Adeladius Makwega – MBAGALA
Dkt. Ayub Ryoba, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (SHIUTA) kuanzia mwaka 2016 hadi mapema mwaka 2026, hivi karibuni ameonekana kuwa mchangamfu katika mitandao ya kijamii kama alivyokuwa awali kabla ya kukabidhiwa jukumu la kuliongoza shirika hilo la Watanzania karibu milioni 72.
Kuibuka kwa kasi kwa Dkt. Ryoba na kuanza kutoa maoni mbalimbali mitandaoni hakukumpa mashaka Mwanakwetu, maana huyu ndiye ndugu Ayub Ryoba anayemfahamu. Lakini kilichombebesha mzigo wa mashaka Mwanakwetu ni ukimya wa Dkt. Ryoba katika kipindi cha miaka kumi akiwa analiongoza Shirika la Utangazaji Tanzania. Je, ndugu huyu alirogwa na nani hadi kutengeneza taswira nyingine ya kivuli cha Dkt. Ayub Ryoba ambaye wengi hawakumfahamu?
Akilini mwa Mwanakwetu, wakati anaandika makala haya, alikumbuka mengi kuhusu Dkt. Ayub Ryoba katika siku zake za mwanzo alipowasili kuhudumu ndani ya SHIUTA.
Awali aliteuliwa na Waziri wa Habari wa wakati huo kuwa mjumbe wa Bodi ya SHIUTA. Akiwa mjumbe wa bodi hiyo, nilikuwa Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa TBC. Nilifunga safari hadi Chuo Kikuu alichokuwa anafundisha nikiwa na Malima Ndelema, ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa RAAWU, Tawi la TBC Makao Makuu. Tulimwelezea hali ya TBC wakati huo.
Tulipofika chuoni, nilimuona dada mmoja aliyemfuata darasani, naye Dkt. Ayub Ryoba alikuja akiwa amevaa makubadhi na akiwa na sigara mkononi. Alizungumza nasi vizuri na kuyapokea yote tuliyomweleza, akisema angeshirikiana na Mwenyekiti wa Bodi ya TBC wa wakati huo, ambaye alikuwa Balozi Mstaafu.
Tulipokuwa njiani kurejea, Malima Ndelema alikuwa na matumaini makubwa sana kuhusu Dkt. Ryoba. Aliniambia alikuwa mwalimu wake katika Chuo cha Habari.
Hii ndiyo taswira ya kwanza iliyonijia.
Nakumbuka kuwa barua ya kwanza kabisa aliyoisaini Dkt. Ayub Ryoba ilikuwa ya kumfukuza Mwanakwetu kazi kwa madai ya makosa mawili ya insubordination. Makosa hayo yalidaiwa kufanyika katika kikao cha wafanyakazi na pia katika kikao cha Waziri wa Habari, wakati hoja hizo zilitolewa mbele ya viongozi na mtoa hoja akiwa Mwenyekiti wa Wafanyakazi kwa maslahi ya wafanyakazi.
Barua hiyo ya Aprili 2016 ilisababisha Mwanakwetu kutofanya kazi na Dkt. Ryoba, wakati hapo awali wafanyakazi wengi waliamini kuwa Dkt Ryoba angekuwa msaada mkubwa kwao. Kwa hakika, akiwa SHIUTA, Dkt. Ryoba alifanya kazi kwa ukaribu sana na baadhi ya wanafunzi wake aliowahi kuwafundisha kozi ya uandishi wa habari, ambapo yeye ni miongoni mwa wasomi wa mwanzo kabisa wa taaluma hiyo wenye Shahada ya Uzamivu ambapo wanafunzi wake wengi bado wanaitumikia TBC.
Kwa hakika, wazee wa RTD walipoona Dkt. Ryoba amesaini barua ya kumfukuza kazi Kiongozi wa Wafanyakazi, walitoa kauli ifuatayo:
"Huyu jamaa hawezi kuliongoza shirika hili vizuri. Chairman Makwega alipokuwa anatoa hoja zake, Dkt. Ryoba hakuwepo. Jambo hili lilipaswa kuamuliwa kwa hekima na kwa kuheshimu chama cha wafanyakazi. Hii imetumika kama silaha ya kuwatisha watumishi wengine. Ngoja tuone."
Hili ndilo jambo la pili linalomjia Mwanakwetu kuhusu Dkt. Ayub Ryoba, Mtanzania mwenye asili ya Mkoa wa Mara na Mkristo Msabato.
Kwa hakika, Mwanakwetu anaunga mkono msimamo wa Dkt. Ryoba wa kuwa mchangamfu katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Hata hivyo, Mwanakwetu anasikitishwa na hali ilivyokuwa kwa kipindi cha miaka kumi, kuanzia Aprili 2016 hadi Aprili 2026. Kama mbinu hii ya uchangamfu angeitumia akiwa madarakani katika kuboresha TBC kwa kuanzisha vipindi bora, vyenye mvuto na vinavyogusa jamii, jambo hilo lingekuwa na manufaa makubwa kwa SHIUTA na Watanzania kuliko maamuzi yake ya sasa.
Kwa hakika, makala haya hayana shabaha ya kumziba domo, kumzodoa, kumng’ong’a Dkt. Ryoba. Lengo ni kutafakari hali ilivyokuwa, matumaini ambayo watu na Watanzania walikuwa nayo kwake, hasa sisi tuliomwona kwa karibu alipokuwa anapiga hodi SHIUTA, na ili wengine wajifunze.
Kwa hakika, uboreshaji wa vipindi vya TBC ulifanywa vizuri na Mkurugenzi wa kwanza wa TBC, Tido Mhando. Yeye ndiye aliyeunganisha TVT na Radio Tanzania na kuunda TBC. Katika kipindi chake, TBC ilianzisha vipindi vipya na vyenye ubunifu na ubora mkubwa. Baadaye, Mkurugenzi Clement Mshana na Dkt. Ryoba waliinufaika na msingi huo, lakini nyota hiyo iliendelea kupoteza mng'ao wake katika kipindi cha miaka 16 tangu kuondoka kwa Tido Mhando.
Mwanakwetu anaamini kuwa jukumu la Dkt. Ryoba lilikuwa kuhakikisha taa ya TBC inawaka zaidi. Badala yake, kwa mtazamo wa Mwanakwetu, katika miaka yake kumi ya uongozi, alikuwa kama mtu anayepunguza kuni katika mafiga ili moto uzimike na kufanya chakula kipakuliwe kikiwa hakijaiva vizuri.
Leo hii Dkt. Ryoba anajaribu kurudisha kuni mekoni wakati mwenye jiko tayari amechukua jiko lake. Moto huo hauwezi kuwaka vizuri. Huko ulipo na kuni zako mvua inanyesha; kuni zimeloana, hivyo moto hauwezi kuwaka.
Mwanakwetu analinganisha hali hiyo na jini lililokuwa nje ya chupa likapewa nafasi kuingia ndani ya chupa, lakini lilipoingia likashindwa kufanya kazi. Sasa liko nje ya chupa; je, linaweza kufanya chochote? Abadani. Miaka kumi ya kula ugali mbichi iweje leo hii uje na hoja ya ugali ulioiva?
Vilevile ni kama zimwi lililokuwa nje ya mbuyu likaingizwa ndani ya mbuyu, likashindwa kufukuta ndani ya mbuyu mkubwa. Je, litaweza kufukuta nje ya mbuyu mchanga?
Mwanakwetu anajiuluza je kwa sasa Dkt. Ryoba anapaswa kuwa mtulivu? Uhuru wa kutoa maoni ni haki yake, lakini hakuitumia ipasavyo akiwa ndani ya "chupa ya jini" na akiwa ndani ya "mbuyu mkubwa". Hili ni deni ambalo, kwa mtazamo wa Mwanakwetu, bado linamkabili. Kama kuna anayejua namna linavyoweza kulipwa, naomba anisaidie.
Mwanakwetu hayasemi haya kwa sababu ya ile barua ya Aprili 2016. Hapana. Dkt. John Pombe Magufuli alifunga ukurasa huo, na hata tunapokutana mimi na wewe Dkt Ryoba huwa tunazungumza vizuri kama mtu na kaka yake katika taaluma. Hoja ya msingi ni ukimya wa miaka kumi, ambao unaibua maswali mengi. Je, watu wanapokuwa madarakani hawapaswi kuzungumza? Je, unatoa funzo gani kwa wanafunzi wako uliowafundisha uandishi wa habari ambao wako SHIUTA je waishi kama wewe ulivyoishi?
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Dkt. Ryoba, uzoefu wako katika taaluma ya habari, ualimu na uongozi ni rasilimali muhimu kwa taifa. Sasa ukiwa nje ya jukumu la uongozi wa SHIUTA, endelea kutumia uhuru wako wa kutoa maoni kwa kujenga sekta ya habari kwa kutoa mawazo, kufanya tafiti, kuandika makala na kuwalea waandishi wa habari na viongozi wanaokuja.
Hata hivyo, ni muhimu pia kutafakari kwa uwazi kipindi chako cha uongozi. Kila kiongozi huacha mafanikio na maeneo yanayohitaji kujifunza. Kukubali kujadili kwa uwazi yaliyofanyika, changamoto zilizokuwepo na maamuzi yaliyofanywa ni sehemu ya uongozi wenye uwajibikaji na urithi mzuri kwa vizazi vijavyo.
Watanzania wengi walikuwa na matarajio makubwa kwako kutokana na historia yako ya kitaaluma. Kwa hiyo, maoni yako ya leo yatakuwa na uzito zaidi ikiwa yataambatana na tafakuri ya uongozi ulioupitia na mafunzo uliyoyapata. Hilo litawasaidia viongozi wa sasa na wa baadaye kuelewa kuwa uongozi ni nafasi ya kutumikia umma, kujifunza na kuacha taasisi ikiwa imara zaidi kuliko ulivyoikuta.
Nakutakia kila la heri katika hatua mpya ya maisha yako, na ninatumaini utaendelea kuitumikia taaluma ya habari na Taifa kwa hekima, uadilifu na uwazi bilakuchoka mpaka pumzi ya mwisho.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Ukimya wa Miaka Kumi na Sauti ya Leo ya Dkt. Ayub Ryoba.”
Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257
.gif)



.gif)
Post a Comment