Adeladius Makwega – MBAGALA
“Kaka Makwega, changamoto kubwa ya Watanzania wa leo si kingine bali ni kitu kimoja tu: wananchi wengi wanawatazama viongozi wao wa leo kuwa wabinafsi, hawana utu na hawajali maslahi ya walio wengi. Wakati viongozi wa awali wa Watanzania hii hii hawakuwa na tabia hizi za viongozi wa sasa.”
Mwanakwetu akasema:
“Hoja lazima iwe na ushahidi. Wewe unayoyasema haya, una ushahidi gani?”
Ndugu huyu akajibu:
“Mwanakwetu, unataka ushahidi? Kifua unacho?”
Mwanakwetu akajibu:
“Ninacho.”
Huku akijipiga kifuani mara tatu.
Mwanakwetu akauhitaji huo ushahidi. Jamaa akasema:
“Nitakupa namba za simu za watu watatu. Ongea nao—huyu, huyu na huyu. Wao watakuwa mashahidi wa hili.”
Mwanakwetu akamuuliza:
“Kwani hoja ni nini?”
Jamaa akaanza kueleza:
“Makwega, wewe umefanya kazi na TAMISEMI kwa ngazi mbalimbali; awali ukiwa Afisa Elimu Msaidizi, baadaye Afisa Habari na pia Mkurugenzi Mtendaji. Unatambua kuwa Wizara hii inasimamia kwa karibu michezo ya aina tatu: UMITASHUMTA—Umoja wa Michezo na Taaluma wa Shule za Msingi; UMISSETA—Umoja wa Michezo na Taaluma wa Shule za Sekondari; na SHIMISEMITA—Mashindano ya Shirikisho la Michezo na Sanaa kwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania. Ndugu, hapa nilipo natoka katika mashindano haya yaliyoanza Agosti 14, 2026 na yanatarajia kumalizika Agosti 29, 2026. Ni mashindano ya wiki mbili. Katika uzinduzi, tulitarajia aje Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, lakini baadaye alikuja Waziri wa TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe.Yote tisa, kumi: kundi kubwa la washiriki kutoka nchi nzima, ambao ni watumishi wa TAMISEMI, hadi sasa hatujalipwa posho zetu za siku 15. Baadhi wamelipwa posho ya shilingi 80,000 kwa siku na wengine shilingi 100,000 kwa siku. Na waliolipwa angalau ni wale wanaotokea hasa katika Halmashauri za D
ar es Salaam.”
Mwanakwetu akawa anamsikiliza ndugu huyu kwa makini sana.
Jamaa akaendelea:
“Imefika siku ya uzinduzi, baadhi ya Halmashauri hatukuwa hata na traki suti wala vifaa vya michezo. Ikabidi tulipofika uwanjani ndipo gari likaja na traki suti; tukavaa uwanjani. Watu wengine wanatucheka. Posho tumeshindwa kulipwa hadi sasa. Hata vifaa vya michezo tunashindwa kuvipata. Kuna faida gani ya kuendesha mashindano katika hali kama hii?”Je, nikivunjika mguu nitapata huduma yoyote? Au kwa sababu mimi ni mtumishi na nina bima ya afya, basi mambo yataishia hapo?”
Jamaa huyu akaendelea:
“Hata kama angekuja Waziri Mkuu kufanya ufunguzi, mambo yangekuwa yale yale. Hata maji ya kunywa wakati wa michezo tunanunua kwa pesa zetu. Chakula kambini ni kidogo; hatushibi. Afadhali jana tumepata mishahara kidogo, imekuwa nafuu kwa sababu tunapasua mifuko yetu wenyewe.”
Baadaye Mwanakwetu akaunganishwa na watu wale watatu waliotajwa kuwa mashahidi.
Mmoja wao akasema:
“Kaka, mimi nafuga sana nguruwe. Nilipokuja kambini, ilibidi nimpe mtu majukumu ya kutunza nguruwe zangu. Ninamlipa shilingi 10,000 kwa siku. Kwa siku 15 ni shilingi 150,000.Angalau ningepata posho ya shilingi 100,000 kwa siku, ningepata shilingi 1,500,000. Hapo kutoa laki moja na nusu siyo shida. Tatizo ni kwamba mpaka sasa sina hakika kama nitaipata hiyo pesa yangu au ndiyo yale ya ‘kilichokwenda kwa mganga hakirudi’? Sijalipwa kitu, na hii ni Agosti 25, 2026. Je, nitapata chochote baada ya mashindano kumalizika? Tunafanya vikao vingi, lakini hakuna majibu.”
Simu ya Mwanakwetu ghafla ikakata chaji. Mwanakwetu akiwa chumbani kwake akatafakari sana hali hii.Akakumbuka pia ziara za Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, alizofanya hivi karibuni.Katika mkoa mmoja, kuna mtu aliwahi kumuuliza Mwanakwetu swali hili:
“Waziri Mkuu anafanya ziara siku nzima. Yeye chakula anakula wapi?”
Mjadala ukawa mkubwa sana.Mtu mwingine akauliza:
“Au wanafungashiwa vifurushi ndani ya magari yao?”
Kisha akatoa hoja:
“Kama ni hivyo, wanakosea sana. Ni vizuri Waziri Mkuu awe anakula chakula cha wananchi. Kipikwe chakula cha wananchi wote, kisha naye ale pamoja nao. Hili litaonyesha udugu baina yetu Watanzania.Utasema mimi ni ndugu yenu kwa maneno? Maneno hayatoshi. Ndugu, mnakula pamoja na mnakaa pamoja naye.”
Mwanakwetu akatafakari sana hoja hii ya kuwajali wengine kwa vitendo, hasa kwa mifano aliyokuwa ameipata. Akajiuliza: Tumeacha wapi utu huu?
Hata Yesu alipokuwa akifundisha, ilifika wakati akatoa alichokuwa nacho kuwapa makutano. Hizi ni simulizi za zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Leo tunakwama wapi?
Labda msomaji wangu nikupeleke katika pilau iliyobeba kumbuku ya miaka 40 .
Mwanakwetu akakumbuka tukio moja ambalo kwake bado ni hai mpaka leo.
“Nakumbuka mwaka 1984, Rais wa Zanzibar, Mhe. Ali Hassan Mwinyi, akiwa Rais wa Zanzibar, alifika katika Kijiji cha Kimanzichana, Mkuranga, Pwani, na kufanya mkutano mkubwa.Ilikuwa imepikwa pilau tele na ng’ombe kadhaa walichinjwa.”
Mwanakwetu wakati huo akiwa darasa la pili, alikula pilau hilo. Na leo, baada ya takribani miaka 40, bado analikumbuka.
Pilau la Rais wa Zanzibar Kijijini Kimanzichana.
Hili si suala la pilau pekee.
“Ni suala la kumbukumbu. Ni suala la utu. Ni suala la kuwajali watu.Ni suala la kiongozi kuwa karibu na wananchi wake.”
Ndugu yetu Mwigulu Nchemba, tunawaacha watu na njaa—labda shibe ya maneno.
Tunatumia gharama kubwa katika maturubai, mapicha na michoro mingi na mambo mengine, chakula kina gharama gani? Lakini wakati mwingine, kinachoweza kubaki katika mioyo ya wananchi si ukubwa wa maturubai, piha na sanamu za viongozi wala gharama za maandalizi, angalia namna ulivyokula nao ulivyoongea nao.Kisa cha mwaka 1984 cha marehemu Ali Hassan Mwinyi nakumbuka pilau siyo kwa kwasababu Mwanakwetu ni mmelo la hasha bali tulikula chakula na Rais wa Zanzibar.
Kinachobaki ni namna ulivyowagusa.
Kiongozi anapokaa na wananchi, akala nao, akasikiliza shida zao na akashirikiana nao, anajenga kitu ambacho hakipimwi kwa fedha: Hata katika mazingira ya sasa, ambapo mahitaji na taratibu za kiutawala ni tofauti na zamani, utu, heshima na kujali wananchi havipaswi kupitwa na wakati. Kwa hiyo, tunapozungumzia posho za watumishi, chakula kambini, maji ya kunywa, vifaa vya michezo na usalama wa washiriki, tusione haya kama mambo madogo.Nyuma ya kila posho kuna mtumishi. Nyuma ya kila mtumishi kuna familia.Nyuma ya kila malalamiko kuna maisha ya mtu. Ikiwa mashindano yameandaliwa kwa ajili ya watumishi, basi watumishi hao wanastahili kuheshimiwa na kutunzwa ipasavyo.
Mwanakwetu, upo?
Kumbuka:
“PILAU YA RAIS WA ZANZIBAR
KIJIJINI KIMANZICHANA.”
Tubadilike, jamani.
Nawatakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
NB: Makala haya yafike katika Ofisi ya Waziri Mkuu na pia Ofisi ya Waziri wetu wa TAMISEMI, kwa ajili ya kuyafanyia kazi malalamiko na hoja zilizotolewa na washiriki wa mashindano haya.
.gif)










.gif)
Post a Comment