Adeladius Makwega – Mbagala
“Makwega, suala la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ni tatizo kwa watoto wetu. Pia, huu mtindo wa wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Nne kupangiwa kwenye vyuo vya kati bila kuwezeshwa mikopo ni kuua ndoto za vijana wetu. Ikiwa vijana hawa hawakuweza kumudu michango wakati wa elimu bure, watawezaje kulipa ada ya vyuo vya kati inayofikia hadi shilingi milioni moja na laki tano?”
Huu ni ujumbe ambao Mwanakwetu ameupokea kutoka kwa mdau mmoja wa elimu akihoji kuhusu hali hii.
Je, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, pamoja na Katibu Mkuu, Caroline Nondo, mna majibu gani kuhusu hoja kama hizi?
Kila mmoja anatambua umuhimu wa programu kama MMES na MEMKWA, na namna ambavyo Serikali ilijitahidi kuwasaidia vijana katika mazingira hayo. Je, kwa kundi hili la sasa tumejipanga vipi kulisaidia?
Hoja ya msingi si kusema na kuongea kana kwamba unajibu hoja. Hoja ya msingi ni kwamba, kabla ya kuwapeleka wanafunzi hawa kwenye vyuo vya kati, ambako wengi wao wanatoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi, mlipaswa kuandaa utaratibu wa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya kuwawezesha kuendelea na masomo.
Kuna baadhi ya watu wanafanya uzembe wa kufikiri na kudhani kwamba watoto wao hawapo katika kundi hili kwa sababu wamefaulu vizuri. Huu ni mtazamo usio sahihi. Niwaambie jambo ambalo huenda hamjalifikiria.
“Kundi hili linalopuuzwa leo ndilo litakaloishi na kuzaana na watoto wenu kesho, kwa sababu hakuna mtu aliyekamilika kwa asilimia 100.”
Unaweza kumpa mtoto wako elimu nzuri, lakini huwezi kuhakikisha kila kitu kuhusu maisha yake. Unaweza kumsaidia kupata mwenza unayemtaka wewe? Hauwezi kumchagulia mtu atakayekutana naye na kuishi naye. Anaweza kukutana na mtu kutoka katika kundi hili linalotaabika leo.
Ndiyo maana Mwanakwetu nasema Waziri na Katibu Mkuu wa Elimu hawatimizi wajibu wao ipasavyo katika kulishughulikia suala hili kwa uzito unaostahili.
Suala la elimu ya watoto wetu ni jambo linalohitaji viongozi wa elimu kulitazama kana kwamba nchi iko katika hali ya hatari. Kutokuwa makini katika jambo ambalo linaonekana dogo leo kunaweza kuleta balaa kubwa kwa taifa letu kesho. Mathalani, tunapowapoteza vijana hawa wenye nguvu na uwezo wa kulijenga taifa, tunakuwa tunapoteza sehemu muhimu ya nguvu kazi ya nchi.
Lazima tufahamu kwamba idadi ya vijana nchini Tanzania, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inapiga kengele ya tahadhari. Tanzania ilikuwa na vijana 20,612,566 wenye umri wa miaka 15–35, sawa na asilimia 34.4 ya Watanzania wote.
Kati yao, vijana wa kiume walikuwa 9,827,426, sawa na asilimia 16.4, huku vijana wa kike wakiwa 10,785,140, sawa na asilimia 18. Takwimu hizi zinaonesha wazi ukubwa wa kundi hili katika taifa letu na mchango wake mkubwa katika nguvu kazi ya nchi.
Naomba msomaji wangu akumbuke pia kwamba, kwa mujibu wa sensa hiyo hiyo ya mwaka 2022, watoto wenye umri wa miaka 0–14 walikuwa 26,399,985, sawa na takribani asilimia 43 ya Watanzania wote.
Ukiunganisha idadi ya watoto na vijana, unapata kundi kubwa sana la wananchi—zaidi ya milioni 47. Hili ni kundi ambalo taifa haliwezi kulipuuza.
Kama kweli tuna nia njema na watoto na vijana wetu, lazima tujiulize: Je, kozi za vyuo vya kati zinaweza kutolewa bure au kwa gharama nafuu kwa kundi kubwa la vijana ambao hawana uwezo wa kugharamia masomo?
Kwa mfano, mafunzo ya ufundi na stadi kupitia taasisi kama VETA yanaweza kuwa sehemu muhimu ya kuwapatia vijana ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Kutoa mafunzo haya kwa gharama nafuu au bure kwa vijana wenye uhitaji kutakuwa ni ishara ya wazi kwamba tunawathamini vijana hawa na tunatambua mchango wao katika Tanzania ya sasa na ya baadaye.
Kundi hili nalo litakua, litaanzisha familia na litazaa watoto. Watawaambia nini watoto wao kuhusu namna tulivyowatendea leo?
Swali ni moja tu:
Tutawezaje kukabiliana na changamoto zinazolikabili kundi la zaidi ya watoto na vijana milioni 47 kwa mbinu zipi?
Hatuwezi kufika salama ikiwa hatutachukua hatua sasa.
Wasomi wa Tanzania mliopewa dhamana ya kusimamia sekta mbalimbali, hasa elimu, acheni uvivu wa kufikiri na kuchukua hatua. Ikiwa unatoa ushauri wenye maslahi kwa taifa lakini watu hawautaki, una wajibu wa kusimama na kueleza msimamo wako. Na kama mazingira yanakulazimisha kujiuzulu, basi uwambie umma wazi:
“Nimejiuzulu kwa sababu hizi na hizi.”
Hatuwezi kuendelea kubaki vile vile kama kuna kujiuzulu kwa watu kadhaa ati mambo yatabaki yaleyale bila mabadiliko, shida ni kukaa kimya wakati mambo hayasongi mbele.
Kwa leo inatosha sana.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka.
“Elimu ya Vijana na Wajibu wa Serikali.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)








.gif)
Post a Comment