JE UTAMPENDA MPAGANI?

 


Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Siku hii Mwanakwetu alikuwa amefanya kazi zake vizuri. Alikuwa ameandika makala moja kuhusu mgogoro wa kazini baina ya ndugu Mbegu, dereva Mzaramo, na ndugu Oforo, Mchaga mhudumu, waliokuwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma mwaka 1964.

 

Mgogoro huu ulisababisha ndugu Oforo kushitakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu au kulipa faini ya shilingi 47 pamoja na kulipa hasara iliyotokana na ajali aliyosababisha.

Ndugu Oforo alilipa faini hiyo na kulipa hasara ya shilingi 600, ambapo alikuwa akikatwa shilingi 50 kila mwisho wa mwezi kwa miezi 12. Msajili wa Hazina wa Tanganyika alipewa jukumu la kusimamia makato hayo.

 

Makala haya Mwanakwetu aliyamaliza kuyaandaa vizuri. Alipokuwa anaingia hatua ya pili ya uhariri, usingizi wa mchana ukamnyemelea. Ili kuupotezea usingizi huo, aliacha kazi yake na kutoka nje ili apunge upepo.

 

Akiwa hapo nje, mara wakapita vijana wawili—msichana na mvulana. Simu yao ilikuwa ikicheza video za Dkt. Emmanuel Nchimbi za kampeni za CCM za mwaka 2015.

 

Kijana wa kiume akasema:

 

“Yaani CCM wanafiki mno! Wamekaa kimya, hakuna hata mmoja anayemzungumzia Nchimbi. Yaani Dkt. Nchimbi kama hakuwa Katibu Mkuu wa CCM, kama hakuwa Makamu wa Rais! Unajua hata Job Ndugai walimfanyia hivyo hivyo. Wakaona watu kimya, na mambo yale yale yanajirudia tena kwa Dkt. Nchimbi! CCM hawana soni! Hivi hawa viongozi wengine wa CCM wanadhani wapo salama?”

Mwanakwetu akawa anawasikiliza vijana hawa kwa makini sana

.

Hapo hapo akapita jamaa mwingine akasema:

“Ahaa, Mwanakwetu, nakuona unapunga upepo.”

Nikajibu:

“Ndiyo.”

Huyu jamaa akapita akaenda zake.

 

Baadaye nikabaki mwenyewe. Kisha nikaingia maliwatoni, nikajisuuza uso wangu na kurudi pale niliposimama.

Nilipokuwa nje, jambo lililokuwa likizunguka kichwani mwangu ni yale maneno ya vijana wale kuhusu unafiki wa wanaCCM.

 

Nikajiuliza:

 

“Utahangaika nao katika mazuri, lakini ukipata shida na viongozi wao wa juu, wanaCCM wanakukwepa. Wanakaa pembeni kana kwamba hawakufahamu kabisa.”

 

Maneno haya yalimuumiza sana Mwanakwetu.

Mara akili yake ikakumbuka matukio mawili ya kweli kabisa—moja la Mkuu wa Wilaya na lingine la Mkurugenzi Mtendaji.

Rais alifanya utenguzi wa Mkuu wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya mpya akafika, akaripoti na kukabidhiwa wilaya yake. Yule aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wa zamani akaondoka katika nyumba aliyokuwa akiishi.Lakini sasa, tatizo likawa kubwa.

Hakuwa na hata nauli ya kurudi kwao.

Mizigo yake aisafirishaje?

Aende wapi?

Afanye nini?

Huyu jamaa ilibidi akajibanze kwa kimada kwa zaidi ya miezi mitatu, akijificha huku akisubiri mambo yake yawe vizuri ili aweze kurudi kwake.

 

WanaCCM waliokuwa wakijua hali hiyo wakawa wanamcheka tu.

 

“Mjinga sana huyu jamaa. Pesa zote alikuwa anakula na makahaba.”

 

Maneno ya namna hiyo ndiyo aliyokuwa akiyasikia. Lakini Mungu si mwanadamu.

Mambo yake yaliponyooka, alipata nauli, akabeba mizigo yake na kurudi kwao. Na katika kipindi kile kigumu, msaada mkubwa alioupata ulitoka kwa yule kimada. Sasa swali linabaki:

Kama yule kimada asingemsaidia, hali yake ingekuwaje? Ni nani angekuwa tayari kumfungulia mlango? Ni nani angempa chakula?

Ni nani angemwambia, “Usijali, utapita tu katika kipindi hiki”?

Na jibu la swali hili, kwa wale waliokuwepo, linajulikana.

Ndiyo maana Yesu katika Mathayo 21.31 anasema:

“Angalieni Makahaba na Watoza Ushuru wasije kuwatangulia Mbinguni.”

Kisa kingine, Hii Ilikuwa Mei 17, 2019, Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Rais alifanya utenguzi wa Mwanakwetu, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi.

Utenguzi ulifanyika Ikulu ya Dar es Salaam Mei 16, 2019.

Mwanakwetu akarudi Mbozi Mei 17, 2019.

Kwa hali ilivyokuwa, alishauriwa na ndugu zake akabidhi haraka ofisi na asilale katika nyumba aliyokuwa akiishi, kwa sababu kulikuwa na hatari zaidi.

Mmoja wa ndugu zake akamwambia:

“Kaka, hawa jamaa siyo wazuri. Watu wanaweza kuingia ndani ya nyumba hiyo, wakakunyonga, halafu wakasema umejinyonga kutokana na stress za kutumbuliwa.”

 

Kuondoka siku hiyo hiyo hakukuwa na budi.

Katika Halmashauri hii nilifanya kazi na madiwani wa CCM, CHADEMA na TLP bila ubaguzi.

Kwa ukweli wa Mungu, madiwani wa CCM walikuwa marafiki zangu zaidi. Hata majumbani kwao nilikuwa nafika na kula ugali wao.

 

Wakati madiwani wa CHADEMA na yule wa TLP, kama vile Bahati Mbugi na akina Mwashitete, nilikuwa nakutana nao zaidi katika mikutano ya maendeleo na vikaoni, na siyo majumbani mwao. Lakini walipokuwa na jambo la kutatua, niliwasaidia mno.

Utenguzi ulifanyika katikati ya mwezi.

Wakati wa Pasaka, Aprili 2019, familia yangu ilikuwa imefika Mbozi na nilikuwa nimelipa karo za wanangu kadhaa pamoja na watoto wengine ninaowalea waliokuwa wakisoma shule za msingi na sekondari na vyuo.Akiba niliyokuwa nayo haikutosha kusafirisha mizigo na kukodi lori kutoka Mbozi hadi Tanga au Mbagala.

Je, ningefanyaje?

Nikampigia simu mzee wangu, Baba , Francis Makwega.

Akaniunganisha na padri mmoja.

Padri huyu akanipa shilingi milioni tatu.

Baadaye wakuu wa Idara ya Elimu Msingi na Elimu Sekondari—akina mama wawili, mmoja Msukuma na mwingine Mnyia—nilipowapigia simu, walienda benki muda huo huo.Kila mmoja akanipa shilingi milioni moja.

Nikawa na shilingi milioni tano.

Lakini bado kulikuwa na jambo jingine.

Mizigo ilikuwa bado ndani ya nyumba.

Nyumba niliyokuwa nikiishi walikuja madereva wa Halmashauri hiyo—tena wale wenye ajira za mikataba mifupi mifupi—na dereva mmoja tu mwenye ajira ya kudumu. Wakawa wananisaidia kufunga mizigo mpaka saa nne usiku.

Nikawa nimemaliza.

Lori likaja.

Likapakia mizigo.

Na mimi nikaondoka.

Lakini kuna jambo moja ambalo hadi leo linaniumiza.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, hakutokea hata diwani mmoja wa CCM kunipigia simu.

Hakuna aliyepiga simu kuniambia:

“Mwanakwetu, pole.”

Hakuna aliyesema:

“Usijali, tutakusaidia.”

Hakuna aliyesema:

“Uko salama?”

Hakuna hata aliyeniuliza kama nimepata pa kwenda.

Badala yake, madiwani wa CHADEMA walinipigia simu, walinitia moyo.

Na diwani mmoja wa CHADEMA ndiye aliyekuwa pamoja nami tangu nilipofika baada ya utenguzi.

Alinisaidia kufunga mizigo.

Akanitafutia lori.

Akapakia mizigo mpaka nilipoondoka usiku ule.

Akanisindikiza kwa gari yake kwa mwendo mrefu.

Diwani huyu wa CHADEMA aliitwa Bahati Mbugi.

Labda nisichume dhambi.

Pengine rafiki zangu wa CCM walimtuma Mheshimiwa Bahati Mbugi ili wao wasionekane.Hili halikuwa hivyo.Lakini moyoni mwangu nilibaki na swali moja:

Kwa nini mtu ambaye nilikuwa namwona kama mpinzani wangu kisiasa ndiye aliyekuwa karibu nami wakati nilipokuwa katika shida, lakini wale niliowaita marafiki zangu wakawa kimya?

Hili ni swali gumu.

Na wakati mwingine majibu yake huwa yanauma kuliko swali lenyewe.

Msomaji wangu, hiki ndicho alichofanyiwa Mheshimiwa Job Ndugai.

Na hiki ndicho anachofanyiwa leo hii Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Ndiyo maana vijana wale wanasema:

CCM ni hodari sana wa unafiki.

Najua Watanzania kadhaa wana watoto wao katika nafasi mbalimbali.

Nawaombeni sana:

Waombeeni watoto wenu.

Waombeeni ndugu zenu.

Kwa sababu haya mambo yanakatisha tamaa.

Usidhani mtoto wako yupo na wenzake kumbe yupo mwenyewe.

Usidhani mtoto wako anakula raha, kumbe anakula karaha.

Usidhani kwa sababu anavaa suti nzuri, gari lina kiyoyozi na anatembea na watu wakubwa basi maisha yake yako salama.

Wakati mwingine nyuma ya tabasamu lake kuna machozi ambayo huwezi kuyaona.

Wakati mwingine nyuma ya cheo kuna upweke mkubwa.

Wakati mwingine mtu anayesifiwa leo, kesho anaweza kupita barabarani huku wale waliokuwa wakimzunguka jana wakivuka upande mwingine wa barabara ili wasikutane naye.

Haya yanaweza kusimuliwa na wachache sana kama akina Mwanakwetu.

Lakini ujumbe wangu kwa wanaCCM, hasa wenye nyadhifa kubwa, ni huu:

Tambueni kuwa jamii inajifunza mengi.

Viongozi wawe makini.

Watu wengine wanauliza:

“Dkt. Nchimbi yupo wapi?”

“Mdogo wake yupo wapi?”

Hakuna anayetoa majibu.

Na kibaya zaidi, wanaolizungumzia jambo hili zaidi ni CHADEMA, wakati wanaCCM wenyewe wako kimya.

Jamani, nani katuroga?

Maana chama kinaweza kuwa na mamilioni ya wanachama, lakini siku ya shida mtu anaweza kujikuta amesimama peke yake.

Unaweza kuwa na vyeo, marafiki, walinzi, magari na watu wanaokuita “Mheshimiwa” kila dakika.

Lakini siku ukivuliwa cheo, ndipo utakapogundua:

Ni nani alikuwa anakupenda wewe, na ni nani alikuwa anapenda cheo chako.

Na hapo ndipo swali langu linapoanzia.

“Wewe kama haumpendi Mkatoliki mwenzako, utampenda mfuasi wa Muhamadi? Je, utampenda Mpagani?”

Mwanakwetu, upo?

Kumbuka:

JE, UTAMPENDA MPAGANI?

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

0/Post a Comment/Comments