BWANA ATAKAPOKUJA TUTAMTAMBUA?

 

 


Adeladius Makwega – Chinangali, Dodoma, Tanzania

 

“Mungu anapatikana katika ukimya, siyo katika makelele. Katika haya makelele, mtuliza makelele wa kweli ni Kristo Yesu. Kuna zaidi kupatikana katika ukimya, maana Mungu mwenyewe ni mkimya.

Katika mtu mkimya na yule anayetamka malengo yake, nani anafanikiwa zaidi? Mkimya.

Sasa mfikirie huyu Mungu mkimya; matendo yake ni makuu. Hata Yesu alikuwa akienda mlimani akiwa na silaha ya kweli ya ukimya, na katika ukimya mambo yananyooka.

Mawimbi yakizidi, rudi kwa Yesu wa Ekaristi.”

 

Haya ni mahubiri ya Padri Evarist Mwaudama, Paroko wa Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, katika Jumapili ya 19 ya Mwaka A wa Kanisa. Katika mahubiri yake, Padri Mwaudama alijikita zaidi katika Injili ya Jumapili hiyo, akitukumbusha umuhimu wa kumtafuta Kristo katika ukimya, hasa wakati wa dhoruba za maisha.

 

Kwa upande wake, Kadinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, aligusia masomo ya kwanza na ya pili, akitukumbusha kwamba Bwana huja kwetu kwa namna ambazo mara nyingi hatuzitarajii.

 

Kadinali Tagle alisema:

 

“Bwana anakuja kwetu. Udhaifu wetu wa kibinadamu wakati mwingine unatufanya hata tujiulize kuhusu uwepo wa Mungu katika maisha yetu. Hasa pale tunapokumbana na hali ngumu, majaribu, kupoteza kazi, migogoro katika familia au kifo cha ghafla.

Watu wengine hujiuliza kwa haki kabisa: Je, Bwana bado yuko pamoja nasi? Au ametutelekeza?

 

Na pia nataka kutoa angalizo hili: mambo yanapokwenda vizuri, ni watu wangapi wanaona uwepo wa Bwana katika maisha yao?

 

Wakati mwingine hata hatushukuru Bwana. Kwa hiyo, iwe katika nyakati nzuri au nyakati mbaya, wakati mwingine tunakosa ule utambuzi kwamba Bwana yuko pamoja nasi. Ni pale tu tunapokuwa katika matatizo makubwa sana ndipo tunapoanza kumtafuta na kusema: ‘Uko wapi?’

Lakini ukweli ni kwamba, kama masomo ya Jumapili hii yanavyothibitisha, Bwana anakuja kwetu, na anakuja kwa namna ambazo sisi hatuwezi kumlazimisha wala kumwelekeza. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa tayari kuupokea uwepo wake, hata pale anapojidhihirisha kwa namna ya kushangaza. Hili ndilo tunaloliita utambuzi wa kiroho.

Kwa hakika, Mungu anakuja kwetu.”

 

Kadinali Tagle aliendelea kulieleza somo la kwanza, linalomhusu Nabii Eliya. Eliya, aliyekuwa akikabiliwa na mateso, alikimbia na kujificha katika pango lililokuwa kwenye Mlima Horebu. Alikuwa akikimbia kutoka kwa waliokuwa wakimtesa, lakini kwa namna fulani alikuwa pia anakimbia kutoka katika utume ambao Mungu alikuwa amempa.

Bwana alimwambia atoke pangoni na kwenda kusimama kwenye mlango wa pango, kwa sababu Bwana angepita hapo. Bwana alitaka kukutana na Eliya, lakini Eliya alipaswa kutoka katika hofu yake, kutoka katika kujificha kwake na kutoka katika sehemu yake ya usalama.

Upepo mkali ulipita, lakini Bwana hakuwa katika upepo huo.

Tetemeko la ardhi likaja, lakini Bwana hakuwa katika tetemeko hilo.

Moto ukaja, lakini Bwana hakuwa katika moto huo.

Baadaye ukaja mngurumo mdogo wa sauti ya kimya, sauti ndogo ya kunong’ona.

Hapo ndipo Bwana alipokuwa.

Kwa hiyo, kupitia simulizi la Eliya, tunafundishwa umuhimu wa hekima na utambuzi wa kiroho. Wakati mwingine tunadhani kwamba Mungu lazima aje kwetu kwa namna kubwa, yenye makelele na nguvu zinazoonekana. Lakini Mungu anaweza kutushangaza; Mwenye Nguvu zote anaweza kuja kwetu kupitia sauti ndogo kabisa ya kunong’ona.

Si kila kelele, ngurumo au tetemeko la ardhi linaloweza kutuonyesha uwepo wa Mungu. Wakati mwingine Mungu Mwenye Nguvu zote huja katika sauti ndogo na tulivu ya kunong’ona.

 

Katika somo la pili, Mtakatifu Paulo anaonekana kuwa na uchungu mkubwa kwa sababu watu wake mwenyewe, ambao ni watu wa ahadi na ambao ahadi za Mungu kwao haziwezi kubatilishwa, bado hawajamtambua Kristo.

 

Wao ni watu wa Mungu. Wamebarikiwa. Lakini bado hawajatambua wakati wa ujio wa Mungu kuwatembelea katika Yesu Kristo.

Tunaona pia ukuu wa moyo wa Mtakatifu Paulo. Anaumia sana na alikuwa tayari hata kulaaniwa ili watu wake wenyewe waweze kutambua kuja kwa Bwana katika Yesu Kristo.

Hili linatufundisha jambo muhimu: Bwana huja kwa namna ambazo hatuzitarajii, na katika hali ambazo zinakwenda kinyume na hekima na matarajio yetu ya kibinadamu.

Tunachohitaji ni neema ya utambuzi wa unyenyekevu.

Bwana anapokuja, tupate kumtambua.

 

Haya yote ni ndani ya kuta na mbele ya altare za Kanisa Ulimwenguni.

Lakini, Mwanakwetu, Jumapili hii ana simulizi gani?

 

MWANAKWETU AENDA MISA

Siku hii, Mwanakwetu alitoka nyumbani kwake saa 11:42 alfajiri, kuelekea Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Misa ya kwanza.

 

Akiwa njiani, aliona watu wawili mbele yake: mama aliyevaa gauni refu na baba aliyevaa suruali nyeusi na shati la rangi ya krimu.

Mwendo wa Mwanakwetu ulikuwa wa kasi zaidi, hivyo baada ya takribani dakika kumi alikuwa tayari amewakaribia. Akawagundua kuwa ni familia ya ndugu Mamba, akiwa na mke wake. Ni familia ya Kikatoliki ambayo Mwanakwetu anasali nayo katika Jumuiya ya Mtakatifu Sesilia.

 

Alipofika sambamba nao, aliwasalimu na kuendelea kuambatana nao kuelekea kanisani.

 

Baada ya takribani dakika tano za kutembea, pikipiki ya mtu aliyekuwa akielekea kusali iliwapita. Inawezekana alikuwa mwanakwaya. Jamaa huyo aliwasalimu:

 

“Tumsifu Yesu Kristo!”

Tukajibu:

“Milele amani!”

Kisha yule mwanakwaya akasimama, na Mzee Mamba akakimbilia kuipanda pikipiki.

Hapo ndipo mke wa Mzee Mamba aliposema:

“Makwega, huyu Mzee Mamba siku hizi anaimba kwaya. Leo hii kachelewa kuamka. Misa inaanza saa 12:00. Mungu bahati amempatia lifti ya bodaboda ili awahi kuimba kwaya, maana sasa ibada imeanza.

Unajua, Makwega, kule kwetu ili uwahi ibada ya Misa ya kwanza unatakiwa uamke saa 11:30. Leo sisi tumechelewa na wewe umechelewa.”

 

Mama Mamba na Mwanakwetu wakaendelea kutembea kuelekea kanisani, shoto kulia, shoto kulia, kwa mwendo wa kasi.

Ghafla, Mama Mamba akasema:

 

“Kanisa letu hili zamani nilikuwa najidai kweli kweli na yule Msukuma, John Pombe Magufuli. Yule kwetu hakuwa Rais tu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kwetu sisi Wagogo alikuwa mtani wetu. Lakini sasa hayupo...”

Mwanakwetu akabaki kimya.

Baada ya muda, Mama Mamba akauliza:

“Hivi Makwega, yule Humphrey Polepole yupo hai?”

Msomaji wangu, Mwanakwetu anajibu nini?

Walikuwa wanaendelea kutembea kwa mwendo wa kasi kuelekea kanisani—shoto kulia, shoto kulia—lakini swali lile likawa zito moyoni.

 

Mwanakwetu akamjibu Mama Mamba:

“Mama Mamba, unajua kazi ya Mungu haina makosa. Kwa sasa hivi tunajidai kupitia Yesu Kristo aliyefufuka kutoka katika wafu, John Pombe hayupo tena.

Lakini kwa hili la Humphrey Polepole, unajua mtu ni heri ujue yupo mahali fulani. Yupo mahabusu fulani, yupo gerezani fulani, yupo nyumbani kwa fulani, yupo kwa mganga wa kienyeji fulani, au hata ameliwa na mnyama porini hilo linakuwa jepesi.

Zamani kwetu Upogoroni, Mahenge, Morogoro, kabla ya wazungu kuja na Ukristo kuingia, ndugu yako angeweza kupotea, labda akaenda kwa mganga wa kienyeji, huko akafa na akazikwa.

Mkiuliza mkapata jibu: ‘Ndiyo, alikuwepo. Alikuwa anaumwa. Tukamtibu kwa dawa za mizizi, lakini hakupata nafuu; akafa.’

 

Pale pale mngechukua nguo zake na kuzipeleka kwenu kama ushahidi kwamba ndugu yenu alikufa. Au kama aliliwa na simba, vile vitambaa vya masalia ya nguo vingekuwa ushahidi.

Sasa huyu ndugu yupo wapi? Yupo na nani? Na hao waliokuwa naye wanamfanyia nini?

Hili jambo linaumiza sana, na mimi sina majibu.”

Walipokaribia kanisani, wimbo wa katikati ulikuwa ukiimbwa.

 

Hadi walipoingia kanisani, walikuwa wamechelewa. Padri alikuwa tayari akisoma Injili na baadaye akatoa mahubiri mafupi. Wakasali hadi ibada ilipofikia tamati.

 

Baada ya Misa, kila mmoja akarudi nyumbani kwa wakati wake.

Mwanakwetu, moyoni mwake, akaweka miadi na nafsi yake kwamba Jumapili ijayo ataamka mapema zaidi ili awahi ibada ya Misa ya Jumapili.

Je kisa hiki cha simulizi ya Mwanakwetu kina funzo lolote?

Hapo ndipo msomaji wangu ninapokuachia swali.

Kadinali Tagle anatukumbusha kwamba Bwana huja kwetu kwa namna ambazo hatuzitarajii. Nabii Eliya alimtazamia Mungu katika upepo, tetemeko la ardhi na moto, lakini Mungu alijidhihirisha katika sauti ndogo na tulivu.

Padri Evarist Mwaudama naye anatukumbusha umuhimu wa ukimya, akisema kwamba Mungu anapatikana katika ukimya na kwamba tunapokumbwa na mawimbi ya maisha, tunapaswa kurudi kwa Yesu wa Ekaristi.

Na Mwanakwetu?

Anatembea kwenda Misa, anakutana na familia ya waamini, mmoja wao anapata lifti ya bodaboda, anaingia kanisani akiwa amechelewa, anasikia Injili na mahubiri, njiani akielekea kanisani anakutana na swali ambalo hana jibu lake.

 

Labda hapa ndipo ukimya wa Mungu unapokutana na makelele ya maisha yetu.

Labda katika maswali ambayo hatuna majibu yake, katika watu tunaowatafuta, katika hofu zetu, katika maumivu yetu na hata katika ukimya wetu, Mungu bado yupo.

Kwa sababu kama alivyotukumbusha Kadinali Tagle:

“Bwana anapokuja, tupate kumtambua.”

Na kama alivyotukumbusha Padri Mwaudama:

“Mawimbi yakizidi, rudi kwa Yesu wa Ekaristi.”

 

Mwanakwetu anasema: Tumsifu Yesu Kristo!

Milele amani.

Kumbuka;

“Bwana Atakapokuja Tutamtambua.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257





















 

 

0/Post a Comment/Comments