Imani, Unyenyekevu na Heshima kwa Ibada

 



Adeladius Makwega – DODOMA

 

“Tuko katika Jumapili ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa. Katika Injili ya leo, Yesu anawauliza wanafunzi wake: ‘Watu wanasema Mwana wa Adamu ni nani? Nanyi mnasema mimi ni nani?’

Wanafunzi wanamweleza Yesu jinsi watu wanavyomfikiria. Wengine wanasema yeye ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, na wengine Yeremia au mmoja wa manabii.

 

Yesu anapowauliza kuhusu uelewa wao binafsi juu yake, Simoni Petro anakiri hadharani: ‘Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.’

 

Ndugu zangu, tazameni jibu la Yesu:

‘Heri wewe, Simoni, mwana wa Yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia jambo hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.’

 

Bwana anawafundisha wanafunzi wake kwamba ni Baba ambaye amemwezesha Simoni Petro kukiri imani yake. Hii imekuwa baraka yake ya pekee. Anakuwa Petro, mwamba, ambaye juu yake Bwana angejenga Kanisa lake; msimamizi aliyepewa jukumu la kulitunza Kanisa la Yesu.

 

Simulizi hii itaendelea Jumapili ijayo.

 

Ndugu zangu. Lakini leo, tutafakari jambo hili: Imani katika Yesu ni zawadi tunayopewa na Baba. Si matokeo ya akili na uelewa wetu wenyewe.

Unyenyekevu ni muhimu ili kuwa msimamizi mwema katika Ufalme wa Mungu.”

 

Haya ni maelezo ya utangulizi wa mahubiri ya Kadinali Luis Antonio Tagle, ambaye ni Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki, yenye makao yake makuu Vatican.

 

Jumapili hii, Agosti 23, 2026, Mwanakwetu alisali katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

 

Katika misa ya kwanza, iliyoanza saa 12 kamili, kulikuwa na mapadri watatu altareni: paroko pamoja na mapadri wengine wawili.

 

Padri aliyeongoza misa aliifanya kwa utulivu mkubwa. Maneno yake yalisikika vizuri na ibada ilikuwa ya utulivu, bila papara.

 

Katika mahubiri yake alisema:

“Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hapa duniani. Mwanadamu ameumbwa kwa namna ya ajabu, namna ya pekee. Ndiye kiumbe pekee aliyeagizwa kwenda kuzaliana na kuongezeka. Mungu angeweza kuamua wanadamu wasizaliane au angeweza kuamua vinginevyo, lakini sasa Mungu anatenda kupitia wanadamu; siyo kwa mawazo yetu, uwezo wetu au akili zetu, hapana.”

 

Padri huyu aliendelea kuhubiri kwa kusema:

 

“Hata katika uongozi, uwe wa kiserikali au kifamilia, haya yote yanatokana na Mungu. Yesu anamkabidhi Petro majukumu haya, huku kundi la wachache lililochaguliwa na Yesu kupitia wale 12 likipewa jukumu la kuendeleza kazi ya Yesu. Kazi hii iliendelea kukabidhiwa kwa wengine hadi ikafika huku Dodoma, hadi hapa Parokia ya Chamwino Ikulu. Kupitia Mtume Petro tunakabidhiwa kazi hiyo. Ndiyo maana walipewa jukumu hili: lolote watakalolifunga duniani litafungwa mbinguni, na lile watakalolifungua duniani litafunguliwa mbinguni.”

 

Haya ni ndani ya kuta na altare za Kanisa.

 

Lakini siku ya leo, Mwanakwetu alikutana na simulizi gani?

 

Mwanakwetu alipokuwa akirudi kutoka kusali misa hii ya kwanza, njiani alikutana na Bi. Lightness Waziri. Mama huyu ni mwanajumuiya wa Mtakatifu Sesilia katika Parokia ya Chamwino Ikulu, jumuiya ambayo Mwanakwetu anasali.

Agosti 22, 2026, Binti Waziri, mama wa Kizaramo, alifika nyumbani kwa Mwanakwetu kumualika kwenye sherehe ya kijana wake aitwaye Yoseph, ambaye angepokea Sakramenti ya Kipaimara Agosti 23, 2026, siku ya Jumapili ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa.

 

Bi. Lightness Waziri, dada wa Mwanakwetu, akasema:

 

“Naona umesali misa ya kwanza. Sisi ndiyo tunakwenda misa ya Kipaimara. Ila usisahau kuja kwangu tule pilau ya Kipaimara pamoja…”

 

Mwanakwetu akamjibu:

 

“Sawa, nitakuja.”

 

Alipoagana na Lightness Waziri, mbele kidogo Mwanakwetu akakutana na mama mmoja wa Kigogo, mwanajumuiya mwenzao ambaye naye alikuwa akiwahi misa ya Kipaimara. Mwanakwetu akamsalimu na kisha wakaagana.

 

Mwanakwetu akaendelea kutembea mwenyewe kurudi kwake. Njiani akakumbuka tukio moja la zamani sana katika vigango vya Kanisa Katoliki huko Uzaramoni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, miaka ya 1988–1993, katika Parokia ya Mbagala.

 

“Tulikuwa tunafika Kigango cha Kiparang’anda saa 10 jioni. Hiyo ilikuwa Jumapili ya tatu kwa mwezi. Tulikuwa na Padri Wolfram, na mara moja moja Padri Fidelis.Waamini kutoka jamii ya Wamakonde na watumishi wa serikali Wakatoliki kule vijijini, kama vile walimu, wauguzi, mabwana na mabibi shamba, walikuwa wakimsubiri padri tangu asubuhi hadi saa 10 jioni bila kuchoka. Padri alipofika, misa ilianza kusaliwa. Na haikuwa kwamba padri alikuwa amechelewa. Hapana. Padri tangu asubuhi alikuwa akisalisha misa katika vigango vingine, akianzia Vikindu, Kisele, Kiziko, Dundani, Mkuranga na mwisho akimalizia Kiparang’anda. Misa ilimalizika jua likiwa limezama, maana Jumapili ya tatu pekee ya mwezi ndiyo padri alikuwa akifika katika vigango hivyo. Jumapili zingine zilikuwa ni misa za katekista tu. Hawa Wakristo Jumapili ya tatu ya mwezi hawakukosa kusali.”

 

Haya ni ya zamani, lakini siku hizi makanisa unaweza kusikia kanisani yakisemwa maneno haya:

 

“Imbeni nyimbo zenye mashairi machache, kuna misa nyingine inafuata.”

 

Wakati mwingine ibada ya misa inaharakishwa kwa sababu kuna misa nyingine inayofuata.

Mwanakwetu anasema:

 

“Jamani, tukumbushane. Mbona wazee wetu hawakuwa hivyo? Mathalani, Padri Fidelis na Padri Wolfram hawakuwa wakiwaambia wale Wakristo wa zama zile,

 

‘Imbeni mashairi machache, tuna misa ya kigango kingine.’

 

“Binafsi sikuwasikia wakisema hivyo. Hakuna nafasi ya kuipunja misa kwa sababu yoyote ile, kwa kisingizio cha muda au misa nyingine.kila misa inapaswa kutendewa haki ile ile.”

 

Hili linawekwa katika makala haya kwa ajili ya kukumbushana tu.

 

Labda kwa leo nimalizie na kisa cha siku ya mazishi ya Padri Fidelis pale ndani ya Kituo cha Kiroho Mbagala. Nadhani ilikuwa mwaka 1993.

 

Binafsi nilikuwepo, ingawa kwa bahati mbaya sikutumikia katika misa hiyo. Siku hiyo watu walikuwa wengi na misa ilifanyika nje ya Kanisa dogo la Mtakatifu Antony wa Padua.

 

Mimi nilikaa jirani na ukuta wa Kanisa dogo la Mtakatifu Antony wa Padua. Misa ilikuwa ndefu sana na kulikuwa na matangazo mengi. Nakumbuka Kardinali Pengo hakufika kwenye mazishi siku hiyo. Padri aliyehubiri alikuwa padri mmoja makini sana.

 

Sehemu niliyokaa nilikuwa pamoja na vijana wenzangu watatu. Tulikuwa tunawahi majadiliano ya masomo ya saa moja usiku. Karibu yetu alikuwa Mzee Mwingizi, ambaye alikuwa Mpogoro.Katika vijana hao watatu, mmoja akasema:

 

“Duu, hii misa ni ndefu sana, haishi tu!”

 

Mzee Mwingizi, ambaye sasa ni marehemu, akasema: maneno haya kwa sauti ya ukali:

 

“Nyie vijana, tumekuja kumzika Padri Fidelis. Kwani kuna mtu amelazimishwa kuja kusali? Msiufanye muda kuwa sanamu yenu la kuabudu.

 

“Padri alikuwa hai, sasa amekufa. Ukija kusali, kunahitaji utulivu wa kila mmoja, tangu anayeongoza misa hadi waamini. Kila misa ina utaratibu wake. Kaeni hapo hadi misa imalizike.”

 

Yule kijana aliyekuwa amesimama akakalishwa chini kweli. Yule kijana aliufyata hadi misa ikamalizika. Ndipo tukaenda kwenye majadiliano yetu ya masomo.

 

Msomaji wangu, haya yote—kuanzia yale ya altareni hadi visa hivi viwili—ni mambo ya Jumapili hii ambayo nilitamani kuyatafakari pamoja nawe.

 

Imani, unyenyekevu, uvumilivu na heshima kwa ibada ni mambo yanayotukumbusha wajibu wetu kama waamini. Kanisa si mahali pa kukimbizana na muda, bali ni mahali pa kumwabudu Mungu kwa utulivu, heshima na moyo wa unyenyekevu.

Mwanakwetu, upo?

 Kumbuka.

Imani, Unyenyekevu na Heshima kwa Ibada.”

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments