Adeladius Makwega – MBAGALA
“Kaka, naona unaandika makala tu za Kumbukumbu na Nyaraka. Sisi wengine umetutenga? Inakuwaje? Au sisi wengine ni watoto wa kambo?”
Haya yalikuwa ni maneno ya mdau mmoja wa Mwanakwetu mapema ya Agosti 14, 2026, baada ya Mwanakwetu kupigiwa simu na rafiki yake huyu anayefanya kazi katika Mahakama za Tanzania, akiwa sehemu ya jamii ya mahakimu na majaji.
Akiyasema maneno hayo kwa utani, Mwanakwetu akamjibu:
“Hapana, siwezi kuwatenga nyinyi. Nanyi ni wadau wangu wa kipindi kirefu. Karibuni nimekuwa nikizungumzia zaidi Kumbukumbu na Nyaraka. Ila tatizo lenu ni kwamba kesi zenu zinatumia muda mrefu hadi mashahidi wanafariki. Mnafanya tushindwe kesi! Kesi hizo zote mnamuongezea mafili Mungu, huku kesi zenu za duniani zikiwa hazimaliziki.”
Jamaa huyu akacheka sana, kisha akasema:
“Mswalie Mtume.”
Mwanakwetu akajibu:
“Swalla alaa Nabii.”
Kisha Mwanakwetu akaendelea:
“Hata hivyo, nafasi ya kubadilisha kada ipo wazi. Unaweza kutoka Mahakama za Tanzania ukaja Kumbukumbu na Nyaraka, ili uje ufaidi uhondo wa Kumbukumbu na Nyaraka.”
Jamaa huyu akauliza kwa shauku:
“Kwani Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka ina majukumu gani?”
Mwanakwetu akamjibu:
“Kusanya na Kuhifadhi: Kupokea na kutunza nyaraka za kihistoria na za kudumu kutoka kwa taasisi za Serikali ambazo hazitumiki tena kwa shughuli za kila siku za kiutawala.
Ukarabati na Dijitali: Kukarabati nyaraka zilizochakaa na kuziweka katika mifumo ya kidijitali ili zidumu kwa muda mrefu.
Urithi wa Waasisi: Kusimamia na kuhifadhi kumbukumbu na vitu vya kihistoria vya viongozi na waasisi wa Taifa.”
Jamaa huyu akawa anamsikiliza Mwanakwetu kwa umakini mkubwa.
Lakini Mwanakwetu, kana kwamba alikuwa bado hajamaliza safari yake ya maelezo, akampigia msumari wa mwisho:
“Hata zile nyaraka zenu za mienendo ya kesi zenu za zamani, hapa zipo zimejaa tele. Na tena, zile nyaraka zilizoandikwa kwa maandishi ya mkono ya mahakimu wa enzi hizo—zimejaa tele!”
Jamaa akastaajabu mno akamsikiliza kwa makini, kisha akauliza:
“Sasa nyinyi ni kama maktaba?”
Mwanakwetu akamjibu:
“Sisi ni zaidi ya maktaba.”
Kabla mazungumzo hayajaendelea, ghafla sauti ikasikika:
“Mheshimiwa, muda wa kuanza shauri namba... umefika.”
Mtoto huyu wa kambo wa makala za Mwanakwetu akasema:
“Kwa heri, kaka. Ngoja niingie mahakamani.”
Wakaagana.
Baadaye, Mwanakwetu akaamua kuendelea kuchapa kazi pamoja na wadau wenzake wa Kumbukumbu na Nyaraka. Lakini mazungumzo yale yakamwachia jambo moja muhimu moyoni—kwamba nyuma ya mafaili, karatasi na nyaraka zilizotulia kimya, kuna historia kubwa ya Taifa inayohitaji kutunzwa, kulindwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Ndipo akaamua kuyaandika makala haya kama yalivyo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hiyo, Kumbukumbu na Nyaraka si karatasi zilizohifadhiwa kwenye mafaili pekee, bali ni hazina ya historia, utambulisho na safari ya Taifa letu. Kila nyaraka ina simulizi yake, kila jalada lina historia yake, na kila kumbukumbu inaweza kuwa daraja linalotuunganisha na yaliyopita ili kuyaelewa yaliyopo na kujenga yaliyo bora zaidi kwa vizazi vijavyo. Hivyo basi, tuzitunze, tuzithamini na kuziendeleza Kumbukumbu na Nyaraka, kwa sababu Taifa lisilothamini kumbukumbu zake linahatarisha kupoteza sehemu ya historia yake.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka.
“Ati Mahakama ya Tanzania Mtoto wa Kambo?”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)





.gif)
Post a Comment