Adeladius Makwega – MBAGALA
Usiku wa kuamkia Agosti 27, 2026, Mwanakwetu alipokuwa akijiandaa kulala, ghafla macho yake yakatua kwenye taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Asha Rose Migiro, kuhusu uamuzi wa kumvua uanachama aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ambaye alijiuzulu tarehe Agosti 25, 2026.
Taarifa hiyo haikuwa taarifa ya kawaida kwa Mwanakwetu.
Dkt. Nchimbi si mtu aliyekuja kwenye siasa jana kama mgeni anayesubiri kuonyeshwa mlango. Ni mwanasiasa aliyepitia madaraja mengi ndani ya chama na katika uongozi wa nchi; aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, balozi, waziri katika wizara mbalimbali na, kabla ya yote hayo, alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa kwa kipindi kirefu.
Mwanakwetu alipoisoma taarifa hiyo, alikaa kimya.
Akasema moyoni:
“Kumbe siku hizi hata historia inaweza kupigiwa kura na kusomewa hukumu na watu ambao huenda hawakuwepo hata kwenye ukurasa huo wa historia!”
Kwa kweli, hekaheka zinazoendelea ndani ya CCM sasa zilimfanya Mwanakwetu ajisikie hata aibu kujitambulisha hadharani kuwa ni kada wa chama hicho.
Si kwa sababu ameacha kuheshimu siasa.
La hasha!
Bali kwa sababu wakati mwingine siasa zinapogeuka kuwa maigizo, hata mtazamaji anaweza kuanza kujiuliza kama jukwaa bado ni la siasa au limehamia kwenye ukumbi wa vichekesho.
Usiku huo baridi ilikuwa kali.
Mwanakwetu akaamua kujilaza kitandani.
Lakini kabla usingizi haujamchukua, ghafla akamkumbuka marehemu Richard Hiza Tambwe, aliyewahi kuwa Mkuu wa Propaganda wa CCM Taifa.
Mwanakwetu akakumbuka maneno ambayo Richard Hiza Tambwe alimwambia mwaka 2015.
“Wewe mtoto wa Doroth, wewe mtoto wa Mwalimu Doroth, angalia CCM yako inavyowavua watu uanachama. Hebu waangalie! Hivi katika CCM nani mwenye uwezo wa kumjadili Dkt. Nchimbi? Ukada wake ndani ya CCM unaweza kupimwa na kikao gani chenye huo mzani? Ukimtazama Dkt. Nchimbi na hao wanaomjadili, nani ana nuru? Hata Dkt. Nchimbi akiongea, nuru unaiona machoni mwake; nuru unaiona katika paji lake la uso.
Hivi visa ni chuki dhidi ya Edward Lowassa tu, hakuna kingine. Ukimuangalia Emmanuel John Nchimbi, unajua kuwa huyu anapeleka matumaini kwa walio mbele yake.”
Maneno hayo yakamrudia Mwanakwetu usiku huo kama wimbo wa zamani ambao umeufahamu kwa muda mrefu, lakini leo ameamua kuusikiliza kwa masikio mapya.
Kwa wale ambao hawafahamu ujirani wa Mwanakwetu na Richard Hiza Tambwe, ulikuwa ujirani wa miaka mingi.
Kwa muda mrefu, Richard Hiza Tambwe aliishi Mbagala Kizuiani, eneo la Transfoma (Kwamalade), pamoja na mkewe, Mama Tulo au Mama Agness.
Haya ni mambo ya miaka mingi, tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Mama wa Mwanakwetu, Mwalimu Doroth Mlemeta, naye aliishi eneo hilo. Ndiyo maana katika siasa za Wilaya ya Temeke na Mbagala, Richard Hiza Tambwe alimwita Mwanakwetu:
“Mtoto wa Doroth!”
Na jamaa wengine walikuwa wakicheka na kusema:
“Kwa nini asikuite Makwega? Kwa nini anatumia jina la mama yako?”
Lakini Mwanakwetu hakujali.
Kwa sababu wakati mwingine jina unalopewa na watu linaweza kuwa na historia kubwa kuliko jina ulilopewa kwenye cheti cha kuzaliwa.
Kwa hakika, usiku huu nilikumbuka sana yale maneno ya Richard Hiza Tambwe kuhusu nuru. Nikajiuliza:
Hivi wale walioshiriki kikao kilichodai kumvua uanachama Dkt. Emmanuel John Nchimbi walikuwepo wakati tunamchagua kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa?Walijua tulimtoa wapi?Walijua tulipitia njia gani hadi tukamketisha kwenye kile kiti?
Ni wangapi waliokuwapo siku hiyo? Au viongozi wa CCM wa sasa wanadhani waliokuwepo wote wamefariki kama alivyofariki marehemu John Gudinita?
Ni wangapi waliijua historia yake kabla hawajakaa kwenye meza na kuanza kumjadili?Nani huyo aliyetoa wazo hilo?
Mwanakwetu anaamini kwamba huenda baadhi yao walikuwa hawajafika hata kwenye ukumbi wa historia hiyo hata kadi za CCM walikuwa hawana. Inakuwaje walowezi wawafukuze wenyeji?
Na hapa ndipo swali linapokuwa zito:
Unawezaje kumhukumu mtu katika ukurasa wa historia ambao wewe mwenyewe hukuwahi kuusoma? Huwezi!
Unaweza kuwa na cheo. Unaweza kuwa na kikao. Unaweza kuwa na muhuri.Unaweza hata kuwa na kipaza sauti. Lakini si kila mwenye kipaza sauti ana nuru ya kuzungumza kwa niaba ya historia.
Mwanakwetu nikajisemea moyoni:
Hakuna mtu anayeweza kumvua uanachama Dkt. Nchimbi katika maana ambayo historia yake imejengwa na safari yake ya kisiasa. Na labda niwaambie jambo moja kwa lugha rahisi.
Labda anayeweza kumvua viatu Dkt. Emmanuel Nchimbi ni mlango wa msikiti wakati anaingia msikitini. Labda anayeweza kumvua kofia ni mlango wa kanisa wakati anaingia kanisani. Na kama ni suala la mkaanda wa suruali yake, basi huyo anayeweza kuuvua ni mkewe!
Lakini linapokuja suala la nuru ya historia yake, mchango wake na safari yake ya kisiasa, hapo mambo yanakuwa tofauti.
Huwezi kuzima jua kwa kulifungia kwenye bahasha. Huwezi kuufuta mchana kwa kutangaza kuwa usiku umeingia.
Na huwezi kumvua mtu nuru yake kwa kikao cha watu waliokaa gizani wakiamini kwamba taa imezimika kwa sababu wao hawaioni.
Asiye na nuru hawezi kumvua chochote mwenye nuru.
Mwanakwetu anasema:
Dkt. Emmanuel John Nchimbi bado ni Mwana CCM.Na kama kuna mtu anabisha, basi abishe na historia. Maana historia haina hofu ya kikao.Historia haiogopi kura.Historia haiogopi vyeo.Historia haigopi mahabusu na historia haigopi mtutu wa bunduki.Na zaidi ya yote, historia haiwezi kufutwa kwa kalamu ya siku moja.
Mwanakwetu, upo?
Kama upo, basi kumbuka maneno haya:
“ASIYE NA NURU HAWEZI KUMVUA CHOCHOTE MWENYE NURU.”
Na kwa wale wanaodhani wamezima taa, huenda wakaja kugundua kwamba walikuwa wamezima tu kibatari chao—wakati jua bado linachomoza.
Nakutakia siku njema.
📞 0717649257
.gif)




.gif)
Post a Comment