Adeladius Makwega – MBAGALA
“Hivi unafahamu kuwa Shemelekwa wamemtumbua? Yule jamaa alikuwa mwema sana. Niliongea naye, akaniambia angenisaidia. Sasa ndiyo basi tena.”
Haya yalikuwa mazungumzo ya Septemba 30, 2026, wakati Mwanakwetu alipowasiliana na ndugu yake ambaye wamefahamiana kwa miaka kadhaa. Mazungumzo yao yalianza kwa kauli hiyo.
Mwanakwetu akamjibu:
“Yule si mwalimu? Hapo riziki yake imefika mwisho. Huwezi kujua Mungu amemuandalia nini, au Mungu amemuondolea nini.”
Ndugu huyo akamuuliza:
“Hivi mtu akitumbuliwa inakuwaje?”
Mwanakwetu akajibu:
“Ni jambo la kawaida. Tena Shemelekwa katumbuliwa akiwa nyumbani kwake. Watu katika nchi hii wametumbuliwa huku vyombo vya habari vikirusha matukio hayo mubashara.
Wapo watu ambao wametumbuliwa Ikulu, katika vikao vyenye watu zaidi ya elfu moja. Maisha lazima yaendelee.
Kikubwa ni kwamba unatakiwa kupiga moyo konde na kusonga mbele.”
Ndugu huyo akauliza tena:
“Sasa Shemelekwa atarudi kwenye kazi yake ya awali?”
Mwanakwetu akajibu:
“Tena hilo ndilo jambo la msingi. Kama yeye ni mwalimu, basi arudi kufundisha kwa moyo wake wote.
Unajua, unaweza kufanya baadhi ya kazi na ukapata kipato kizuri, lakini kiroho usikue. Mwisho wake unaweza kuwa mtu wa kiburi, chuki na roho mbaya. Sasa kama unafanya kazi halafu unazidi kuwa mtu mbaya, hilo ni hatari.
Ni heri mtu akue kiimani, ni heri uwe na hofu ya Mungu maana hapa duniani tunapita.”
Ndugu huyo akakubaliana na maneno hayo:
“Hilo ni sahihi.”
Kisha akaendelea:
“Kuna mtu leo unaweza kumuuliza: ‘Ndugu yangu, Oktoba 29, 2025, Tanzania ilipata shida. Wewe ulikuwa wapi na ulikuwa na nani?Na ulikuwa unafanya nini? Halafu ukamtaka awataje hao aliokuwa nao ili waje kuthibitisha ukweli huo. Swali hili wapo ambao hawezi kulijibu.”
Mwanakwetu akaongeza:
“Unajua, baada ya utenguzi, unaporejea katika kazi yako ya awali na ukaifanya kwa moyo wote, jambo hilo linaweza kukujengea heshima hata kwa watu wa taaluma yako waliobaki huko.
Watakuheshimu kwa sababu utakuwa mfano wa mtu aliyepitia changamoto, lakini hakukata tamaa. Unaweza kuwa umeondolewa kwenye nafasi fulani, lakini ukarudi kwenye kazi yako ya awali na ukaifanya kwa uadilifu na moyo wote.
Si jambo zuri mtu kuogopa utenguzi kiasi cha kufikia hatua ya kubadilika na kuwa mtu mwingine. Mtu asiwe haramia au bedui kwa kisingizio cha kutaka kulinda nafasi yake. Hilo si jambo sahihi.”
Baada ya mazungumzo hayo, Mwanakwetu akaagana na ndugu yake na kuendelea na safari yake kwenda kula chakula cha mchana. Safari haikuwa ndefu.
Akiwa njiani, ghafla akamkumbuka Mwita Waitara Mwikabwe, ambaye ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa Mara.
Mwanakwetu akajisemea moyoni:
“Waitara ni mwalimu mzuri sana wa Basic Mathematics. Anapolifundisha somo hili, wanafunzi wanamwelewa vizuri sana.
Kama angekuwa Profesa wa Hisabati, angeweza kusaidia sana kuelimisha jamii kuhusu somo hili. Kwa kipaji chake cha ualimu, angeweza pia kuwa mwandishi wa vitabu vya Hisabati na kutoa manufaa makubwa kwa jamii.
Lakini sasa amewekeza nguvu zake katika siasa, ambako, kwa mtazamo wangu, siasa za CCM hazihitaji sana kutumia mantiki ya kihisabati.”
Mawazo hayo yakamfanya Mwanakwetu atafakari zaidi kuhusu maisha, kazi na nafasi ambazo mwanadamu hupitia.
Maana wakati mwingine mtu anaweza kuondolewa kwenye nafasi fulani na akadhani maisha yake yamefika mwisho. Lakini kumbe huo unaweza kuwa mwanzo wa ukurasa mwingine wa maisha yake.
Kazi inaweza kubadilika. Cheo kinaweza kuondoka. Nafasi inaweza kupotea. Lakini kipaji, taaluma, utu na imani ya mtu vinaweza kubaki kuwa sehemu muhimu ya maisha yake.
Ndiyo maana, katika maisha, mtu anapokutana na changamoto, anapaswa kupiga moyo konde na kuendelea mbele.
Hayo ndiyo baadhi ya mawazo ambayo Mwanakwetu aliyapata kutokana na mazungumzo yale, pamoja na kumbukumbu zake nyingine, na akaamua kuyaweka katika makala hii.
Na mwisho wa yote, swali linabaki:
Mwanakwetu, upo?
Kumbuka.
“Maisha Lazima Yaendelee.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)









.gif)
Post a Comment