Adeladius Makwega – Mbagala
Tanzania ya sasa inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 72. Idadi hii inaweza kuongezeka mara mbili ndani ya kipindi kifupi, kwa kuwa idadi ya watoto na vijana ni kubwa kuliko idadi ya watu wazima na wazee.
Kulingana na takwimu za idadi ya watu katika Afrika ya Kati, Mashariki na Pembe ya Afrika, Ethiopia inaelezwa kuwa na watu takribani milioni 180, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa na takribani milioni 100, huku Tanzania ikiwa na watu kati ya milioni 68 na 73.
Kwa ukweli wa Mungu, watu milioni 73 wa Tanzania, ukilinganisha na watu milioni 100 wa Kongo, idadi ya watu wa Kongo inaonekana kuwa na nafuu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwemo migogoro ya kivita, kuliko Watanzania. Maana, kwa Kongo, changamoto za majanga zimekuwa sehemu ya maisha yao kwa muda mrefu.
Kwa sasa, Mwanakwetu anahisi kuwa hali hii ya Kongo inaweza kuhamia Tanzania ikiwa viongozi wa Tanzania na dunia kwa ujumla kama wataendelea kudhani kuwa hali ya Tanzania bado haijavuka mstari mwekundu.
Mawazo haya yamemjia tu Mwanakwetu siku ya leo, na akaamua kutafakari jambo hili pamoja na wewe, msomaji wake.
“Unapopewa nafasi ya uongozi katika mataifa yenye binadamu zaidi ya mmoja, inapotokea shida, mathalani vita au janga lolote, maana yake jamii hii inakuwa kero kwa jamii jirani. Dunia inaingia gharama katika kulitatua jambo hilo, na kusababisha madhara makubwa kwa jamii jirani, ikiwamo hata kusambaa kwa magonjwa fulani wakati wa janga hilo, ukimbizi, na kulishwa chakula watu waliokuwa wakifanya shughuli zao.”
Msomaji wangu, naomba nikurejeshe nyuma zaidi.
Wakati Mwingereza alipomkabidhi Julius Nyerere Tanganyika, Desemba 9, 1961, hawa jamaa walijiridhisha kwa asilimia 100 kuhusu tabia, mwenendo na hata hulka ya Nyerere; alikuwa mtu wa namna gani katika hali zote, iwe furaha au matatizo.
Ndiyo kusema, Tanganyika African National Union (TANU) ndiyo iliyokabidhiwa Tanganyika kwa mikono miwili, wakiamini kuwa nchi hiyo ingebaki salama.
Mtu mmoja aliniambia kwamba hata zile kesi za awali za Julius Nyerere, Mzungu alikuwa akipima namna Julius Nyerere alivyokuwa baada ya kukutana na matatizo. Hili sina hakika wala sijathibitisha ukweli wake, lakini niliambiwa hivyo.
Hata huko Kongo, Patrice Lumumba alikuwa ameandaliwa, lakini tatizo ni kwamba wale waliomuua walifanya hivyo mapema sana, na baadaye nchi ikaingia katika mikono ya madhalimu.
“Tanganyika haikukabidhiwa chini ya KAR, chini ya Jeshi la Polisi lililotoka kwa mkoloni,Jeshi la Magereza na wala chini ya Idara ya Usalama iliyotoka kwa mkoloni. Bali ilikabidhiwa kwa watu wa Tanganyika, Nyerere na wenzake, wakifahamika kwa majina yao, koo zao na baba zao, hulka zao na tabia zao. Huku vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa wasaidizi tu, kama walivyokuwa walimu, wauguzi na watumishi wengine.”
Taifa la watu milioni 73 linapotokea tatizo, watu wengi wanaweza kupoteza maisha, kupata vilema vya kudumu na kadhalika.
Watanzania wanakumbuka yale ya Oktoba 29, 2025. Sitaki kuwarudisha katika haya, maana naamini Mungu mwenye rehema atawahukumu waliofanya haya mmoja baada ya mwingine na vizazi vyao.
Kunapotokea tatizo, hata kama limegusa mtu mmoja tu, lazima lifanyiwe kazi haraka. Maana unaweza kusema, “Hali hii haijavuka mstari mwekundu.” Lakini tambua kwamba katika hoja ya uhai wa binadamu, hata kama ni mtu mmoja tu, jambo hilo limevuka mstari mwekundu lazima lifanyiwe kazi.
Mawazo haya pia yanaonekana katika misimamo ya marais wawili wa Marekani, Franklin Roosevelt na Harry Truman.
Rais Truman, katika hotuba yake kuhusu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, alikwenda mbali na kutoa maelezo haya:
“Kama dunia ingekuwa na Umoja Imara, basi idadi ya watu waliofariki katika Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia isingalitokea. Lakini kuanzia sasa, mwaka 1945, Umoja wa Mataifa lazima tuwe wakali zaidi ili vifo vingine vya binadamu visitokee. Maana, kama vitatokea, itakuwa ni kwa uzembe wetu; na hata ninyi leo hii mnaopiga makofi mtafariki, mtakuwa marehemu kwa uzembe huo.”
Haya ni Mwanakwetu anayatafakari huku macho yake yamejawa na machozi: Taifa la Tanzania, hivi tunakwenda wapi, jamani?
Unaweza kusema, kwa nini Mwanakwetu siku ya leo anakufukuru?
Mwanakwetu, kwa umri wangu, nimeshiriki vikao vya CCM tangu ngazi ya shina, tawi, kata, wilaya, mkoa na hata vikao vya taifa, kwa kuingia kama mjumbe halali , kama mwalikwa na wakati mwingine kama mgombea ili kujieleza na kuulizwa maswali ili kutimiza haki ya kuchaguliwa.
Mwaka 2010, Mwanakwetu niligombea nafasi ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Uspika, siku ambayo CCM ilimpiga mkasi Mheshimiwa Samwel Sitta.
Kikao kilifanyika Makao Makuu ya Chama, Dodoma, na Mwanakwetu nilialikwa. Baadaye, Mwenyekiti wa CCM Taifa wa wakati huo akaagiza watia nia tuingie ukumbini, tutambuliwe, tujieleze na kuulizwa maswali.
Katika watia nia wote, nadhani Kazimbaya Makwega na kijana mmoja, mhasibu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, ndiyo tulikuwa watia nia wenye umri mdogo.
Katika kikao hiki, lipo jambo lililonishangaza sana, hasa wasaidizi wa Rais, ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa waliokuwa mbele jukwaani huku wakingia na kutoka. Mara wanaingia, mara wanatoka; wote wakiwa vijana kutoka vyombo vya ulinzi.
Mtu mmoja wetu akasema maneno haya:
“Hivi vikao vya taifa mbona vinachekesha? Hawa wasaidizi wa Rais, ambaye ndiye Mwenyekiti wa chama, wao ni wajumbe? CCM Taifa haina sekretarieti? Wao, kama wanamsubiri Rais, wangebaki mapokezi. Hapa yeye ni mwanachama wa CCM na mwenyekiti wa kikao.
Katika vikao vya tawi, hivi mlinzi wa magari ya tawi la CCM au mlinzi wa mwenyekiti wa tawi anaweza kuthubutu kuingia ukumbini wakati mjadala wa waliomba kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa unafanyika? Hili haliwezekani.”
Mwanakwetu nikamwambia:
“Si huko tu. Hata ngazi ya wilaya na mkoa, mtu hawezi kuingia kikaoni zaidi ya mjumbe halali wa kikao.”
Jamaa akasema:
“Hivi huyo mwenyekiti wetu akikengeuka, mnaweza kushughulika naye katika vikao vya chama? Au mwenyekiti ni malaika aliyekamilika kwa asilimia 100?
Pale CCM, Green Guard pamoja na sekretarieti yao ndiyo wenye jukumu la ulinzi na huduma zote ndani ya kikao. Maana wale wanaorandaranda siyo sekretarieti; wako kwa ajili ya mtu mmoja.”
Haya mambo yote yamempa tafakari kubwa Mwanakwetu, na kisha kusema haya:
Hii ni hatari, maana inawapa tamaa watumishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama kutaka kufanya siasa na kuchagua upande fulani wakati wa matatizo au taifa linapoingia njia panda.
Hii ni hatari, na ndiyo maana Ibara ya 147(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inapiga marufuku rasmi mwanajeshi, polisi au mwanachama yeyote kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama kujihusisha na chama chochote cha siasa.
Sheria hii imewekwa ili vyombo vya ulinzi na usalama vibaki huru na visitoke upande wowote wa kisiasa. Pia, hoja ni kwamba vitatumikia wananchi wote na taifa lote kwa usawa.
Swali ni: Je, vipi katika uteuzi wa wanajeshi, polisi na watumishi wengine wa vyombo hivyo katika nafasi za kisiasa?
Tukumbushane: hoja ni ile ile — ni ukiukwaji wa Ibara ya 147(3).
Hii inazuia hamu na tamaa ya baadhi ya watu katika vyombo hivyo kuzitamani nafasi hizo na hata kuchagua upande ili kujinufaisha.
Hoja hii leo inaweza kuonekana kuwa ndogo, lakini siku moja inaweza kutugharimu mno na kuwagharimu wahusika.
“Maana sasa Tanzania maneno ni mengi. Humphrey Polepole yupo wapi? Wamechukua huyu, wamefanya hivi, wamempeleka kule; mbona haonekani? Dkt. Emmanuel Nchimbi, mbona simu zake haziiti? Mbona, mbona, mbona vyombo vya ulinzi havina majibu? Je, huko kukaa kimya siyo kuchukua upande wa kisiasa? Huko siyo kukiuka Ibara ya 147(3)?”
Mwanakwetu, upo?
Kumbuka:
“HAVIPASWI KUCHUKUA UPANDE WA KISIASA.”
Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257
.gif)





.gif)
Post a Comment