.gif)
Adeladius Makwega – MBAGALA
Mwanakwetu ana kumbukumbu ambazo, kwa mtu ambaye hakuwapo katika matukio hayo, zinaweza kuonekana kama hadithi za zamani. Lakini kwangu, haya si ya kusimuliwa na mtu mwingine. Nilikuwepo. Nilishuhudia. Nilisikia kwa masikio yangu mwenyewe.
Mwaka 1995, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi baada ya kurejea kwa mfumo huo. Mwanakwetu alipiga kura katika kituo cha Masandale Shule ya Msingi, Wilaya ya Same, Kilimanjaro.
Wakati wa kampeni, Wilaya ya Same ilipokea wagombea mbalimbali maarufu waliokuwa wakishiriki katika uchaguzi huo.
Mmoja wa waliowahi kufika kwanza alikuwa Augustine Lyatonga Mrema. Alifanya mkutano wake eneo lililokuwa karibu na nguzo na nyaya za TANESCO zilizokuwa zimelazwa chini, karibu na ofisi ndogo ya taasisi hiyo ya umeme.
Katika kunadi sera zake, Mrema alieleza mambo mbalimbali, miongoni mwao akigusia historia yake, nafasi zake serikalini na dini yake.
Alisema:
“Aisee ninasema wazi, mimi ni mzaliwa wa mkoa huu wa Kilimanjaro. Kazi yangu nilipokuwa Waziri na Naibu Waziri Mkuu mliona nilivyokuwa napambana na majambazi, na pia mimi ni Mkatoliki.”
Mwanakwetu, haya si mambo niliyoyasikia kutoka kwa mtu mwingine. Nilikuwa katika mkutano huo.
Nakumbuka hata nilivyokuwa nimevaa: suruali ya rangi ya khaki, shati jeupe, pullover neti nyeupe na viatu vyeusi. Wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne Same Sekondari.
Haya ndiyo mambo ambayo leo yanaweza kuonekana madogo, lakini kwa mtu aliyekuwepo wakati huo, yanabaki kuwa kumbukumbu ya historia ya kisiasa ya Tanzania.
Mikutano ya kampeni iliendelea kwa ngazi mbalimbali—Udiwani, Ubunge na Urais.
Katika uchaguzi huo, mgombea ubunge wa CCM alikuwa Bi. Gladness Mzirai, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu.
Lakini katika upande wa urais, mgombea mwingine aliyefanya mkutano Same alikuwa Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba wa CUF.
Alifanya mkutano upande wa kushoto karibu na barabara ya Same–Moshi, eneo la kuingia kituo cha mabasi cha Same. Mwanakwetu nilishiriki katika mkutano huo.
Profesa Lipumba alinadi mambo mbalimbali, lakini sentensi moja inabaki kichwani kwa Mwanakwetu:
“Mimi nilikuwa mshauri wa Rais wa masuala ya uchumi, sasa nataka nikafanye mimi mwenyewe, maana sijaridhika na kuwa mshauri. Kumshauri mtu anaweza kukubali au kukataa ushauri huo.”
Profesa Lipumba pia alijitambulisha kwa kueleza historia yake, nafasi alizowahi kushika na imani yake ya Kiislamu.
Lakini tofauti na baadhi ya mikutano mingine, aliruhusu wananchi kuuliza maswali.
Mwanakwetu nilipata nafasi ya kumuuliza:
“Wewe umekuwa mshauri wa Rais. Kama Rais Mwinyi ameshindwa mambo kadhaa kuyafanya, je, unaona kuwa unaweza kujitenga na kushindwa kwake?”
Jibu lake ni hili:
“Kumshauri mtu anaweza kukubali au kukataa ushauri huo.”
Hapo ndipo nilipoanza kuona jambo moja muhimu katika siasa: kuna tofauti kati ya kuwa mshauri wa mwenye mamlaka na kuwa mtu anayebeba mamlaka mwenyewe.
Kando ya mkutano huo kulikuwa na vijana wawili kutoka Same Sekondari, kutoka Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu. Mmoja wao alifahamika kama Rashidi Haruna. Baada ya mkutano, wakati wa kurejea shuleni, tulizungumza mambo mengi kuhusu Profesa Lipumba—hasa namna alivyokuwa tayari kusikiliza maswali ya wananchi na kuyajibu hadharani.
Rashidi Haruna, ambaye kwa sasa ninafahamu anaishi Mbagala Sabasaba, baadaye alibadili dini na kuwa Mkristo Mlokole.
Haya ni kumbukumbu ambazo zimebaki ndani ya Mwanakwetu kwa zaidi ya miaka 30.
Mgombea mwingine aliyefanya mkutano Same alikuwa Benjamin Mkapa.
Mkutano wake ulifanyika juu ya kituo kikuu cha mabasi cha Same Mjini, upande wa kuelekea Mbugani–Mkomazi. Mkutano ulikuwa na watu wengi, na Mkapa alitambulishwa pamoja na mke wake, Anna Mkapa.
Mwanakwetu alikuwepo.
Katika mkutano huo, upande wa CCM ulitoa hoja iliyokuwa na mantiki ya kampeni ya wakati huo:
“Mrema kasema yeye ni Mkatoliki na amezaliwa Kilimanjaro. Profesa Lipumba kasema alikuwa mshauri wa Rais na ni Muislamu. Mzee aliyepo sasa anakwenda kupumzika pamoja na washauri wake wote. CCM inakuja na kitu kipya, naye Benjamin Mkapa. Isitoshe, yeye kaoa Kilimanjaro. Kwa hiyo kazi kwetu watu wa Kilimanjaro kuamua. Nawaombea tumchague Mkapa; mama dada yetu Anna hawezi kutufanyia mambo mabaya.”
Mwanakwetu nilikuwepo katika mkutano huu na nilikerwa sana na jambo moja: CCM haikutoa nafasi ya kuuliza maswali kwa mgombea.
Hapa ndipo tofauti ya mikutano miwili iliponigusa: mmoja ulikuwa na nafasi ya maswali kutoka kwa wananchi, mwingine haukuwa hivyo.
Mwisho wa siku, Benjamin Mkapa akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa kuwa mwaka 1995 nilikuwa Kidato cha Nne, baada ya kumaliza mitihani nilirudi Dar es Salaam.
Huko Dar es Salaam nilishuhudia hekaheka za uchaguzi uliofanyika upya kutokana na changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa awali. Wakati huo niliona pia watu kama Dkt. Masumbuko Lamwai, ambaye baadaye alikuja kuwa mbunge machachari.
Haya ndiyo mazingira ambayo yalimjenga Mwanakwetu katika kuangalia siasa: si kwa kusimuliwa tu, bali kwa kushuhudia matukio, kusikiliza hoja na kuona namna wananchi walivyoshiriki katika siasa.
Mwaka 2005, katika Uchaguzi Mkuu wa tatu wa vyama vingi, Mwanakwetu alikuwa Iringa, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Sanaa ya Habari.
Katika uchaguzi huo, Jakaya Kikwete alishinda urais.
Akiwa Chuo Kikuu alipata bahati ya kusoma pamoja na vijana wawili waliokuwa wanachama wa CCM—Suguta Manchare Heche na Mjengi Lissu—ambao wote walisoma Shahada ya kwanza ya sharia LLB Heche 2008 wakati Mjengi 2007 wakaja kuwa wanasheria.
Suguta Manchare Heche ni mdogo wa damu na John Heche, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa huku Mjengi Lissu akiwa mdogo wa Tundu Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Mwanakwetu alikuwa Katibu Mwenezi wa CCM wa tawi la Chuo Kikuu, na baadhi ya kadi za uanachama hawa alizitoa yeye mwenyewe.
Haya yanaweza kuonekana kama kichekesho leo hii.
Lakini ndiyo kumbukumbu ninayoijua.
Nani leo angeweza kuamini kwamba watu ambao leo wanahusishwa na siasa za upinzani ndugu zao ni makada wa CCM?
Hata vyombo vya ulinzi na usalama vinaweza visiwe na kumbukumbu ya kila jambo hili kwa sababu haviwezi kuwa sehemu ya kila tukio linalofanyika katika dunia hii.
Swali muhimu linakuja: Kwa nini Mwanakwetu anakumbuka mambo yaliyotokea zaidi ya miaka 20 au 30 iliyopita?
Jibu ni rahisi:
Kwa sababu siasa ninayoizungumza siyo niliyoisoma jana kwenye mitandao ya kijamii. Nimeiona ikibadilika mbele ya macho yangu.
Nimeona mfumo wa chama kimoja.Nimeona kurejea kwa mfumo wa vyama vingi.Nimeona kampeni za 1995.Nimeona uchaguzi wa 2000 na 2005.Nimeona kizazi cha wanasiasa kikibadilika.Na leo naona mjadala mpya ukijengwa kupitia mitandao ya kijamii.
Na hivi karibuni Mwanakwetu nilichapisha bango kuhusu kupinga udhalilishaji unaofanywa kwa kutumia video zilizotengenezwa au kubadilishwa kwa teknolojia dhidi ya watu wengine.
Katika maoni yaliyotolewa, majina ya baadhi ya wanasiasa yalitajwa, yakiwemo Nchimbi, Polepole, Lissu, Majaliwa, January Makamba na Warioba, huku baadhi ya majina mengine ya wanasiasa yakiwa hayakutajwa. Lakini jambo la muhimu hapa si jina moja tu.
Jambo la muhimu ni taswira inayojengwa na mjadala wenyewe.Kwa sasa, jina la Mwigulu Nchemba limeibua mjadala mkubwa katika chapisho hili. Na hapa ndipo takwimu zinapoanza kuwa na maana.
Kwenye chapisho hilo hadi mapema Oktoba 7, 2026 kulikuwa na:
👍
Likes: 165
💬 Comments: 193
↗️ Shares: 3
Kwa mtazamo wa kwanza, mtu anaweza kusema likes 165 ni nyingi.
Lakini ukiangalia kwa jicho la mchambuzi, kuna jambo jingine kubwa zaidi:Maoni 193 yamezidi likes 165.
Hii ni takriban asilimia 17 zaidi ya likes.
Hii haimaanishi kwamba watu 193 wanampinga au kumuunga mkono mtu anayezungumziwa.
Comments si kura.
Maoni yanaweza kuwa ya kuunga mkono, kupinga, kukosoa, kuuliza, kushambulia hoja, kumtetea anayezungumziwa au hata kumkosoa mwandishi wa chapisho. Lakini jambo moja linaonekana wazi:
Chapisho limezalisha mjadala mkubwa kuliko reaction ya kawaida ya “like”.
Hapa ndipo Mwanakwetu anapoona jambo ambalo si rahisi kuliona kwa kuangalia namba pekee. Likes 165, comments 193 na shares 3 zinatoa picha ya aina fulani ya siasa:
Watu wanazungumza sana, lakini hawasambazi sana.Hii inaweza kumaanisha kwamba suala hilo limewagusa watu walioliona, lakini bado hakuna ushahidi wa kutosha kusema limeenea kwa kiwango kikubwa nje ya kundi hilo.
Kwa hiyo, comments nyingi si lazima ziwe umaarufu.
Wakati mwingine comments nyingi ni ishara ya mgawanyiko.Wakati mwingine ni ishara ya hasira.Wakati mwingine ni udaku wa kisiasa.Wakati mwingine ni utetezi.Na wakati mwingine ni upinzani mkali.Ndiyo maana mchambuzi makini hapaswi kuangalia likes pekee.
Anapaswa kuuliza:
Watu wanasema nini?Wanasema kwa nini?
Ni upande gani unaonekana kuwa na hoja nyingi?Ni upande gani unaonekana kuwa na hisia nyingi kuliko hoja?
Na zaidi ya yote:
Je, mjadala huu unamjenga au unamdhoofisha mwanasiasa anayezungumziwa?
Hii ndiyo Tanzania ya siasa za leo.
Hali hii ni tofauti kwa namna nyingi na Tanzania ya mwaka 1995.
Mwaka 1995, kampeni zilifanyika zaidi katika viwanja, barabarani na kwenye mikutano ya hadhara.Leo, uwanja mkubwa wa siasa umehamia pia kwenye mitandao ya kijamii.
Zamani mwanasiasa alihitaji jukwaa na kipaza sauti.
Leo anaweza kuzungumziwa na maelfu ya watu bila hata kuwa kwenye jukwaa.
Zamani wananchi walimuuliza mgombea swali kwenye mkutano.Leo wananchi wanamuuliza mwanasiasa swali kupitia comment.
Zamani hoja ilibaki kwenye uwanja wa mkutano.
Leo hoja inaweza kuendelea kwa siku nyingi kwenye mitandao.Na hapo ndipo kuna tofauti kubwa:
Siasa zimekuwa za haraka zaidi, lakini pia zimekuwa na kelele nyingi zaidi.
Mwanakwetu akitazama historia kutoka 1995 hadi leo, hawezi kusema siasa za Tanzania zimebaki pale pale.Watu wamebadilika.Vyama vimebadilika.Wanasiasa wamebadilika.Teknolojia imebadilika.Lakini jambo moja linaonekana kuendelea:Ushindani wa kisiasa bado upo.
Na leo ushindani huo hauishii kwenye mikutano ya hadhara.
Uko kwenye Facebook.
Uko kwenye WhatsApp.
Uko kwenye video.
Uko kwenye comments.
Uko kwenye mabango ya mitandao.
Na wakati mwingine, comment moja inaweza kuanzisha mjadala mkubwa kuliko hotuba nzima ya mwanasiasa.
Kwa hiyo, ninapoona comments 193 dhidi ya likes 165, siangalii tu namba.
Naona dalili ya jamii inayotaka kuzungumza.
Lakini bado swali linabaki:
Joto hili la kisiasa linapanda au linapungua?
Na kama linapanda, linatokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi, au linaongezeka kwa sababu ya mgawanyiko, hasira na ushindani wa kisiasa?Kwa mjadala huu Mwanakwetu anaona kuwa Mwigulu Lameck Nchemba anaibua mjadala mkubwa kwa jamii ya Watanzania.
Mwanakwetu upo ?Kumbuka:
“Jamii ya Watanzania Wanoataka Kuzungumza.”
Nakutakia siku njema.
✉️ makwadeladius@gmail.com
📞 0717649257













%20Facebook.png)
%20Facebook.png)
.gif)
Post a Comment