Adeladius Makwega – MBAGALA
“Mzee, wale wanaokaa ndani ya chuo katika mabweni wanalipa laki tatu kwa mwaka, lakini mimi ninavyoona ni heri nibaki nje, maana bei ya chakula mle ndani ni ghali mno. Ninapokaa nje, chumba kimoja nipo na mwenzangu; ndani ya miezi mitatu nalipa shilingi 105,000. Changamoto ni bili ya umeme, lakini huku nje, mathalani, sina pesa ya mboga, nitapika ugali wangu katika jiko la gesi na nitanunua matembele ya 500. Nitakula ugali wangu kwa amani, siku itapita salama, sitokufa kwa njaa. Sasa, mle ndani ya chuo nitaweza kula mkahawani kila siku? Hilo, baba, siliwezi.”
Haya ni maneno ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini Tanzania akizungumzia changamoto wanazopata wakiwa Chuo Kikuu.
Mwanakwetu, akilini mwake, akiwa anapata picha ya hali hii, akajisemea moyoni:
“Wako watumishi wa umma nchini Tanzania hawali katika mikahawa kutokana na gharama za maisha kuwa kubwa; wanakula mlo mmoja tu. Sembuse kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu anayetegemea mkopo wa elimu ya juu au mzazi wake masikini?”
Mwanafunzi huyu pia aligusia hili la asilimia ya mikopo wanayopewa wanafunzi hao:
“Ada ni milioni moja na nusu, unapewa laki saba, laki nane; unaitoa wapi?”
Mwanakwetu aliagana na wanafunzi hao na kisha kukaa na kutafakari kwa kina hali hii.
Mwanakwetu anashauri yafuatayo:
Vyuo Vikuu vyote vya umma mishahara inalipwa na Serikali Kuu, lakini vyuo binafsi mishahara inalipwa kutokana na makusanyo ya ada na gharama zingine za uendeshaji wa elimu.
Mwanakwetu anashauri vyuo vya umma vitoe elimu, lakini visifanye makusanyo ya ada kwa wanafunzi wa Kitanzania waliochaguliwa na TCU kujiunga navyo. Hili liwe marufuku. Kisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu itoe mikopo kwa wanafunzi wote wenye sifa, itoe mkopo wa asilimia 100 kwa huduma nyingine, ikiwamo chakula, pa kukaa, vitabu, malazi na mafunzo ya vitendo.
“Haiwezekani pesa itoke serikalini kisha irudishwe serikalini.”
Kwa utafiti mdogo, vyuo vikuu vya umma vinakaguliwa na CAG. Jina la mwanafunzi, karo aliyolipa na kama kuna deni, mkaguzi wa ndani ataibua hoja, kisha CAG atasimamia hoja ya pesa ya umma haikukusanywa, ambayo hili ni haki.
Lakini wanafunzi wengi wanashindwa kumalizia hiyo sehemu ya ada. Unaweza kusema baba yake ana nyumba bora, baba yake ana mshahara mkubwa, lakini nyumba hizo hakuna anayepanga; mishahara hiyo wamekopea, hakuna kitu. Na wengine ni watoto wa wakulima, hali ni mbaya zaidi, ati unamyima mwanafunzi mkopo kisa amesoma shule binafsi, hili siyo sahihi.
“Ifahamike wazi kuwa kusomeshwa na serikali ni fursa ya kila Mtanzania , inalinda heshima ya serikali kwa vijana wake, lakini linapofanyika hili kwa ubaguzi siyo sahihi maana kodi inapolipwa na kila mmoja analipa, kwa nini tufanye ubaguzi?”
Tunaendeleaje na hali kama hii? Nani huyu mwenye mapembe makubwa tunayemuogopa? Pesa ni zetu, nchi yetu; kwanini tuwatese watoto wetu?
Mwanakwetu, ninahuzunika sana kuona wasomi wetu, akiwemo Profesa Adolf Mkenda na Katibu Mkuu Elimu, Profesa Carolyne Nondo, wameshindwa kushauri hili vizuri.
Mathalani, Profesa Nondo ni msomi, lakini akiwa anaongea na umma ana maelezo mengi yasiyokwisha. Hana summary; maelezo mengi ya nini? Hautaheshimiwa kwa maelezo mengi unayoyatoa katika umma. Utaheshimiwa kama kiongozi kama unatatua kwa wakati changamoto za watoto wa Kitanzania katika ngwe uliyopewa.
“Mkiwa viongozi, saidieni hawa watoto wetu. Hata nyinyi mmesaidiwa na watu; upo ushahidi mkubwa, na ndiyo maana leo hii nyinyi mnaitwa wasomi.Sasa tunawadai huo usomi tuuone katika kutatua changamoto hizo”
Je, tukisema hawa viongozi maprofesa wanatupotezea muda, hawaoneshi umahiri katika nafasi wanazopewa, tutakuwa tumekosea? Tunataka umahiri katika kazi na kuyatatua matatizo kwa wakati.
Mwanakwetu, nashauri Bodi ya Mikopo kuhusu ada ya wanafunzi kwenye vyuo binafsi wapewe, lakini vyuo vya umma vimejengwa kwa kodi ya Watanzania au wakati mwingine kwa mikopo ambayo Watanzania wanalipa. Siyo sahihi mwanafunzi akose kukamilisha karo ya 800,000, asifanye mitihani na aache masomo. Hili siyo sahihi.
Nasisitiza haya:
“Profesa Mkenda, badilisheni mitazamo yenu, muwafanyie kazi Watanzania wengi. Profesa Nondo, acha maneno mengi, dada yangu , acha maelezo mengi; wasaidie mabinti wa Kitanzania wasome. Kama CAG ameshauriwa hili, amegoma, tujue yeye ni tatizo ili tuangaike nayeye. Lakini Dkt Charles Kicheere ni muelewa. Vinginevyo, wewe Profesa Mkenda na Profesa Nondo hampaswi kubaki katika nafasi hizo; mnapaswa kuondolewa mara moja.”
Kwa leo inatosha sana.
Salaam ziwafikie Profesa Mkenda na Profesa Nondo, popote mlipo. Pesa Yetu, Nchi Yetu, Kwanini Tuwatese Watoto Wetu
Mwanakwetu, upo? Kumbuka.
“Pesa Yetu, Nchi Yetu, Kwanini Tuwatese Watoto Wetu.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)







.gif)
Post a Comment