KILA JAMBO LINA ALFA NA OMEGA

 




Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Haya yalikuwa mazingira ya mkahawa ambao, kwa kweli, ulikuwa umechoka sana. Wapishi na mwenye umiliki wa mkahawa huo walikuwa wa kabila la Wakisi, jamii inayohusishwa na marehemu Deo Philikunjombe.

 

Wakisi ni jamii inayojulikana kwa watu wake watulivu, wenye busara na wanaothamini elimu. Kwa mujibu wa mtazamo wa Mwanakwetu, ukanda huu pia unaaminika kuwa miongoni mwa maeneo nchini Tanzania yenye wasomi wengi.

 

Kwa faida ya msomaji wangu, nitaje baadhi ya wasomi ninaowafahamu kutoka ukanda huu: Profesa Andolongwise Katule na Profesa Nicolous Bangu. Hawa walikuwa maprofesa kweli, si maprofesa wa kutengenezwa.

 

Mwanakwetu alinunua chakula katika mkahawa huu kwa heshima ya marehemu Deo Philikunjombe, lakini pia kwa heshima ya familia nyingine za Wakisi ambazo ana uhusiano nazo.

 

Msomaji wangu unaweza kujiuliza: Mwanakwetu alijuaje asili ya wamiliki wa mkahawa huu?

 

Jibu lilikuwa rahisi tu: majina yao yote yalikuwa na asili hiyo.

 

Katika mkahawa huo kulikuwa na watu wengine waliokuwa wakizungumza kwa makundi. Mwanakwetu alipokuwa ameketi kwenye meza yake, akaja mtu mwingine akamsalimia, kisha akaagiza ugali, nyama, maharage na mboga za majani.

 

Baada ya muda mfupi, yule mtu akasema:

 

“Dada, nina njaa sana kweli. Ugali huu nitashiba?”

 

Mhudumu hakujibu kitu.

Meza nyingine nazo zilikuwa na mazungumzo, hasa kuhusu siasa, ingawa baadhi ya watu walizungumza kwa sauti za chini.

 

Mwanakwetu akaendelea kula.

Pembeni yake alikuwapo trafiki mmoja aliyekuwa amevua kofia yake na anakula kwa wasiwasi. Alikuwa amegeuza mgongo kiasi, huku akila haraka kana kwamba kuna jambo lililokuwa likimsumbua, huku akigeukageuka.

Kwa mtazamo wa Mwanakwetu, wasiwasi wa kijana huyo trafiki uliibua maswali mno, huenda ulikuwa na sababu kubwa nay na msingi.

 

Mwanakwetu akawaza mambo manne:

Labda alikuwa na kesi kazini.

Labda alikuwa na kazi iliyohitaji kufanyika muda mfupi baada ya kula.

Au labda sasa vijana wetu wa vyombo vya ulinzi na usalma hawawaamini raia ambao ni ndugu zao ambapo ndiyo wanaowazaa?

Au labda mjadala uliokuwa ukiendelea katika mkahawa ule ulikuwa umemfanya atafakari mambo mengi.

 

Hayo yote Mwanakwetu aliyawaza tu.

Lakini mjadala ule ulikuwa na anuani moja kubwa:

 

“Je, kwa sasa CCM ipo au haipo?”

Jamaa mmoja akasema:

 

“Kwa sasa CCM ipo wapi? Mimi ni Katibu wa CCM wa Kata. Hata mihutasari ya chama kutoka ngazi ya tawi, kata hadi wilaya, nani anaandika? Vikao hivyo vinafanyika lini? Wewe unasikia tu Kamati Kuu imekaa, Halmashauri Kuu imekaa, vikao vimefanyika kwa njia ya mtandao. Lakini vikao vya chama vinaanzia ngazi ya chini. Chini kumekufa, juu kuna nini? Chama kipo juu, chini hakuna. Chama kiwepo angani, chini hakuna.Mungu mwenyewe yupo huko alipo lakini duniani anawatuma wajumbe wake, anafahamu kila kinachofanyika.”

 

Hawa jamaa wawili walikuwa wamekaa kwenye meza ya pembeni.

 

Mjadala ukaendelea.

Mmoja wao akasema:

“Kwa sasa huwezi kuwa mbunge mpaka uwe na milioni 700 za kuhonga. Wewe kijana wa UVCCM, ndiyo kwanza umemaliza Chuo Kikuu au unasoma VETA;au ulikiwa Miss Temeke hiyo pesa ya kuwahonga wajumbe wa CCM, milioni 500-700, unaitoa wapi? Baba na mama yako masikini. Matajiri wakiingia sehemu wanaharibu kila kitu, yaani kwenye dini mkiwakaribisha umakini unahitajika. Hata ukiwa unataka kuwa mbunge wa Viti Maalumu kazi yao kuhongwa tu.Sasa hapa ni mawili lazima: ama ufanye biashara haramu, au matajiri wenye fedha wakununue ili uwe wakala wao na kufanikisha mambo yao.”

 

Mjadala ukawa mzito zaidi.

Jamaa mwingine akasema:

“Ukisema CCM ina changamoto, unakosea. CCM haipo? Imekufa, tena kifo cha mende.Tatizo ni hawa watu walioaminiwa na wazee wetu. Wametuwangusha. Na kama wametuangusha, lazima na sisi tuwaangushe. Na changamoto kubwa zaidi ni hili la Dkt. Emmanuel Nchimbi. Hili limewaharibia kabisa.”

Kumbuka haja jamaa wanaongea mkahawani.

 

Yule trafiki alikuwa mweupe na amenyolewa kipara. Ghafla akasimama, akalipa fedha yake na kuondoka haraka.

 

Alipokuwa akiondoka, jamaa mmoja akasema:

“Naona mnaongea kwa uhuru sana. Mnasema bila woga. Hata polisi hamumuogopi?”

 

Mwingine akajibu:

 

“Unamuogopea nini? Yeye mwenyewe anakula ugali kwa mashaka-mashaka ili awahi kurudi kibaruani kwake juani.

“Pengine msafara utapita hivi punde, naye anatakiwa akatafute ugali wa wanawe. Sasa kila mmoja anahangaikia mashaka yake.”

 

Mjadala ukaendelea.

 

“Inawezekana matajiri katika kila eneo ndiyo wanaowafanikisha vijana wa UVCCM kuwa mawakala wao, kuwa wabunge na baadaye kuingia serikalini. Na wao ndiyo wanaogharamia hizo milioni 500-700 za kuhonga.

“Sasa hivi tujiulize: Julius Nyerere alipokuwa mwalimu, kama angekubali kuhongwa na kuwa wakala wa matajiri, leo tungekuwa wapi?

“Nani angekuwa wakala wa Watanzania maskini? Nani angekuwa wakala wa wakulima na wafanyakazi?

 

“Ndiyo maana tunasema CCM imeshindwa kulishughulikia suala la rushwa.”

Mwanakwetu alipomaliza kula, akasimama, akalipa fedha yake na kuondoka.

 

Mazungumzo na Emmanuel Yesaya

Akiwa njiani, Mwanakwetu aliwasiliana na Kada wa CCM jijini Dar es Salaam, Emmanuel Yesaya.

Naye akamwambia:

 

“Makwega, mimi na wewe tunafahamiana. Dkt. Emmanuel Nchimbi anawafahamu vizuri viongozi hawa wa leo. Badala ya kumsikiliza, wao wanapambana naye. Kilichowauma ni msimamo wake kuhusu Katiba Mpya. Hakuna kingine. Hili si jambo salama kwa CCM. Kama kuna jambo, viongozi lazima wazungumze.Hata kama wewe ni kiongozi katika ya sasa inakusaidia wewe leo je utakaa kuwa kiongozi milele? Kama viongozi wanakamatana na kushindwa kuzungumza, je, mwananchi wa kawaida anapata tafsiri gani? Kama suala la Humphrey Polepole bado halijaisha, vipi kuhusu la Dkt. Emmanuel Nchimbi? Kila jambo lina Alfa na Omega.”

 

Baada ya mazungumzo hayo, ndipo Mwanakwetu akaamua kuyaandaa mazungumzo na matukio aliyokusanya katika makala hii.

 

Mwanakwetu Anasema Nini Leo?

Haya ni makala ya muhtasari wa mambo yaliyokusanywa na Mwanakwetu kati ya Agosti 25, 2026 na Agosti 29, 2026, mara baada ya Dkt. Emmanuel Nchimbi kujiuzulu nafasi ya Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mwanakwetu, upo?

Kama upo, basi kumbuka jambo hili:

“KILA JAMBO LINA ALFA NA OMEGA.”

Kila jambo lina mwanzo wake.

Kila jambo lina mwisho wake.

Na kila jambo, siku moja, hufika kwenye ukurasa wake wa mwisho.

Nakutakia siku njema.


Barua pepe: makwadeladius@gmail.com


Simu: 0717649257
















 

 

0/Post a Comment/Comments