Adeladius Makwega – Dodoma, Tanzania
Tuko katika Jumapili ya 20 ya mwaka A wa Kanisa. Katika Injili ya Jumapili hii, mwanamke Mkanaani anatupatia mfano wa kile ambacho Bwana anakita imani kuu.
“Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi. Binti yangu anateswa sana na pepo.”
Hata hivyo, Yesu anamjibu mwanamke huyo kwa maneno makali:
“Nimetumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli tu. Si vema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
Hapo ndipo mwanamke huyo wa Mataifa anapoonyesha ukubwa wa imani yake. Anamwambia Yesu:
“Tafadhali, Bwana, kwa maana hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza ya bwana wao.”
Jibu hili linaonyesha unyenyekevu wake, ufahamu wake kuhusu wokovu, pamoja na imani yake kwa Mungu ambaye ni wa watu wote. Kwa wingi wa rehema za Mungu, kila mtu anaweza kupata sehemu katika neema yake.
Neema ya Mungu itamfikia kila mmoja wetu, ndugu zangu. Imani katika Yesu inaweza kuwaunganisha watu wa tamaduni na rangi mbalimbali.
Haya ni baadhi ya mafundisho yaliyotolewa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Kiranja Mkuuwa Idara ya Uinjilishaji ya Kanisa Katoliki inayohusika na uenezaji wa Injili duniani.
Nako katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padri aliyesalisha Misa ya kwanza alisisitiza sana umuhimu wa kuwa na mahusiano mema katika maisha yetu. Alieleza kuwa kila tunayeishi naye jirani ni shahidi wa maisha yetu, iwe katika ndoa, familia, ujirani au katika mazingira mengine ya maisha.
Katika parokia hii, jambo lingine kubwa lililosisitizwa kwa waamini ni kukamilisha maandalizi ya kumpokea Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya, ambaye anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Kipaimara.
Majira ya saa moja kamili asubuhi, Mwanakwetu alipokuwa akitoka kusali Misa hii ya kwanza, alikutana na akina mama watatu waliokuwa wakiwahi ibada ya pili. Kwa ilivyoonekana, wawili kati yao walikuwa waamini wageni katika parokia hiyo. Mmoja wa wageni hao alisema:
“Kule tulikokuwa kulikuwa na kwaya ya watoto, na yenyewe ilipangiwa kuimba kama kwaya nyingine. Hili lilitusaidia mno, maana watoto wale walijifunza kuimba mapema. Kwaya ilikuwa na kila kitu, hadi sare, ilikuwa na akaunti na uongozi imara. Hata mimi nilijifunza kuimba mapema sana. Sina hakika kama makanisa mengine yana kwaya za watoto imara, thabiti na ya kuigwa kama ile…”
Kwa kuwa walikuwa wakipishana , Mwanakwetu hakuyasikia mazungumzo yote. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalitosha kumfanya atafakari kwa kina kuhusu nafasi ya watoto katika maisha ya Kanisa.
Swali ni kwako wewe unayesoma makala haya: Je, kanisani kwako kuna kwaya ya watoto ya aina hiyo?
Najua jibu unalo sisi watu wa mataifa ?
Kama mwanamke Mkanaani alivyodhihirisha imani yake kwa unyenyekevu na uvumilivu, ndivyo tunavyopaswa kuwalea watoto wetu katika mazingira yatakayowajengea imani, vipaji, nidhamu na upendo wa Kanisa. Kwaya ya watoto si mahali pa kuimba tu. Inaweza kuwa shule ya malezi, nidhamu, ushirikiano na imani. Mtoto anayepata nafasi ya kushiriki katika huduma za Kanisa tangu akiwa mdogo hujifunza kuwajibika, kushirikiana na wengine na kulitumikia Kanisa kwa moyo. Kwa hiyo, ni muhimu kila parokia kutafakari: Tunawapa watoto wetu nafasi gani katika Kanisa? Tunawajengea mazingira gani ya kukuza vipaji vyao na imani yao?
Kumbuka
Imani inaweza kuunganisha watu wa tamaduni, rangi na mazingira mbalimbali. Lakini pia imani inahitaji kulelewa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Watoto ni sehemu muhimu ya Kanisa la leo na la kesho.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)

.gif)
Post a Comment