MZEE WA SARAFU NA SWALI LA IMANI KWA ASKARI WETU

 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Kondakta, tangu asubuhi hujafanya biashara? Nipe chenji yangu, mimi nashuka! Mimi nikikosa mia nitapanda basi lako? Sitaki utani, naomba chenji yangu.”

 

Siku hii nilipanda basi dogo la abiria nikitoka mjini kuelekea nje ya mji. Kwa bahati nzuri, nilipata kiti. Tulipoanza safari, kwa bahati mbaya kondakta alipokea pesa kutoka kwa abiria lakini akakosa chenji. Hali hiyo ilianza kuleta malalamiko mengi , maneno haya yalipamba safari yetu.

 

Kondakta huyu alikuwa mtu mpole sana na hakujibu malalamiko hayo. Alipofika kwangu, nikampa shilingi 2,000 zilizokuwa nazo sarafu za mia moja kadhaa na mia mbili kadhaa.

 

Akasema:“Mzee, asante sana.”

Baada ya kuhesabu pesa, akasema bado nina deni la shilingi 300. Nikampa sarafu ya shilingi 500, naye akanirudishia shilingi 200. Pesa hizo zilimsaidia sana. Alirudi mbele na kuendelea kutoa chenji kwa wale abiria waliokuwa wamekwama. Baadaye akaja tena upande wangu na kuniuliza:

 

“Mzee, una mia tano mbili?”

Nikaingiza mkono kwenye mfuko wa juu wa begi langu nikampa, naye akanipa noti ya shilingi 1,000. Tuliendelea na safari kwa dakika 10 au 15 hivi, tukafika katika kituo kimoja. Hapo wakapanda wanafunzi pamoja na akina mama wawili waliokuwa nadhifu. Nywele zao zilikuwa zimepambwa vizuri na walikuwa wamevaa magauni mazuri. Walipoingia ndani ya gari, walijifuta vumbi kwa leso na kukaa. Baadaye akaingia kijana mmoja wa Jeshi la Polisi Tanzania akiwa amevaa sare zake, pamoja na koti la polisi lililofanana na sare hiyo.

Watu wote hawa walipata viti. Walimu wawili wa kike wakakaa upande wa kushoto wa Mwanakwetu. Wanafunzi wakakaa kwenye kiti cha nyuma cha watu sita, huku yule polisi akiketi mbele ya Mwanakwetu, baada ya kuvuka kiti kimoja.

 

Kondakta akaanza kukusanya nauli. Alipofika kwenye kiti alichokaa polisi, dada mmoja akampa pesa yake. Nyuma ya kiti hicho cha polisi kulikuwa na kiti cha dada mmoja aliyekuwa na ndevu. Kiti kilichofuata alikuwa amekaa Mwanakwetu, huku nyuma kabisa wakiwa wamekaa wanafunzi wa sekondari, ambao kwa makadirio walikuwa wa kidato cha pili au cha tatu. Wale wanafunzi wakawa wanamtazama kondakta anavyokusanya nauli, huku wakiongea kwa sauti ya chini kwa lugha ya Kigogo:

 

“Mbona kondakta hajachukua nauli kwa polisi?”

 

Wakaendelea kunong’ona kwa Kigogo:

 

“Hawa wote ni wakonongo, hawafahamu Kigogo. Polisi wetu ni bahili sana.”

Vijana hawa walizungumza kwa uhuru kabisa wakicheka. Mmoja wao akaongeza:

“Kwa yule dada aliye jirani na polisi, kondakta amechukua. Kwa yule dada mwenye ndevu amechukua. Kwa huyu mkubwa—Mwanakwetu—amechukua. Kwanini hajaomba nauli kwa polisi? Akija nitamuuliza.”

 

Wakati huo kondakta akaja upande tuliokuwa tumekaa mimi na wanafunzi. Akachukua nauli ya walimu jirani zangu. Kwa kuwa tayari alikuwa ameshachukua pesa, akaomba tena chenji ya shilingi 500. Nikaingiza mkono kwenye mfuko wa begi langu na kukuta sarafu nne. Nikazihesabu na kumwambia:

“Nina shilingi 450.”

 

Akasema: “Nipe hizo hizo.”

Nikamkabidhi, naye akanipa shilingi 500.Kondakta akacheka na kusema:

“Mzee, kuanzia leo nitakuwa nakuita Mzee wa Chenji. Umefuga bao la mkono mithili ya Diego Maradona. Saluti sana, mzee!”

 

Msomaji wangu, tambua hili: Kwa kawaida, katika begi langu huwa ninahifadhi sarafu zote ninazozipata. Hii hunisaidia sana ninapohitaji nauli, kwa sababu mara nyingi huwa ninakuwa na sarafu nyingi. Kondakta akafika kwenye kiti cha watu sita kilichojaa wanafunzi. Akapokea nauli, ndipo yule mwanafunzi mtundu akauliza kwa Kigogo:

 

“Mbona haujachukua nauli kwa polisi?”

Kondakta akacheka, kisha akajibu kwa Kigogo:

“Nikirudi mbele nitachukua.”

 

Kondakta akarudi kimya kimya, akakaa mlangoni na kuendelea na safari. Baada ya muda, mmoja wa wale wanawake wawili yaani wale walimu akasema:

“Kondakta, kondakta! Mimi nashuka Sheli ya Total.”

Kweli kondakta akasimamisha basi na mama huyo akashuka.

 

Mwanakwetu akawa anacheka moyoni namna kituo cha mafuta cha Total kilivyoitwa “Sheli ya Total”. Moyoni nikasema:

 

“Huyu mwalimu wetu anashindwa kutofautisha haya makampuni mawili ya mafuta. Maana Shell ni kampuni ya mafuta, kama ilivyo Total.”

Tukaendelea mbele kidogo, yule polisi pamoja na dada mmoja wakashuka. Safari ikaendelea. Mwanakwetu akawa anatafakari sababu iliyofanya askari wa polisi na hata wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kufikia hali ya kutolipishwa nauli katika mabasi.

Hoja kubwa ilikuwa hii:

 

Kumbuka kwamba, katika miaka ya baada ya uhuru wa Tanganyika, serikali ilifanya mambo mbalimbali makubwa ya kujenga taifa, yakiwamo sera za vijiji vya ujamaa. Katika kipindi hicho pia kulitokea mgogoro kati ya Uganda na Tanzania, ambao hatimaye ulisababisha Vita vya Kagera. Vita hivyo vilifikia hatua ya kuondolewa madarakani kwa Nduli Idi Amin Dada.

 

Baada ya vita kukamilika, wanajeshi na askari wote walioshiriki katika vita hivyo walitazamwa na Watanzania kama mashujaa. Wale waliopoteza maisha waliaminika kuwa wamekufa kishujaa, na wale waliorudi walipokelewa kama mashujaa. Waliokuwepo Dar es Salaam wanasema hoja haikuwa tu kutolipa nauli. Hata watu wazima waliwapa askari nafasi zao kwenye mabasi ya usafiri wa umma, kama vile UDA na KAMATA kwa kuwapisha kiti bila kujali rika la askari.

 

Mwanakwetu bado alikuwa ndani ya basi. Likaendelea na safari kidogo, kisha wale wanafunzi wakashuka huku wakimtania kondakta. Basi likaendelea hadi kituo kingine, ambacho Mwanakwetu naye alishuka. Kondakta akamtania:

 

“Ah, Mzee wa Sarafu, umefika? Asante sana, mzee.”

 

Mwanakwetu aliposhuka, vijana wa bodaboda wakataka kumbeba hadi kwake. Akawaambia:

“Hapana, mimi ninatembea kwa miguu.”

 

Akaendelea na safari yake kwa miguu huku njiani akijisemea moyoni:

 

“Wale wanafunzi wa sekondari walikuwa na kiu ya kuona polisi analipa nauli. Uhodari wa askari wetu katika Vita vya Kagera upo kwenye historia, na wapo waliouona na kuushuhudia. Lakini kwa sasa, historia hiyo inashindwa kumtetea yule askari katika akili za hawa wanafunzi wa sekondari.”

Akili ya Mwanakwetu inatfakari;

“Kwa sasa, hata kama yule polisi angekosa kiti, sidhani kama kungekuwa na mtu wa kumpisha. Angesimama hadi afike pale alipokusudia kushuka.”

Mwanakwetu alifika kwake, akakaa na kutafakari yaliyotokea. Hatimaye akaamua kuyaandika makala haya kama yalivyotokea.

 

Hitimsho,

Kwa hiyo, kushuka kwa imani ya wananchi kwa baadhi ya askari wa vyombo vya ulinzi na usalama hakutokani na historia ya taasisi zao, bali kunaweza kuchangiwa na matendo ya kila siku yanayoonekana kukinzana na misingi ya nidhamu, uadilifu na usawa. Askari anapokuwa katika sare, habebi heshima yake binafsi pekee, bali hubeba taswira ya chombo anachokiwakilisha. Ndiyo maana jambo dogo mathalani polisi kijana anaingia katika gari hatoi shikamoo kwa wazee, au anakutana na wazee anawapita tu, hiyo siyo haki. Kuvaa sare za polisi hakumfanyi kijana wa miaka 20-30 awe mtu mzima.

“Vijana wa polisi wafahamu hili mathalani wewe kwenu ni Morogoro unafanya kazi Arusha na yupo polisi mwingine kwao Arusha anafanya Morogoro, chochote unachofanya ugenini ni sawa sawa umekifanya kwenu maana Kanuni ya tatu ya mosheni inasema every action there is equal to the opposite reaction.Ukifanya uonevu, ukamdhalilisha mtu ugenini na mwingine atamdhalilisha nduguyo kwenu, kila mmoja aliye mbele yako tambua ni ndugu yako wa damu.Katika jamii hii yenye madhaifu tele ndipo tunapozaliwa.”

 

Matukio haya madogo madogo yanaoanishwa na matumizi mabaya ya silaha yaliyopita ambapo si vizuri kuyarudia yanatafsiriwa na wananchi, hasa vijana, kama ishara ya kupungua kwa uadilifu na uwajibikaji na uonevu kwao. Heshima ambayo vyombo hivi viliijengwa kwa miaka mingi inapaswa kulindwa katika kila jambo, kubwa na dogo. Suluhisho si kuwalazimisha wananchi kuwaheshimu askari kwa sababu ya sare au cheo, bali askari wenyewe waijenge heshima hiyo kwa matendo yao. Kila askari anapaswa kuwa mfano wa nidhamu, uadilifu, unyenyekevu, uzalendo na kuheshimu sheria na taratibu anazotakiwa kuzilinda. Wananchi wanahitaji kuona askari anayeheshimu haki, anayewajibika na anayejiona kuwa mtumishi wa taifa, si mtumishi kwa wakubwa na viongozi tu kwa kuwa anawapigia saluti maana wanaolipa mishahara yote, posho zote ni wananchi hawa hawa wadogo wadogo.

Imani hujengwa kwa matendo; na heshima ya sare huanzia katika tabia ya anayeivaa.

 

Mwanakwetu, upo? Kumbuka.

“MZEE WA SARAFU NA SWALI LA IMANI KWA ASKARI WETU”

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

NB Makala haya ni maalumu kwa mdogo wnagu Afande Juma Francis Fidelis Makwega

 








0/Post a Comment/Comments