.gif)
Adeladius Makwega – MBAGALA
Hii ni Agosti Mosi, 2026, siku ya kwanza ya mwezi mpya wa nane nchini Tanzania, hapa nilipo ndugu yenu Mwanakwetu.
Siku hii kulikuwa na ukimya kidogo. Hata nilipojaribu kuwasha soketi za umeme hazikutoa majibu. Nikajua labda hapa kwangu kuna tatizo la umeme. Nilipoenda kwa jirani kumuuliza, nyumba yake ilikuwa kimya; hodi yangu haikuitikiwa. Nilirudi kwangu na kuamua kuchagua nguo zangu kadhaa zilizohitaji marekebisho kwa fundi.
Nilibaini kuwa mashati yangu matatu yalihitaji kukatwa mikono ili yawe ya mikono mifupi, maana yalikuwa na mikono mirefu huku yakiwa yameniruka.
Mengine vifungo vilikuwa vimepotea.
Pia, suruali moja ilikuwa imetatuka na ilihitaji kushonwa, huku suruali ya pili ikiwa na baka ambalo nilihitaji ushauri wa fundi.
Nilitoka kwangu hadi kwa fundi wa kushona nguo. Hapa nilikaribishwa na mafundi watatu: mama mtu mzima, kijana, na binti mmoja mrefu mweusi. Ofisi yao ilikuwa na mashine za kushona karibu kumi, ikiwemo moja ya kudalizi, huku kazi zikiendelea.
Kati ya mafundi hawa watatu, nikamchagua kijana wa kiume. Alinipokea vizuri, nikampa nguo zangu, na akasema kazi zote zitafanyika vizuri, isipokuwa suruali yenye baka—hakuwa na suluhisho lake.
“Hapa ungekuwa kijana ningekuwekea kitambaa kingine juu, lakini wewe ni mzee watashangaa—huyu mzee vipi? Suruali nyeusi na kipandiko chekundu?”
Fundi kijana akataja gharama kuwa shilingi 8,000 za Kitanzania (sawa na dola 3.20 za Kimarekani). Nikamuomba apunguze hadi shilingi 5,000, lakini akakataa. Nikapanda dau na kusema, “Basi nakupa shilingi 6,000.” Fundi kijana akasalimu amri na kukubali. Nikatoa noti ya shilingi 10,000; akapokea. Kisha nikamuomba nikae kwenye kochi, akaniruhusu. Nikaketi, naye akamalizia kushona gauni moja kabla ya kuanza kukarabati nguo zangu.
Baadaye, yule mama fundi mtu mzima akasema:
“Kweli, Samweli, unamuachia mama Hillary ashone gauni la huyu mteja mwenye
mdomo?”
Samweli akajibu:
“Nimemuelekeza vizuri, mama Hillary. Hata hapa nilipo, namfuatilia hatua kwa
hatua.”
Kando ya miguu ya Mwanakwetu, kijana mdogo alikuwa anamsalimu kwa “Shikamoo” nyingi. Fundi yule binti akasema mtoto anakusalimu.
Ndipo nikashtuka—kumbe naamkiwa na huyu malaika! Nikaitikia salamu hiyo. Hapo ndipo nikabaini kuwa yule mtoto mdogo ndiye Hillary; yule binti fundi ndiye mama Hillary; yule fundi kijana ni baba Hillary; na yule mama fundi mtu mzima ni mama wa Samweli.
Hillary alikuwa anafanya vurugu: mara anataka kuula mkasi, mara anamsumbua mama yake, mara anashika gurudumu la mashine ya kushona, mara anasema,
“Mama nataka kulala, nipeleke nikalale.”
Kazi ziliendelea huku zikisindikizwa na milio ya mashine za kushona, kelele za Hillary, na sauti za magari kwa mbali.
Ghafla akafika mama mmoja mtu mzima, akanisalimu, kisha akamfuata mama fundi mtu mzima na kusema:
“Hili gauni mlilonishonea naona kama ni refu sana; naomba mlipunguze. Hata hapa
kiunoni ni kubwa.”
Mama fundi mtu mzima akasema sawa.
Mteja huyo akaongeza:
“Nilidhani nyinyi ni Wasabato—Jumamosi hamfungui. Kumbe mnafungua. Nyinyi
mnasali wapi?”
Mama fundi mtu mzima akajibu kuwa wao ni Wapentekoste.
Akaongeza:
“Gauni lako nimelipokea, lakini leo hakuna umeme. Nikilipunguza lazima nitapiga
overlock, na hiyo inahitaji umeme. Hadi utakaporudi, ni vizuri ujaribu tuone
hayo mapungufu.”
Mteja akasema:
“Yaani kujaribu mpaka nivue nguo zote hizi?”
Mama fundi akajibu:
“Ndiyo maana kipo chumba cha kubadilishia nguo—kazi yake ndiyo hiyo.”
Mama huyo mteja alikataa kupima na kusema walishone tu hivyo hivyo, kisha akaondoka
.
Alipokuwa anaaga, alisema atarudi Jumamosi ijayo, yaani Agosti 8, 2026, akitumaini umeme utakuwa umerudi, kwani hali ya umeme haieleweki.
Milio ya mashine za kushona iliendelea kusikika, pamoja na sauti za magari na bodaboda kwa mbali. Hillary aliendelea na vurugu:
“Mama, nipeleke nikalale… mama, twende ukanibebe… siwezi kulala, lazima
unibembeleze.”
Mama Hillary akaacha kushona gauni lile, akamchukua Hillary na kumpeleka chumba cha kubadilishia nguo ili amlaze. Mama fundi mtu mzima akasema:
“Si mlimdekeza wenyewe, sasa hangaikeni naye.”
Mama Hillary akaenda kumlaza Hillary, naye akalala. Mama Hillary akarudi kazini na kuendelea kushona.
Mama fundi mtu mzima akasema:
“Samweli, angalia mama Hillary anavyoshona hapo makwapani—hapo lazima pashonwe vizuri, pavutike.”
Samweli akamwambia mama Hillary kwa upole:
“Hapo makwapani unatakiwa kushona kama nilivyokuambia.”
Hapa Mwanakwetu nilibaini kuwa mama Hillary ni mke wa Samweli, yule mama fundi mtu mzima ni mama mkwe wake, na mama Hillary bado ni mwanafunzi wa kushona—ndiyo maana anafuatiliwa kwa karibu, na wala hakasiriki.
Ghafla akatokea mama mjamzito. Akapimwa gauni lake na Samweli vizuri—kuanzia kifuani, tumboni hadi urefu. Baadaye, kazi za Mwanakwetu zikakamilika. Nikapewa chenji ya shilingi 4,000 na kuondoka.
Nilipofika nyumbani, umeme haukuwepo. Ulirudi majira ya jioni. Ndipo nikaamua kuandaa makala haya kama yalivyo—ikiwa ni muhtasari wa siku ya Agosti Mosi, 2026.
Je, makala haya yana mafunzo gani?
Katika ukimya wa asubuhi na kelele za mchana, maisha yanatufundisha kwa njia zake zisizo na kelele nyingi. Makala haya yanabeba mafunzo yafuatayo:
Kwanza, uvumilivu ni nguzo ya maisha. Changamoto kama ukosefu wa umeme hazizuii maisha kusonga mbele—zinatufundisha kusubiri na kuendelea.
Pili, kazi ni utu. Juhudi za mafundi zinaonyesha kuwa heshima ya mtu hujengwa katika kile anachokifanya kwa mikono yake na moyo wake.
Tatu, familia ni shule ya kwanza. Ndani ya karakana ndogo, tunaona malezi, mafunzo, na mahusiano yakijengwa kwa pamoja—kazi na upendo vikitembea sambamba
.
Nne, kujifunza hakukomi. Mama Hillary anatukumbusha kuwa kila mtaalamu alianza kama mwanafunzi, na mafanikio huja kwa uvumilivu na unyenyekevu.
Tano, maisha ya kawaida yana uzuri wake. Katika matukio madogo yasiyo na umaarufu, ndipo hadithi halisi za maisha hujificha.
Mwisho Kauli “mlimdekeza wenyewe, sasa hangaikeni naye” ni sauti ya hekima iliyojificha katika mzaha wa maisha ya kila siku, ikibeba ukweli kwamba kile tunachokilea kwa mikono yetu hukua na kuwa kivuli kinachotufuata. Ni onyo lenye upole lakini lenye uzito, likikumbusha kuwa kuyakalia kimua mabaya yasiyo na mipaka yanaweza kuzaa madhara makubwa si familia tu bali kwa jamii nzima, na matendo ya jana huzaa matokeo ya leo. Mimi na wewe tuangalie tusije kuwa tunavuna tulichopanda wenyewe kwa mzaha.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka.
“Mmemdekeza Wenyewe Sasa Angaikeni Naye.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257





.gif)





Post a Comment