TBC ISIJIDANGANYE KWA JINA LA SERIKALI

 




Adeladius Makwega – Mbagala

 

Msomaji wangu, nakuomba nikusimulie kisa hiki.

 

Siku moja tulikuwa katika kikao chenye wajumbe kadhaa kwa ajili ya maandalizi ya shughuli iliyokuwa irushwe na vyombo vya habari. Mapendekezo yakaanza kutolewa kuhusu vyombo vya habari vitakavyoalikwa. Kila chombo kilitajwa kimoja baada ya kingine.

 

Ilipofika zamu ya TBC, mjadala ukaibua swali moja:

"Ni nani miongoni mwenu ambaye amewahi kuitazama TBC, kuisikiliza redio yake au kutembelea mitandao yake ya kijamii hivi karibuni?"

 

Kikaoni, mjumbe mmoja tu alijitokeza. Yeye alisema kila siku husikiliza kipindi cha Usia wa Baba, kinachorusha vipande vya dakika tano vya hotuba za Hayati Julius Kambarage Nyerere.

 

Baada ya mjadala, wajumbe wengi walikubaliana kuwa TBC isialikwe. Hata hivyo, mama mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa shughuli hiyo na ndiye aliyekuwa akiigharamia, akasema:

"Hapana, tuialike TBC. Viongozi watajiona. Najua sisi hatuitazami, lakini viongozi lazima wajitazame."

 

Hapo yule mjumbe aliyekuwa amesikiliza kipindi cha Usia wa Baba akaungwa mkono na mama huyo mfadhili, na hatimaye TBC ikaalikwa.

 

Yule jamaa aliyekuwa amesikiliza Usia wa Baba alikuwa ni Mwanakwetu, ambaye ni mdau wa TBC kwa sababu nyingi. Kati ya sababu hizo ni kwamba aliwahi kufanya kazi TBC, na wafanyakazi wenzake walimchagua kuwa Mwenyekiti wa Wafanyakazi.

 

Shughuli hiyo ilifanyika vizuri, na vyombo vyote vya habari vilivyoalikwa, ikiwamo TBC, vilishiriki kikamilifu.

 

Baada ya shughuli hiyo, Mwanakwetu akaanza kujiuliza maswali mengi.

 

Miongoni mwao ni hili:

"Mwaka 2016 TBC ilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 600 wenye ajira za kudumu na mikataba. Hivi kama mtazamo huu kwamba TBC haijishughulishi vya kutosha na mambo ya umma utaendelea, mwisho wake utakuwa nini? Nilikuwa Mwenyekiti wa Wafanyakazi. Inawezekana ikafika siku TBC ikavunjwa, wafanyakazi wakalipwa stahiki zao, lakini nani ataumia zaidi kama si wale wafanyakazi zaidi ya 600? Hivi hawa jamaa zangu wa TBC wanayafikiria haya?"

 

Mara nyingi, kabla ya taasisi kuundwa huwa kunakuwa na mijadala mingi. Vivyo hivyo, kabla ya taasisi kubomolewa pia huwa kunakuwa na mijadala mingi.

 

Mara nyingi husikika malalamiko kama haya:

 

"Wanapokuja katika mikutano yetu, tukianza kutoa hoja kamera wanazihamishia studio. Hawatupi nafasi ya kutoa maoni. Wao wanawapa nafasi viongozi tu."

 

Maneno ya aina hii yanapaswa kubadilika mara moja.

Ikumbukwe kwamba TBC iliundwa kwa sheria, na pia inaweza kubadilishwa au kuvunjwa kwa sheria. Msingi wa sasa wa kisheria ni Tanzania Broadcasting Corporation Act, No. 3 of 2025. Kabla ya hapo, kuanzia mwaka 2007 hadi 2025, TBC iliendeshwa chini ya Public Corporations Act, 1992 kupitia Government Notice Na. 186 ya mwaka 2007.

 

Kwa hiyo, ukiwa mkuu wa taasisi kama TBC, ni lazima ufahamu kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini (Employment and Labour Relations Act, CAP. 366), mwajiri hawezi kumfukuza au kumwondoa mfanyakazi kwa sababu tu hana tena mahitaji naye bila kufuata taratibu za sheria.

 

Ni kweli kwamba mwajiri anaweza kusitisha ajira ikiwa hana tena uhitaji wa nafasi ya mfanyakazi kutokana na sababu za kiutendaji, kama vile biashara kupungua, mabadiliko ya teknolojia au marekebisho ya muundo wa taasisi. Hata hivyo, sheria inaruhusu jambo hilo chini ya misingi ya operational requirements (redundancy/retrenchment), lakini masharti yake lazima yafuatwe.

 

Masharti hayo ni pamoja na kuwa mwajiri awe na sababu halali na ya haki ya kusitisha ajira; afuate utaratibu wa haki, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na kufanya mashauriano pale inapohitajika; atoe notisi ya kusitisha ajira au malipo badala ya notisi kwa mujibu wa sheria au mkataba wa ajira; na amlipe mfanyakazi stahiki zake zote, ikiwamo mshahara unaodaiwa, malipo ya likizo ambayo hayajatumika pale inapostahili, pamoja na severance pay pale sheria inapohitaji.

 

Sheria pia inasema kuwa kusitisha ajira kutahesabika kuwa si kwa haki (unfair termination) endapo mwajiri atashindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na sababu halali, sababu hiyo ilikuwa ya haki kwa kuzingatia tabia au uwezo wa mfanyakazi au mahitaji ya uendeshaji wa mwajiri, na kwamba utaratibu wa haki ulifuatwa.

 

Msomaji wangu, rejea sana maneno haya niliyoyaweka kwenye mabano:

 

"Kwa mfano biashara imepungua, mabadiliko ya teknolojia au marekebisho ya muundo wa kampuni; sheria inaruhusu kusitisha ajira kwa sababu za operational requirements (redundancy/retrenchment)."

 

Pia yakumbuke maneno haya:

 

"Wanapokuja katika mikutano yetu, tukianza kutoa hoja kamera wanazihamishia studio. Hawatupi nafasi ya kutoa maoni. Wao wanawapa nafasi viongozi tu."

 

Maneno ya aina hii yanapoendelea kusikika bila kuwepo mabadiliko ya tabia, yanaweza kuifanya sheria ya ajira na mahusiano kazini kuanza kufanya kazi pale ambapo mazingira ya kiutendaji yanabadilika.

 

Ndiyo maana mwanahabari mmoja mwenye asili ya Tanzania anayeishi Marekani aliwahi kuniambia:

"Wakati umefika Serikali ya Tanzania iache kumiliki vyombo vya habari ili kuondoa lawama dhidi yake. Huku Marekani, VOA ipo kwa ajili ya propaganda za nje za taifa lao, lakini ndani haina nafasi hiyo. Rasilimali za TBC zinaweza kuwekwa chini ya TCRA na kukodishwa kwa wadau wanaotaka kufanya biashara hiyo, au kama hilo haliwezekani, zinaweza kuuzwa kwa mnada ili serikali ikajielekeze katika majukumu mengine."

Msomaji wangu, rejea pia kauli hii:

 

"Hapana, tuialike TBC. Viongozi watajiona. Sisi hatuitazami, lakini viongozi lazima wajitazame."

 

Katika kikao cha watu 15, mjumbe mmoja tu ndiye aliyekuwa akiunga mkono TBC, kisha akaungwa mkono na yule mama aliyekuwa mfadhili wa shughuli hiyo. Hili ni jambo ambalo viongozi wa TBC wanapaswa kulitafakari kwa kina.

 

Ndiyo maana ninaamini kuwa Dkt. Ayub Ryoba, akiwa mmoja wa wasomi wa taaluma hii, anapaswa kukubali ukweli kwamba historia itatoa tathmini yake kuhusu uongozi wa shirika hili. Huo ni mjadala wa wazi unaostahili kufanywa kwa kuzingatia matokeo na maslahi ya umma.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwisho wa yote, viongozi wa TBC, wafanykazi wezangu wa zamani pale TBC na Wizara husika  haimaswi kuamini kwamba TBC itaendelea kuwepo kwa sababu tu ni taasisi ya serikali. Historia inaonyesha kuwa taasisi hujengwa kwa sheria, hukua kwa kuaminiwa na wananchi, na zinaweza kubadilishwa au hata kufutwa kwa sheria pale zinaposhindwa kutimiza matarajio ya umma. Hivyo, viongozi na wafanyakazi wa TBC na wizara husika wanapaswa kutafakari kwa kina sauti zinazotoka kwa wananchi, wadau na wataalamu wa habari, kwa sababu malalamiko yanaporudiwa kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi, huwa yanageuka kuwa hoja za msingi za kufanya mageuzi makubwa ya taasisi.

 

Mwanakwetu hana lengo la kuiona TBC ikiporomoka; anatamani kuiona ikirejea kuwa chombo cha habari kinachoaminiwa, kinachowapa nafasi Watanzania wote, kinachosimamia taaluma na kinachotumikia maslahi ya umma bila upendeleo. Huo ndio urithi ambao waanzilishi wa shirika hili waliutarajia, na huo ndio wajibu wa viongozi wa leo kuutunza. Maana taasisi haihifadhiwi kwa sheria pekee, bali kwa uadilifu wa uongozi, ubora wa huduma na imani ya wananchi wanaoitazama, kuisikiliza na kuiona kuwa sauti yao.

Mwanakwetu upo ?Kumbuka

“TBC Isijidanganye kwa Jina la Serikali.”

Nakutakia siku njema.

 

Barua pepe:

makwadeladius@gmail.com

Simu: 0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments