Adeladius Makwega-Mlali
Dodoma, Tanzania
Kwa mujibu wa tafakari iliyotayarishwa na Padri Bonaventura Maro, C.PP.S., na kuchapishwa na Redio Vatican pamoja na mitandao yake ya kijamii, kwa muhtasari anasema yafuatayo:
“Dominika ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa inatukumbusha kuwa Mungu ni mwenye upendo, huruma na ukarimu usio na mipaka. Katika changamoto za maisha kama njaa, kiu na mahangaiko mbalimbali, Mungu hatuachi peke yetu, bali anatutunza na kutuliza kiu ya mioyo yetu kupitia Neno lake na Ekaristi Takatifu. Yesu anatufundisha kwamba hakuna kitu cha kidunia kinachoweza kutosheleza roho ya mwanadamu isipokuwa ushirika na Mungu.
Injili ya kulisha watu zaidi ya elfu tano inaonesha huruma ya Yesu kwa watu waliokuwa na mahitaji ya kiroho na kimwili. Kupitia mikate mitano na samaki wawili, Yesu anatufundisha kuwa kile kidogo tulicho nacho tukimkabidhi Mungu kwa imani na shukrani, anaweza kukibariki na kukizidisha ili kiwafaidishe wengi. Hivyo, Wakristo wanaitwa kuwa na moyo wa ukarimu, kushirikiana na kuwahudumia wahitaji.
Ekaristi Takatifu ni ishara kuu ya upendo na ukarimu wa Mungu. Ndani yake Kristo anatupa Chakula cha Uzima na kutuimarisha katika safari ya imani. Baada ya kupokea Ekaristi, waamini wanaitwa kuwa mashuhuda wa upendo wa Kristo kwa kuwahudumia wengine, huku wakiamini kwamba hakuna jambo lolote linaloweza kututenga na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu.”
Haya ni ya Padri Bonaventura Maro, kama yalivyonukuliwa na Redio Vatican, nami nimeyatoa kwa muhtasari wake.
Je, Makadinali wanasema nini kuhusu Dominika hii ya tarehe 2 Agosti 2026?
“Katika Injili tunasikia kuhusu muujiza wa Bwana wa kuwalisha watu zaidi ya 5,000. Muujiza huu wa kuzidisha mikate mitano na samaki wawili umeandikwa katika Injili zote nne.
Katika simulizi ya Mtakatifu Mathayo, sura ya 14, baada ya mafundisho ya Yesu kuhusu Ufalme wa Mbinguni tuliyoyasikia katika Jumapili zilizopita, tunakumbuka pia kukataliwa kwake huko Nazareti na kuuawa kwa Yohane Mbatizaji. Kukumbuka muktadha huu kunatupa uelewa wa kina zaidi wa muujiza huu.
Katika wakati huo, mifano ya Yesu ilitimia kwa uhalisia. Katika Ufalme wa Mungu, kile kinachoonekana kuwa kidogo kinaweza kuleta wingi mkubwa kinaposhirikishwa. Tunapolipokea Neno la Mungu, tunashibishwa.
Ndugu zangu, bado tutaendelea kumtafuta na kumfuata Yesu katika ulimwengu unaotupatia njia nyingi zinazodai kutuletea kuridhika na utimilifu wa maisha.
Bwana si mgumu kumpata. Katika Misa Takatifu, anawalisha wote wanaoketi mezani pake kwa Mwili na Damu yake, akitudumisha na kutulisha kwa baraka na neema ya Mungu. Upendo unakuwa mwingi na kufurika.”
Haya ni maelezo ya utangulizi wa tafakari ya Dominika hii yaliyotayarishwa na Kadinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide ya Uinjilishaji ya Kanisa Katoliki, inayoratibu shughuli za uinjilishaji duniani.
Katika Dominika hii, nilishiriki Misa Takatifu katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Nilihudhuria Misa ya kwanza iliyoanza saa 12:00 asubuhi.
Wakati wa matangazo, msomaji alisahau kusoma matangazo ya ndoa. Baadaye alirudi na kuyasoma matangazo mawili ya ndoa kwa mara ya kwanza:
Tangazo la kwanza lilimhusu Stephen Marko Edward wa Tabora, mwana wa Marko Edward na Rose Maganga, anayetarajia kufunga ndoa na Zakia Rajabu Athumani wa Tabora, binti wa Rajabu Athumani Kushanga na Fatuma Hassan Peter. Ndoa hiyo inatarajiwa kufungwa tarehe 5 Septemba 2026. Waamini wenye kizuizi chochote kuhusu ndoa hiyo walitakiwa kutoa taarifa katika parokia husika.
Tangazo la pili lilimhusu Nicodemus Steven, mwana wa Severine Protas Makunzo wa Ihumwa na Rosadina Linus Tershoni, anayetarajia kufunga ndoa na Regina Shija John, binti wa Paulo Mwagama Habius wa Kishilu, Mwanza, na Marietha Paulo Kisumu. Ndoa hiyo inatarajiwa kufungwa tarehe 10 Oktoba 2026. Mwenye kizuizi chochote alitakiwa kutoa taarifa kwa Paroko wake.
Katika Kanisa Katoliki, ndoa ni mojawapo ya Sakramenti saba. Matangazo ya ndoa hutolewa mara tatu kabla ya ndoa kufungwa ili kutoa nafasi kwa yeyote mwenye kizuizi halali kukitaarifu kwa Kanisa.
Nilipokuwa narudi nyumbani, nilikutana na tukio lililonifanya nitafakari.
Awali nilimwona ndege mmoja mwenye mkia mrefu, lakini sikuweza kumtambua. Niliposonga mbele, nikakutana na ndege wengine watatu wa aina hiyo. Nikajiuliza ni ndege wa aina gani. Ghafla nikasikia milio yao, nikawaona wengine watano. Nilipozidi kuwakaribia, walikimbia, kisha ndege wote tisa wakaruka na kuingia ndani ya ukuta wa Ikulu ya Chamwino.
Ndani ya eneo la Ikulu kulikuwa na mazingira ya kijani kibichi, ilhali nje ya ukuta kulikuwa na ukame na nyasi zilizokauka sana. Baadaye nikagundua kuwa wale walikuwa tausi waliotoka ndani ya Ikulu kwenda kula mbegu za mti uliokuwa umejaa mbegu nyingi nje ya ukuta, karibu na eneo la vijana wanaouza samani.
Nilijiuliza: Kwa nini tausi wale walitoka katika mazingira mazuri ya ndani ya Ikulu na kwenda kutafuta chakula nje ya ukuta, ambako kulikuwa na ukame zaidi? Sikupata jibu.
Nilipofika nyumbani ndipo nikaandika makala haya.
Je, tukio la tausi hao tisa kutoka nje ya ukuta kutafuta chakula lina funzo lolote kwangu mimi Mkristo ninayeishi katika hii dunia?
Mwanakwetu nilikuwa najiuliza hivi ninaweza kuitafakari kwa namna ya kiroho. Nikajisemea mwenyewe kuwa huu si unabii bali matukio ya kawaida ya maisha ambayo kila mmoja anakutana nayo lakini yanaweza kutusaidia kutafakari ukuu wa Mungu.
Tausi waliotoka ndani ya ukuta wa Ikulu kwenda kutafuta mbegu nje, kisha wakarudi ndani, wanatukumbusha kwamba kila kiumbe hutegemea Mungu kwa riziki yake. Ingawa ndani ya Ikulu kulikuwa na mazingira mazuri zaidi, walitoka kutafuta chakula mahali pengine. Hii inaweza kufanana na Injili ya Dominika hii, ambapo Yesu aliwalisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, akionyesha kwamba Mungu ndiye chanzo cha riziki na kwamba hakuna kiumbe anayesahaulika mbele zake.
Pia nikadhani na hili:
Mbegu zilizokuwa nje ya ukuta zinaweza kuwa ishara ya neema za Mungu zinazopatikana hata mahali ambapo kwa macho ya kibinadamu panaonekana kuwa na ukame. Mara nyingi tunaamini baraka zinapatikana mahali penye wingi na neema, lakini Mungu anaweza kutulisha hata katika mazingira yanayoonekana kuwa magumu. Hivyo, si mazingira yanayotoa uzima, bali Mungu anayevibariki vilivyomo ndani yake.
Pia unaweza kuhusisha na somo la kwanza kutoka Isaya 55:
Kama Nabii Isaya anavyowaalika wenye njaa na kiu wamjie Mungu wapate chakula cha bure, ndivyo tausi walivyotoka kutafuta chakula walichokihitaji. Mwanadamu pia hawezi kushibishwa na mali, mamlaka au anasa pekee; anahitaji kumrudia Mungu, ambaye humpa chakula cha uzima kupitia Neno lake na Ekaristi Takatifu.
Hitimisho linaweza kuwa:
Tukio la tausi halikuwa muujiza wala unabii, bali linaweza kuwa mwaliko wa kutafakari kwamba Mungu huwajali viumbe wake wote. Ikiwa anawajalia ndege chakula, sisi aliotuumba kwa sura na mfano wake hatupaswi kuishi kwa hofu, bali kwa imani, tukiamini kwamba atatupatia tunachohitaji kwa wakati wake. Kama anavyosema Yesu: "Waangalieni ndege wa angani... Baba yenu wa mbinguni huwalisha" (Mathayo 6:26).
Mwanakwetu upo?
Kumbuka:
“Mikate Mitano, Samaki Wawili na Vipi Kwa Tausi Tisa?”
Nakutakia siku njema.
Adeladius Makwega-Mlali
Dodoma, Tanzania
Barua pepe:
Simu: 0717 649 257
.gif)

.gif)
.gif)





Post a Comment