“Waziri ameagiza hatua za kinidhamu—lakini je, ameamuru mtu afukuzwe?”
Adeladius Makwega – MBAGALA
“Hii taarifa kwa umma ipo vizuri sana. Kwa mtazamo wangu, haina maana kwamba mtumishi husika tayari amehukumiwa. Hata kama baadaye atafukuzwa, jambo la msingi litakuwa kama mchakato wa kinidhamu ulifuata sheria.”
Hayo ni maoni ya mdau mmoja aliyewahi kufikia ngazi ya Ukurugenzi katika taasisi kubwa ya umma nchini, aliyatoa kwa njia isiyo rasmi baada ya taarifa ya Wizara ya Ardhi kusambaa katika kundi la MwAnAkWeTu tarehe 13 Agosti 2026.
Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Afisa Habari wa Wizara, Eleutheri Mangi, ilieleza hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Ardhi baada ya malalamiko ya wananchi wa Bahari Beach kuhusu matumizi ya ardhi yanayodaiwa kwenda kinyume na mpango wa matumizi ya eneo hilo.
Kilichotikisa mjadala ni agizo la Waziri kwamba mtumishi anayehusika asimamishwe kazi na achukuliwe hatua za kinidhamu.
Lakini swali likabaki:Je hili ni agizo la kumfukuza kazi?
Kisheria, jibu ni hapana—si moja kwa moja.
Kwa mtumishi wa umma, Public Service Act, Cap. 298 R.E. 2023 inaweka utaratibu maalumu kabla ya dismissal. Lazima kuwe na charge, mtumishi apewe nafasi ya kujibu, na inquiry ifanyike kwa mujibu wa kanuni.
Kwa lugha nyepesi:
Maagizo ya Waziri → Uchunguzi → Charge → Majibu ya mtumishi → Inquiry → Uamuzi.Hapo ndipo sheria inapoweka mizani.
Ikiwa uchunguzi utabaini kwamba mtumishi alikiuka taratibu kwa uzito, alitumia vibaya mamlaka, au alihusika katika kitendo kinachostahili adhabu kali, dismissal inaweza kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa.
Lakini kama ushahidi utaonyesha kwamba hakuhusika, hakuwa na mamlaka ya kufanya uamuzi huo, au mazingira hayafikii kiwango cha kosa la dismissal, sheria bado inamlinda apewe haki ya kusikilizwa.
Swali ni je Barua ya Waziri siyo hukumu? Hili ndilo jambo ambalo huenda likapotea katika mjadala wa mitandao.
Waziri anaweza kuagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe, lakini hilo halimaanishi kwamba mtumishi tayari amepatikana na hatia.Ndiyo maana kuna tofauti kubwa kati ya kusema:
“Waziri ameagiza mtumishi achukuliwe hatua za kinidhamu.”
na kusema:
“Mtumishi amepatikana na hatia na anapaswa kufukuzwa.”
Ya kwanza ni taarifa inayoweza kuthibitishwa kwa barua ya Waziri; ya pili ni hitimisho ambalo linapaswa kusubiri mchakato wa kisheria.
Hapo ndipo uwajibikaji na haki vinapokutana na taarifa hii ikiwa imechapishwa?
Kwa mtazamo wa mdau mwingine, publication hii kusambaza inaweza kuwa na faida katika kuhakikisha kwamba maagizo ya Waziri hayabaki kwenye karatasi.
Wananchi wanaweza kufuatilia:
“Je, uchunguzi umefanyika?Je, mtumishi alipewa nafasi ya kujitetea?Je, timu ya wataalamu ilifanya kazi yake kwa weledi?Na mwisho wa yote—nini kilibainika? Maana utumishi wa umma ni mali ya Watanzania kama yalivyo madini haiwezekani waziri auchukue mpira akiwa mwenyewe,kutoka goli lake akijipige chenga mwenyewe, ajipige kanzu mwenyewe na kisha akafunge goli yeye mwenyewe,”
Kwa hiyo huo siyo uamuzi wa kumfukuza mtu.Huu ni uwajibikaji kwa umma.
Mwanakwetu anasema,Mjadala huu haupaswi kuishia kwenye swali la:
“Atatimuliwa au hatatimuliwa?”
Swali kubwa zaidi ni:
“Je, maagizo ya Waziri yatafuatwa, uchunguzi utafanyika kwa haki, na ukweli utajulikana?”
Kama mtumishi amekosea, sheria ichukue mkondo wake.
Kama hakukosea, apewe haki yake.
Na kama atafukuzwa, bado sheria inampa njia za kukata rufaa kulingana na utaratibu wa Utumishi wa Umma.
Kwa kifupi: Barua ya Waziri ni mwanzo wa mchakato—si mwisho wa hukumu.
Hitimisho;
“Pongezi kwa Afisa Habari wa Wizara ya Ardhi, Eleutheri Mangi, kwa taarifa hii iliyowasilishwa kwa wakati na kwa uwazi. Si taarifa tu, bali imefungua mjadala muhimu kuhusu uwajibikaji na utekelezaji wa maagizo ya Serikali.”
Aridhi ni Mali ,Utumishi wa Umma ni Hazina na Sheria ni mlinzi.
Mwanakwetu upo ? Kumbuka:
“Taarifa ya Ardhi Yafungua Mjadala.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
.gif)


.gif)
Post a Comment