha na video zilizodai kumuonyesha Ncube katika uhusiano wa kimapenzi na mke wa mtu. Tukio hilo likawa sehemu ya mzozo mkubwa wa kisiasa uliokuwa tayari umejengwa kati yake na serikali ya Mugabe. Baadaye Ncube alijiuzulu nafasi yake ya Askofu Mkuu wa Bulawayo.”
Funzo hapa si kumhukumu mtu kwa picha. Funzo ni hili:
Picha inapogeuzwa kuwa silaha ya kisiasa, hoja inaweza kupotea na mjadala wa taifa ukahamia kwenye maisha binafsi ya watu.
Na hata baada ya picha kusambaa, matatizo ya msingi ya nchi hayaondoki.
Siasa za kuchafuana na kushambuliana kwa picha za utupu hazijengi Tanzania.
Kumdhalilisha mtu kwa picha, kumvisha maneno au sauti ambazo hakuzisema, au kutumia picha kama silaha ya kisiasa hakubadilishi sera, hakujibu hoja wala hakutatui tatizo la mwananchi.
Picha inaweza kusambaa kwa kasi. Inaweza kupata maelfu ya views. Inaweza kuleta vicheko. Inaweza kuleta hasira. Lakini mwisho wa siku swali linabaki pale pale:
Hoja iko wapi? Ushahidi uko wapi?
Kama kiongozi amekosea, sema kosa lake. Kama sera ni mbaya, ibainishe. Kama uamuzi una madhara, yaonyeshe. Kama kuna ushahidi, uweke mezani.
Tusifanye siasa kuwa mashindano ya nani atatengeneza picha ya kumdhalilisha mwenzake zaidi.
Picha za chumbani zinaweza kuchekesha kwa dakika chache, lakini hazijengi shule, hazitengenezi ajira, hazipandishi uchumi na hazitatui matatizo ya mwananchi.
Tanzania inahitaji siasa za akili, hoja, sera, ushahidi na uwajibikaji.Hali hii ndivyo ilivyokuwa Zibambwe hata kama Robert Mugabe alitengeneza mapicha yale lakini mwisho wa siku alishindwa.
Na mwisho, meza iko wazi.
Sinia langu limejaa hoja.
Kibakuli chenu nacho kikiletwa mezani, hakitazamiwi kwa ukubwa wake—tutatazama kilichomo ndani.
Kama kina hoja, tuiweke mezani.
Kama kina ushahidi, tuuweke mezani.
Kama kina takwimu, tuiweke mezani.Lakini kama kina picha za kutupiana na kuchafuana tu, basi hakitatusaidia kujenga Tanzania.
Kwa sababu uwanja wa siasa za Tanzania si uwanja wa mikanda ya picha za chumbani.
Ni uwanja wa hoja, sera, ushahidi, uwajibikaji na maendeleo ya Watanzania.
Mimi nakuja na sinia langu lililojaa hoja. Ninyi njoo na kibakuli chenu—mradi tu kiwe na hoja.
Meza iko wazi.
Mwanakwetu upo?Kumbuka
“Kibakuli Kilichojaa Sisimizi.”
Nakutakia Siku Njema
0717649257
makwadeladius@gmail.com




Post a Comment