HODARI WA KUBADILISHA SUTI


 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Septemba 3, 2026, Mwanakwetu alimkumbuka Padri Fidelis, ambaye ndiye aliyesimamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Antony wa Padua, Mbagala, iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Shule hii hapo awali ilifahamika kama AMET.

 

Najua ndugu zangu waliosoma shule hii katika kipindi hicho cha awali mtanisaidia kunijulisha: AMET ilikuwa na maana gani?

Hapa nangoja jibu kutoka kwa Sauda Lilingani, Demetria Makwega na wengineo popote mlipo.

 

Mimi nilibahatika kusoma twisheni tu katika taasisi hii enzi za Profesa Robert Mfugale, Dkt. Komba, Brother Linuma, Mzee Sagala na enzi zile za Mhasibu Marandu.

 

Nakumbuka pia mwaka 1989, waliofanya mtihani wa kujiunga na shule hii waliongozwa na Edwin Ngutu, maarufu Kijana wa Kijaluo, ambaye alipata alama za juu kuliko wote. Kwa bahati mbaya hakwenda kujiunga na shule hii; alikwenda Kibasila Sekondari, ambako baada ya kufanya vizuri katika shule ya umma.

 

Kwa wale wanaokumbuka, majengo ya awali ya taasisi hii yalikuwa katika maeneo mawili tofauti. Kwanza yalikuwa pale kilipo Kituo cha Kiroho Mbagala, eneo lililokuwa likifahamika kama Mbagala Msalabani, ambalo sasa linajulikana kama Mbagala Misheni. Baadaye shughuli zilihamia Parokiani Mbagala Zakhem.

 

Baada ya ujenzi kufikia hatua nzuri, shule hii ikahamishiwa katika eneo ilipo sasa, jirani na Mbagala Makuka na Mbagala Sabasaba.

Siku ya leo msomaji wangu, naomba nikusimulie namna Padri Fidelis, ambaye alikuwa na asili ya Italia, alivyokuwa akisimamia ujenzi wa shule hii.

 

Asubuhi aliamka, akasali sala za masifu ya asubuhi, kisha akaongoza Misa ya asubuhi. Baada ya Misa alizungumza na waamini wachache, halafu akaelekea moja kwa moja kwenye eneo la ujenzi.

 

Alipofika, alikuwa na maswali mengi.

“Mbona hapo mmejenga hivyo?”

“Mbona hapo watoto wanakanyaga?”

Na wakati mwingine alisisitiza kwa ukali:

“Sitaki kuona mnajenga vibaya!”

Baada ya hapo alirudi katika makazi yake kwa ajili ya majukumu mengine. Lakini mchana alirudi tena kwenye eneo la ujenzi kukagua kazi ilivyokuwa ikiendelea, kutoa maagizo kwa mafundi na kuhakikisha mambo yanaenda kama alivyotaka.

 

Jioni, kuanzia saa kumi na nusu hadi jua linapozama, alikuwa tena eneo la ujenzi.

Ndipo alipomalizia siku yake.

Baadaye alirudi katika makazi yake.

Haya ninayakumbuka sana.

Kwa nini?

Kwa sababu Mwanakwetu na watoto wenzake kadhaa wa kipindi hicho tulikuwa jirani sana na Padri Fidelis. Tulimwona. Tulimjua. Tuliona namna alivyokuwa akifanya mambo yake.

 

Msomaji wangu unaweza kusema:

“Mwanakwetu, leo umetuletea simulizi za kanisani tu?”

La hasha!

 

Nina hoja nzito kwa kila mmoja wetu.

 

Septemba 3, 2026, nikiwa ndani ya basi la daladala, ndugu mmoja alisema maneno ambayo yalinifanya nimkumbuke sana Padri Fidelis.

 

Alisema:

“Unajua Magufuli alisoma Kemia na hata Hesabu alikuwa anaifahamu. Kwa kipindi kirefu wasomi wengi walikuwa na tabia ya kukwepa Hesabu. Hili ni somo ambalo halikwepeki. Unaweza kumpa mkandarasi kazi, badala ya kujenga jengo ambalo linatakiwa kuwekwa nondo nane, yeye akaweka nondo sita na nusu au akaweka nondo nne tu huku akizikata na kuzionesha kama nondo nane. Kwa kutazama kwa macho utaona nondo nane, lakini ukweli ni kwamba hizo ni nondo nne tu. Suala la ujenzi wa mradi wowote linatakiwa kuzingatia sana ujuzi wa anayesimamia mradi huo na pia moyo wa anayesimamia mradi huo.”

 

Akaendelea kusema:

 

“Unaweza kuwa na ujuzi lakini ukaongea na mkandarasi wakati jengo la umma linajengwa, halafu yeye akawa anakujengea jengo lako nyumbani.‘Bwana, mimi najenga hapa kwa ratio hii. Usiniwekee vikwazo; na wewe nitakujengea jengo lako.’

Hapa jamaa huyu anao ujuzi, lakini tamaa imemloga na kazi ya umma inaharibika.”

 

Jamaa huyu ndani ya daladala akaendelea kusema:

 

“Magufuli alikuwa na jamaa zake wanne… Kuandika, Mfugale na Kijazi. Hawa walimuongoza vizuri na kazi ilifanyika vizuri. Ukichanganya na ule moyo wa Rais Magufuli wa kuhoji-hoji, mambo ya umma yalikuwa yanaenda vizuri sana.”

 

Tupo ndani ya basi Mwanakwetu anatega sikio vizuri, shatani mshenzi sana akaingilia kati mjadala huu na kwa bahati mbaya, ndugu huyu alishuka katika eneo ambalo kulikuwa na ujenzi mkubwa wa Kiwanja cha Michezo. Hivyo Mwanakwetu hakupata nafasi ya kusikia zaidi ya hapo.

 

Lakini maneno haya ya ndugu kwa uchache wake yalitosha kunirudisha nyuma katika historia.

Mwanakwetu akiwa safarini akamkumbuka Padri Fidelis wa Mbagala na ujenzi wa Shule ya Mtakatifu Antony wa Padua mwishoni mwa mwaka 1989 kama nilivyosimulia awali.

 

Mwanakwetu akajiambia:

 

“Padri Fidelis alipokuwa anasimamia ujenzi ule, aliifanya kazi yake kwa moyo wote. Hoja ya ujuzi wake wa ujenzi siifahamu. Lakini jambo moja nalifahamu: alikuwa na moyo wa kufuatilia.”

 

Na hapa ndipo tunapofika kwenye hoja kubwa.

Mwanakwetu aliposhuka ndani ya basi lile akasema moyoni:

 

“Sasa wewe leo hii upo katika taasisi ya umma. Pembeni yako kuna ujenzi mkubwa unaofanyika. Wewe ndiye mwenye dhamana ya mradi huo kwa niaba ya umma. Je, unajua kinachoendelea? Unaweza kuwa unasimamia ujenzi wa mabilioni ya fedha, lakini hujawahi hata kupita eneo la mradi kuangalia kinachoendelea. Huna moyo wa kufuatilia. Huna muda wa kuuliza.Huna hamu ya kujua.Huna hata ujasiri wa kumhoji mkandarasi.Lakini kila mwisho wa mwezi mshahara unaingia.

Hapo ndipo Mwanakwetu nasema:

HATUWEZI KWENDA HIVYO!

Padri Fidelis, hata kama hatujui alikuwa na kiwango gani cha utaalamu wa ujenzi, alifika eneo la mradi mara tatu kwa siku. Sasa wewe pangu pakavu tia mchuzi una elimu.Una nafasi.Una mshahara.Una mamlaka.Una wataalamu pembeni yako.Una mkandarasi.Una mshauri wa mradi.Una fedha za umma.

Lakini HUNA MOYO WA KUFUATILIA?Sisi watu wa Mbagala hatuna nguvu nguvu yetu kukupiga laana, kukutusi ili hubadilike.Huo si uzembe tu.Huo ni uzembe unaogusa moja kwa moja dhamana ya umma.

Baraka ulizojaliwa, ofisi uliyopewa, suti unayovaa, tai unayofunga, viatu unavyong'arisha na gari unalotumia, kinyoyozi unachotumia ofisini kwetu, na karani wetu anayekuhutumia havikufanyi uwe msimamizi wa mradi.

 

Kinachokufanya uwe msimamizi ni uwajibikaji wako.Unaweza usiwe mhandisi.Unaweza usiwe fundi.Lakini lazima uwe na moyo wa kuuliza.

“Mbona mmejenga hivi?”

“Kwa nini mmeweka hivi?”

“Kwa nini kazi imechelewa?”

“Kwa nini vifaa hivi vimetumika?”

“Kwa nini fedha hizi zimetumika?”

“Kwa nini ubora wa kazi hii hauko sawa?”

Hapo ndipo usimamizi unapokuwa usimamizi.

 

Nyinyi mnaovaa suti na wakati mwingine mashati ya vitenge, majumbani kwenu hamjengi?Nawauliza tena majumbani kweni hamjengi?

La sivyo, utakuwa kiongozi kuvaa suto tu.

 

Hodari sana wa kusema maneno haya:

“Naomba kwenye mlango wa mbele wa nyumba yangu niwekee kitasa cha automatiki nikifika tu kitasa kinafunguka, weka kiyoyozi vyumba vyote, usiweke sakatu ya kawaida weka tairisi za Marekani….nyinyi nyinyi tunawaona…”

 

Serikali inatoa fedha zote za mradi.Utaratibu wa sasa unampa mkandarasi mshauri.Wataalamu wapo.Mikataba ipo.Fedha zipo.Lakini mradi unajengwa vibaya.Makosa yanaachwa.Kazi inachelewa.Baadaye inaibuka hoja ya kubomoa sehemu iliyojengwa.Hili linatokeaje?Linapotokea, nani anawajibika?Mkandarasi?Mshauri?Msimamizi?Mkuu wa taasisi?Au kila mtu ananyosha kidole kwa mwenzake?

Hapana! Dhamana ya umma si mahali pa kujificha.

Kama ulikabidhiwa kusimamia mradi na hukusimamia, unapaswa kuwajibika.Kama uzembe wako umeongeza gharama za mradi, unapaswa kuwajibika.Kama uzembe wako umechelewesha mradi, unapaswa kuwajibika.Kama uliona kosa ukakaa kimya, unapaswa kuwajibika.

Na kama ulijua lakini ukaamua kutofuatilia kwa sababu ulikuwa busy kuvaa suti na kukaa ofisini, basi usishangae wananchi wakakuuliza:

“Suti yako imesaidia nini katika kujenga jengo hili?”

Mwanakwetu anasema wazi:

Watu wanaosababisha hasara ya umma kwa uzembe wao hawapaswi kulipwa kana kwamba wamefanya kazi nzuri.Hasara inayotokana na uzembe wa mtendaji haipaswi kuishia kwenye taarifa za ukaguzi pekee.Lazima uwajibikaji ufuate.

Sasa jamani, wale wenye tabia hizi mnaoyasoma makala haya, nawaombeni:

BADILIKENI!

Jifunzeni kwa John Pombe Magufuli.Jifunzeni kwa Padri Fidelis.Si lazima uwe mhandisi ili uwe msimamizi mwenye moyo.Si lazima ujue kila kitu.Lakini lazima uwe na nia ya kujua.

Si lazima ujenge mwenyewe.Lakini lazima ufuatilie anayejenga.Si lazima uwe fundi. Lakini lazima uwe na uwezo wa kuuliza.

Mwanakwetu upo?

Vinginevyo tutamuomba Mungu awachukue mapema ili mkaadhibiwe.

Kumbuka:

“HODARI WA KUBADILISHA SUTI.”

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

 






















0/Post a Comment/Comments