MAHAKAMA YA TANZANIA ITUMIE WATAALAMU IPASAVYO

 

 





Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Mawakili wanapaswa kuheshimu taratibu za Mahakama. Hawapaswi kutumia vyombo vya habari kuingilia au kuathiri mwenendo wa shauri lililo mbele ya Mahakama. Mawasiliano kuhusu shauri yanapaswa kufanywa kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni za maadili ya mawakili na maelekezo ya Mahakama. Mahakama inakumbusha kwamba mwenendo wa mashauri unapaswa kuendelea kwa namna inayohakikisha haki na uadilifu wa mchakato wa Mahakama.”

 

Hayo ni baadhi ya maudhui yaliyomo katika tangazo la Mahakama ya Tanzania lililotolewa tarehe 12 Agosti 2026, likihusu mwenendo wa mawakili katika mawasiliano yao na vyombo vya habari.

Tangazo hilo pia linarejea Tangazo la Serikali Na. 118/2018, pamoja na Ibara ya 30(1)(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mwanakwetu alipolisoma tangazo hili, hakukimbilia kulihukumu. Alikaa chini na kujiuliza maswali kadhaa—maswali ambayo anaamini yanaweza kusaidia kujenga Mahakama yetu na kuboresha namna taasisi hii muhimu inavyowasiliana na wananchi.

 

Jamani ee! Kama nia ya mtoa tangazo ilikuwa ni kuwaelekeza mawakili kuhusu mwenendo wao mbele ya vyombo vya habari, swali la kwanza linajitokeza lenyewe:

Kwa nini Mahakama ilichagua kutoa tangazo kwa umma badala ya kuwasiliana moja kwa moja na kundi lililolengwa—yaani mawakili?

 

Hili si swali la kubeza. Ni swali la namna bora ya kutumia mifumo ya mawasiliano iliyopo ndani ya Mahakama. Kwa sababu, kwa Mtanzania wa kawaida, marejeo kama Tangazo la Serikali Na. 118/2018 na Ibara ya 30(1)(2)(d) ya Katiba si mambo anayoyafahamu kila siku. Mwananchi wa kawaida akiona tangazo kama hili anaweza kujiuliza:

Hili Serikali Gazette Na. 118/2018 inasema nini? Ibara hii ya Katiba inahusu nini? Na inahusianaje na jambo hili? Ili kupata majibu, atalazimika kwenda kuzitafuta nyaraka hizo, kuzisoma na kujaribu kuzielewa.

 

Hapo ndipo Mwanakwetu anaona kuna jambo la kujiuliza kuhusu namna taarifa inavyowasilishwa kwa walengwa na kwa umma.

 

Mahakama ya Tanzania tayari ina mifumo mbalimbali ya mawasiliano na wadau wake, ikiwemo mfumo wa e-Wakili. Ikiwa ujumbe unawalenga moja kwa moja mawakili, kwa nini wasingepewa maelekezo hayo kupitia njia rasmi zinazowafikia moja kwa moja?

 

Kwa mfano, kama Mahakama inataka kuwaambia:

 

“Mawakili wote na wadau wengine wa Mahakama...” inaweza kutumia mifumo yake rasmi kuwafikishia ujumbe huo walengwa wake.

 

Halafu, kama kuna sababu ya kuwajulisha wananchi, taarifa kwa umma inaweza kutolewa kwa namna tofauti, kwa lugha inayomwelekeza mwananchi kuhusu jambo hilo na umuhimu wake.

 

Hapo ndipo tunapofikia swali lingine. Je Hili ni Tangazo kwa mawakili au kwa umma? Kama Mahakama iliona suala hili lina maslahi mapana kwa umma, basi kulifanya liwe wazi kwa wananchi kunaweza kuwa na mantiki. Lakini kama walengwa wakuu ni mawakili, Mwanakwetu anauliza:

Kwa nini taarifa hiyo isiende kwanza moja kwa moja kwa mawakili?

Na zaidi ya hapo:Je, kuchapisha taarifa kama hii kwa umma kunaweza kutafsiriwa tofauti na wananchi ambao hawajahusika kabisa na mashauri ya Mahakama? Tusisahau kwamba Mahakama si kwa ajili ya mawakili pekee. Ni mahali ambapo wananchi huenda kusikiliza kesi za ndugu zao, kutoa ushahidi, kufuatilia haki zao au kutafuta huduma za kisheria. Kwa hiyo, kila neno linalotoka katika taasisi hii linaweza kutengeneza mtazamo fulani kwa jamii.

Kwa nini msajili asitumie njia rasmi za mawasiliano na mawakili? Hapa Mwanakwetu anauliza swali lingine la kiutawala: Kama walengwa ni mawakili, kwa nini ujumbe usipelekwe moja kwa moja kupitia njia rasmi za mawasiliano zilizopo kati ya Mahakama na mawakili?

Na kama kulikuwa na umuhimu wa taarifa kufika kwa umma, kwa nini Kitengo cha Mawasiliano cha Mahakama kisihusishwe katika kuiandaa kwa lugha ya taarifa rasmi kwa umma?

Hili si suala la kutafuta nani wa kulaumiwa. Ni suala la kutumia kila mtaalamu katika eneo lake la utaalamu.

Msajili ni msajili na AFISA HABARI NI AFISA HABARI

Mwanakwetu anaamini kwamba taasisi kubwa kama Mahakama haiwezi kuwa na tatizo la wataalamu. Ikiwa kuna maafisa waliobobea katika mawasiliano ya umma, uandishi wa taarifa, mahusiano ya umma na usimamizi wa taarifa za taasisi, ni busara taaluma hizo zitumike ipasavyo.

Msajili ana wajibu wake. Jaji ana wajibu wake. Hakimu ana wajibu wake.Mhasibu ana wajibu wake. Afisa Manunuzi ana wajibu wake . Na Afisa Mawasiliano ana wajibu wake.

Hii ndiyo maana ya kutumia rasilimali watu kwa ufanisi.

 

Mwanakwetu anauliza:

 

“Au ukiwa ndani ya kuta za Mahakama, Jaji na Hakimu ndiyo mhasibu, Afisa Manunuzi, Afisa Habari—yaani kila kitu?”

La hasha! Kila mtaalamu apewe nafasi ya kutumia taaluma yake.

Hili si jambo dogo kama tunataka mahakama Imara.

Mtu anaweza kusema:

 

“Mwanakwetu, kwa nini unaleta mjadala mkubwa kwenye tangazo moja tu?”

 

Mwanakwetu anasema: kwa sababu taasisi hujengwa na vitu vidogo vidogo vinavyofanyika kila siku.

Mahakama inaheshimiwa si kwa majengo yake pekee. Inaheshimiwa pia kwa namna inavyopokea kesi, namna inavyoendesha kesi, namna inavyowasiliana na wananchi, namna inavyowasiliana na wadau wake na namna inavyotumia wataalamu wake.

 

Leo Tanzania inapitia maboresho makubwa katika sekta ya Mahakama.Tunashuhudia ujenzi wa majengo, maboresho ya huduma na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Mahakama. Fedha hizo, kwa sehemu kubwa, zinatokana na rasilimali za Taifa na mikopo ambayo hatimaye Taifa linapaswa kuilipa.

 

Kwa hiyo, wananchi wana haki ya kuangalia si majengo pekee, bali pia utendaji wa taasisi ndani ya majengo hayo.

Tusimwelewe vibaya Mwanakwetu. Mwanakwetu hasemi Mahakama isitoe taarifa kwa umma.Kinyume chake. Mahakama inapaswa kuwa na mawasiliano bora zaidi na wananchi.

Lakini anachouliza ni:

Ni nani anapaswa kuandaa taarifa hiyo? Inapaswa kuwafikia nani? Kwa njia gani?Kwa lugha gani?Na kwa wakati gani?

Hayo ni maswali ya msingi katika taasisi yoyote inayohudumia umma.

 

Mwanakwetu anaomba jambo moja pia lieleweke.Waandishi wa habari wanapokwenda Mahakamani, hawaji kwa sababu wanapenda kutembea ndani ya majengo ya Mahakama.

Hawaji kwa sababu wanafurahia kukanyaga vizimba vya Mahakama. La hasha!

Wanakwenda kwa sababu kuna jambo la umma linalohitaji kufahamishwa.

 

Kuna wananchi wengi ambao hawawezi kufika Mahakamani. Kuna ndugu wanaosubiri kujua kinachoendelea.

Kuna wananchi wanaotaka kufahamu namna haki inavyotendeka.

 

Hivyo, mwandishi wa habari anapokwenda Mahakamani, mara nyingi anabeba jukumu la kupeleka taarifa kutoka Mahakamani kwenda kwa wananchi ambao hawakuweza kufika hapo.Wakili ataongea na vyombo vya habari kwa sababu jamii ina kiu, kama hoja ni kanuni zifutwe na mahakimu na majaji waongee na jamii maana jamii ndiyo mwenye mali kwanini wawekewe kizingiti? Kuwakea kizingiti jamii kunaweza kusababisha mahakama kupunguziwa bajeti na kuonekana kana kwamba mahakama haipo na jamii.

 

Ndiyo maana Mahakama na vyombo vya habari vinahitaji kujenga uhusiano wa kikazi, wa heshima , wa kuaminiana na kidugu kama mahusiano ni ya kidugu kwanini tuwekeane kizingiti cha taarifa?

 

Mwanakwetu anaamini kuwa Mahakama ya Tanzania inapaswa kuendelea kujenga udugu, ujirani na mapenzi mema na wananchi. Heshima ya Mahakama haijengwi kwa ukimya wa wananchi.

Inajengwa kwa wananchi kuelewa kinachofanyika, kuamini kwamba haki inatendeka na kuona kwamba taasisi yao inawaheshimu.

 

Kwa hiyo, kila taarifa inayotoka Mahakamani iwe nafasi ya kujenga uaminifu, si kuongeza hofu. Na kila mtaalamu ndani ya Mahakama apewe nafasi ya kutumia taaluma yake kwa manufaa ya taasisi.

 

Mwanakwetu anaamini kuwa kama Idara/Kitengo cha Mawasiliano cha Mahakama kitahusishwa kikamilifu katika taarifa zinazolenga umma, lugha ya taarifa inaweza kuwa rafiki zaidi kwa wananchi, bila kupunguza uzito wa mamlaka ya Mahakama, hawa maafisa habari ndani ya mahakama wamesoma na wanahabari hawa vyuoni hawa ni ndugu, ndugu na ndugu wanaongea vizuri.

 

Hili si shambulio kwa Mahakama.Wanahabari siyo wahalifu.Ni swali la kujenga. Ni swali kutoka kwa mwananchi anayetamani kuona Mahakama ya Tanzania ikiwa imara, yenye heshima, yenye uwazi na yenye uhusiano mzuri na wananchi na vyombo vya habari.

 

Mwanakwetu anaamini kuwa Mahakama imara hujengwa si kwa sheria na majengo pekee, bali pia kwa mawasiliano yenye weledi, uwazi na heshima kwa wananchi. Ikiwa walengwa ni mawakili, wafikiwe kwa njia inayowahusu moja kwa moja; na ikiwa umma unapaswa kufahamu, taarifa itolewe kwa lugha inayoeleweka na kwa ushirikishwaji wa wataalamu wa mawasiliano, vizingiti havina maana. Tuiheshimu Mahakama, lakini pia tuiulize kwa heshima na tuijenge pamoja, vinginevyo tunaibomoa.

 

Mwanakwetu upo? Kumbuka.

“Msajili ni Msajili, Afisa Habari ni Afisa Habari: Wataalamu Watumike Ipasavyo”

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

0/Post a Comment/Comments