Adeladius Makwega-MBAGALA
“Bwana Mungu, nirudishie haki yangu, niponye maovu yanayonitesa. Ewe Mungu, mbona wanitupa…”
Waimbaji wanaendelea kuimba:
“Nitajongea
altare yangu,Furaha yangu na heri yangu siku zote,
Nitajongea altare yangu,Furaha yangu na heri yangu siku zote…”
Haya yalikuwa majira ya asubuhi. Waamini walikuwa wameingia kanisani kwa ajili ya kusali Misa ya Jumapili. Kanisa lilikuwa dogo, lenye waamini wachache mno. Hakukuwa na maandalizi makubwa, hawakuwa na waimbaji wa kutosha, wala kiongozi wa kwaya. Vifaa vya muziki vilikuwa vichache, zaidi ya kayamba moja iliyokuwa imewekwa kwenye benchi la kwaya.
Mwanakwetu akaikuta kayamba hiyo, akaichukua na kuanza kuicheza taratibu huku wimbo wa Kiingilio ukiendelea kuimbwa.
Misa ikaendelea kama kawaida yake. Lakini Mwanakwetu hakuielewa vizuri lugha iliyokuwa ikitumika. Muda wa mahubiri ulipofika, Askofu akaanza kuhubiri. Askofu huyu alikuwa akitokea Jimbo Katoliki la Alexandria nchini Misri, huyu ni Askofu Mwarabu. Alianza mahubiri kwa lugha ya Kiarabu, huku sista akiwa anafanya tafsiri kwa Kiingereza.
Hapo ndipo Mwanakwetu akaanza kuambulia baadhi ya maneno ya mahubiri hayo.
Askofu akasema:
“Nilipokuwa Padri, nilipigiwa simu na ndugu mmoja ambaye alikuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la eneo hili. Alinisimulia kuhusu suala la rushwa ya ngono kazini.”
Kansela wa taifa lao, ambaye alikuwa mwanamke, alikuwa amefanya uteuzi wa Mkuu wa Shirika la Utangazaji, ambaye naye alikuwa mwanamke. Mara baada ya uteuzi huo kutangazwa, kukaibuka malalamiko kwamba huenda nyuma ya uteuzi huo kulikuwa na rushwa ya ngono.
Kumbuka, mteuzi alikuwa mwanamke na aliyeteuliwa alikuwa mwanamke.
Akilini mwangu nikajiuliza:
“Inawezekanaje? Je, kuna mahusiano ya jinsia moja?”
Nilipomuuliza vizuri ndugu aliyenipa taarifa hii, alijibu:
“Hapana.”
Akaeleza kwamba mshauri wa Kansela wa masuala ya utangazaji alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke aliyeteuliwa.
Hapo kidogo nikaelewa.
Nikamuuliza:
“Je, aliyefanya uteuzi analifahamu hilo?”
Ndugu huyu akajibu:
“Sina hakika nalo, maana haya ni mambo ya wakubwa.”
Nikamuuliza tena:
“Je, una hakika gani kwamba taarifa hii ni ya kweli?”
Akanijibu kwamba mshauri huyo wa Kansela na mwanamke aliyeteuliwa walikuwa wamewahi kufanya kazi pamoja hapo awali na, kwa mujibu wa taarifa alizokuwa nazo, walikuwa na uhusiano wa kimapenzi pika pakua. Akaongeza:
“Kila mmoja anajua mambo haya, lakini hakuna wa kumfunga paka kengele.”
Mahubiri hayo yakaendelea.
Askofu akasisitiza kwamba katika maisha ya kazi kuna mambo mengi yanayoweza kusemwa kwa wivu, chuki au kwa nia ya kumchafua mtu. Kwa hakika, duniani hakuna mkamilifu. Lakini wale wanaopewa dhamana ya kufanya maamuzi wanapaswa kuwa waangalifu, waadilifu na wenye kuheshimu haki.
Maana katika majukumu yoyote, panapotokea hoja ya upendeleo wa aina yoyote, inaweza kuleta migawanyiko, kuvunja moyo wa wafanyakazi na kufanya iwe vigumu kwa taasisi au jamii kufikia malengo yake.
Mfanyakazi aliyekata tamaa na kuona kwamba haki haipo mahali pake anaweza kupoteza moyo wa kazi.
Kisha Askofu akasema:
“Rushwa yoyote ni mbaya na ina madhara makubwa kwa jamii.”
Maneno hayo yakamfanya Mwanakwetu awaze zaidi.
Kwa mafundisho ya Kanisa Katoliki, haki na uadilifu ni mambo ya msingi katika mahusiano ya binadamu.
Rushwa sasa inapohusisha matumizi mabaya ya mamlaka, upendeleo usio wa haki au kumshawishi mtu kufanya jambo lisilofaa kwa ajili ya kupata manufaa, inagusa moja kwa moja wajibu wa kuheshimu haki na utu wa mwanadamu.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki, katika kifungu cha 2409, inataja rushwa miongoni mwa vitendo vinavyokiuka wajibu wa haki katika matumizi ya mali na mamlaka. Hii inatufundisha kwamba mtu mwenye dhamana hapaswi kutumia nafasi yake kwa manufaa yasiyostahili au kwa kupindisha haki.
Katika suala la ngono, Kanisa pia linafundisha kwa msisitizo juu ya heshima ya mwili na utu wa mwanadamu.
Mtume Paulo, katika 1 Wakorintho 6:18–20, anawaonya Wakristo kuukimbia uasherati na anakumbusha kwamba mwili wa Mkristo ni hekalu la Roho Mtakatifu.
Katekisimu, katika kifungu cha 2353, inafundisha kwa uzito kuwa tendo la ngono nje ya ndoa, wakati kifungu cha 2355 kinazungumzia vitendo vinavyomfanya mtu kuwa chombo cha starehe ya kingono na hivyo kudhalilisha utu wake.
Kwa mtazamo huo, kutumia kazi, cheo, alama, huduma, zabuni, nafasi au mamlaka nyingine kama njia ya kudai au kutoa ngono ni jambo linalogusa si tu maadili ya ngono, bali pia haki, utu wa binadamu, matumizi ya mamlaka na uaminifu katika jamii.Mtu hapaswi kugeuzwa kuwa bidhaa.
Mwili wa mwanadamu si bidhaa ya biashara.
Utu wa mwanadamu haupaswi kuwa bei ya kupata ajira, cheo, huduma au nafasi.
Na mwenye mamlaka anapaswa kukumbuka kwamba mamlaka ni dhamana, si ruhusa ya kumtumia mwingine kwa maslahi yake binafsi.
Vivyo hivyo, Kanisa linatufundisha kwamba katika kutathmini uwajibikaji wa mtu, ni muhimu kuangalia mazingira halisi. Kuna tofauti kati ya mtu anayefanya uamuzi kwa hiari na mtu anayeshinikizwa, kutishwa au kulazimishwa na mwenye mamlaka. Hivyo, katika suala la rushwa ya ngono, si sahihi kuwahukumu wahusika wote kwa kipimo kimoja bila kuangalia mazingira na kiwango cha uhuru wa kila mmoja.
Mafundisho haya yanatukumbusha jambo moja muhimu: haki haiwezi kujengwa juu ya unyonyaji wa utu wa mwingine.
Ibada ikaendelea hadi mwisho. Lugha iliyokuwa ikitumika, kwa kadiri Mwanakwetu alivyoweza kukumbuka, ilikuwa imebadilika na sasa ilikuwa ya Kijerumani, ambayo nayeye hakuweza kuifahamu vizuri.
Hatimaye, Misa ikafikia tamati na mwisho wimbo huu ukaanza kuimbwa:
“…Tutayarishe mapito yake,Bwana anakuja na enzi kutuokoa.Bwana anakuja, anakuja, anakuja kwetu…(Anakuja!)Anakuja na enzi, anakuja kutuokoa…”
Wakati wimbo huu ukiendelea kuimbwa, ghafla Mwanakwetu akakurupuka na kushituka.
Akaamka!
Akapepesa macho!
Akaangalia huku na kule.
Kumbe alikuwa usingizini.
Alikuwa anaota!
Hakukuwa na kanisa.
Hakukuwa na Askofu.
Hakukuwa na sista.
Hakukuwa na kwaya.
Hakukuwa na kayamba.
Na wala hakukuwa na Misa!
Simu yake ilikuwa imezimwa ikiwa inachaji. Akaifuata saa yake na kuiangalia.
Ilikuwa ni majira ya saa 9:33 usiku wa manane.
Akasema:
“Lo salale , kijana wazamani wa Mbagala kumbe nilikuwa naota! Hizi ndoto za usiku wa manane zina balaa.”
Hapo hapo akaanza kukumbuka yote aliyoyaota.
Akaanza kukumbuka kanisa.
Akaanza kumkumbuka Askofu.
Akaanza kukumbuka simulizi ya rushwa ya ngono.
Akaanza kukumbuka mahubiri.
Lakini kulikuwa na jambo moja ambalo hakuweza kulikumbuka vizuri.
Aya ile ya Wakorintho na vifungu vya Katekisimu vilikuwa vimetoweka ndotoni mwake.
Mwanakwetu akaingia mtandaoni.
Akaanza kutafuta.
Akasoma.
Akaangalia tena.
Na ndipo akavipata.
Wakati anayaandika makala haya, akaweka marejeo hayo kwa usahihi wake ili simulizi hii isiishie kuwa ndoto tu, bali pia iwe nafasi ya kutafakari juu ya haki, utu wa binadamu, matumizi ya mamlaka na mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu maadili ya maisha ya mwanadamu.
Lakini sasa swali linabaki:
Je, ilikuwa ni ndoto tu?
Au ndoto hiyo ilikuwa imekusanya pamoja mambo ambayo Mwanakwetu aliwahi kuyasikia, kuyafikiria au kuyatafakari?Jibu hilo namwachia msomaji.
Maana wakati mwingine, ndoto huja usiku, lakini ujumbe wake unaweza kuendelea kutafakariwa mchana kweupe na mimi wewe na yule.
Mwanakwetu, upo?Kumbuka:
“Hizi Ndoto za Usiku wa Manane Zina Balaa.”
Nakutakia siku njema.
✉️
makwadeladius@gmail.com
📞 0717649257
NB Kama makala haya yatakuwa yamekiuka maudhui yoyote ya kikanisa basi ni makaso ya Adeladius Francis Fidelis Petro Makwega Kazimbaya wa Mbagana la namba msamaha kwa makosa hayo mbel ya Kanisa na Mungu .
.gif)
.gif)









.gif)
Post a Comment