“KAMWE HATUTAKUBALI KUFANYA HIVYO” — JULIUS NYERERE

 

 

Adeladius Makwega – Mbagala

 

Kuna wakati historia haipo kwenye vitabu pekee. Wakati mwingine hujificha katika karatasi ya zamani, picha, barua au hotuba iliyowahi kutolewa miongo kadhaa iliyopita.

 

Kazi kubwa ni kuipata, kuihifadhi na kuhakikisha inafika kwa kizazi cha leo na kesho.

 

Hiyo ndiyo kazi inayofanywa na taasisi mbalimbali, za umma na binafsi, nchini Tanzania, Umoja wa Mataifa na duniani kote.

 

Safari hiyo haiishii katika kuzipata kumbukumbu; zinakusanywa, zinahakikiwa na kuhifadhiwa ili wananchi, watafiti na vizazi vijavyo waweze kuzifikia.

 

Miongoni mwa kumbukumbu hizo ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika mwaka 1961, wakati wa makabidhiano ya Tanganyika kutoka kwa Gavana Sir Richard Turnbull.

Lakini swali linabaki: Je, hotuba hiyo inapatikana yote, neno kwa neno? Tuseme ipo na inapatikana.

 

Kwa mtu wa kawaida, inaweza kuonekana kama karatasi ya zamani. Lakini kwa taifa, ni kipande muhimu cha historia kinachoweza kuturudisha katika wakati ambao Tanganyika ilikuwa ikifungua ukurasa mpya wa safari yake.

 

Historia inapohifadhiwa, haibaki kuwa hadithi ya zamani. Huwa daraja linalounganisha kizazi cha jana, cha leo na cha kesho.

 

Jambo la muhimu ni hili: Mwalimu Nyerere hakuwa na hotuba hiyo pekee. Alitoa hotuba nyingi zilizobeba misimamo, falsafa na mtazamo wake kuhusu taifa, Afrika, amani, uhuru na haki za binadamu duniani.

 

Leo nakuletea sehemu ya hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1985.

 

Mwalimu Julius Nyerere alitoa hotuba hiyo akiwa Rais wa Tanzania, mbele ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, siku ya Ijumaa, tarehe 27 Septemba 1985. Ilikuwa miongoni mwa hotuba zake muhimu katika jukwaa la kimataifa na pia hotuba yake ya mwisho katika Mkutano Mkuu akiwa Rais.

 

Katika sehemu hiyo, Nyerere alisisitiza msimamo wa Tanzania wa kutokaa kimya mbele ya hatari au sera anazoona zinapingana na amani na haki.

**“Katika hotuba yangu hii ya mwisho mbele ya Mkutano Mkuu, nimeeleza matukio, mwelekeo na mahitaji kama tunavyoyaona sisi Watanzania. Nchi yangu haitaacha kusema mambo hayo hata Rais mpya atakapochukua madaraka. Kwa kuwa sisi ni nchi maskini na isiyoendelea, hatuna nguvu yoyote duniani isipokuwa nguvu ya kusema tuliyopewa na Mkutano huu—na nguvu ya utu wetu. Kukaa kimya tunapoona hatari, au kujizuia kukosoa sera ambazo tunaona zinapingana na maslahi ya amani na haki, kungekuwa ni kusalimu amri kwa uhuru na heshima yetu. Hilo kamwe hatutafanya.”

 

Rekodi rasmi ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa hotuba hiyo imehifadhiwa katika kumbukumbu yenye alama A/40/PV.13.

Kauli hiyo inaacha swali muhimu kwa msomaji wa leo:

 

Je, kizazi cha sasa bado kinazifahamu hotuba na kumbukumbu zinazobeba misimamo ya waasisi wa taifa?

Nakuuliza wewe unayesoma na kusikia makala haya.

Hili lazima tutafakari.

 

Kwa sababu kila hotuba inayohifadhiwa ni zaidi ya maneno. Ni sauti ya jana inayorudi kuzungumza na kizazi cha leo.

Mwanakwetu, upo? Siku ya leo nilitamani ufahamu haya.

KUMBUKA:

“HILO KAMWE HATUTAFANYA.”

Nakutakia siku njema.


Simu: 0717649257


Barua pepe: makwadeladius@gmail.com


 







0/Post a Comment/Comments