ATI HAWEZI KUIONA PEPO?

 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Haiwezekani katika kozi yetu, darasa lililosajili karibu wanafunzi 300, dropout iwe zaidi ya 100. Hili ni haki? Mimi najua shida kubwa ni umaskini. Maana mtu anapewa mkopo wa laki saba, wakati ada ya chuo ni shilingi milioni moja na nusu. Hiyo laki nane anaitoa wapi?”

 

Yaani sisi Watanzania tumejaa vituko mno!

 

“Mara baada ya dropout hiyo, hakuna anayefuatilia kilichotokea, wala kushangaa na kuuliza sababu ni nini. Mimi nawaomba wafuatilie. Kama hoja ni kukosa laki nane ya karo, basi chuo si cha serikali; mwanachuo aendelee na masomo, kisha baadaye atalipa. Kama atashindwa, basi siku akija kuchukua cheti atalipa deni hilo.”

 

Mwanakwetu yupo ndani ya basi, anayasikiliza madai haya.

 

Akawa anasikiliza kwa umakini mkubwa hoja hizo.

 

Kisha akasikia:

 

“Unajua hawa maprofesa wengi hawawezi kwenda mbinguni.”

 

Mwanakwetu, akilini mwake, akajiuliza: Duuu! Tumefika huko? Naona jamii inamsaidia Mungu kazi ya kuhukumu!

 

Vipi wasomi mahiri kama Profesa Issa Shivji? Vipi Waziri Profesa Paramagamba Kabudi? Vipi maprofesa wangu walionisomesha mimi? Kweli mbingu wataikosa?

 

Kichwa cha Mwanakwetu kikauma mno.

 

Mmoja wa vijana akaendelea:

 

“Kwa mfano, Profesa Mkenda, yeye ni waziri. Angefuatilia hili, maana kila chuo kikuu kama kilipokea wanafunzi 500 mwaka wa kwanza, ajiulize: dropout zipo ngapi? Na kwa nini katika kila jina? Hoja zitolewe. Hili nalo sina hakika kama huwa wanafanya uchunguzi.”

 

Mwanakwetu moyoni akasema, Lo! Salale! Sasa inamaanisha hata Profesa Adolf Mkenda peponi hakanyagi?

 

Mwanakwetu hana majibu. Anataka kuuliza, lakini vijana hao wako mbele yake na wanaongea kwa ukali mno.

 

Akajisemea mwenyewe:

 

“Hebu ngoja nijiulize mimi mwenyewe. Hivi na mimi nitaiona pepo?”

 

Wale vijana wakafika kituo kimoja na kushuka. Wakaanza kugombana na kondakta kuhusu nauli. Neno lao la mwisho likawa:

“Sisi wanachuo hatuna pesa, kaka. Pesa yenyewe tunayopewa ni kidogo tu. Hapa tunakwenda field, na wewe kondakta ukiendelea hivi, hata wewe huwezi kuziona mbingu! Tupe chenji yetu. Tutakulaani? Sasa nasema na wewe, kondakta, na dereva wako hamuwezi kuziona pepo. Nyinyi mbingu mtaishia kuzisikia masikioni mwenu tu hapa duniani.”

 

Lahaula la kwata!

Maneno hayo:

 

“Huwezi kuziona mbingu; mbingu utazisikia hapa hapa duniani tu.”

 

Maneno haya yalimpa burudani kubwa Mwanakwetu. Huku akicheka, akaendelea na safari hadi mahali fulani, akashuka na kuendelea na safari yake—madongo poromoka!

 

Kisha alipofika huko ndipo akaamua kuyaandika makala haya kama yalivyo.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu alikuwa mwalimu katika shule za msingi na sekondari nchini Tanzania kipindi kile cha MEMKWA na MESS, ambapo walimu walihakikisha watoto wote waliokuwa na umri wa kwenda shule walisakwa na kupelekwa shuleni, iwe msingi au sekondari, huku miundombinu ikijengwa vizuri.

 

Hata kundi la wasichana walioacha shule ili kuwa mabinti wa kazi, wazazi wao walisakwa na kuhakikisha mabinti hao wanarejeshwa nyumbani na kisha shuleni ili waendelee na masomo.

 

Kwa sasa, makundi yale ya MESS na MEMKWA ndiyo yapo vyuoni, na wengine tayari wamemaliza.

 

Mwanakwetu anashauri haya

Ni vizuri kufanyika uchunguzi haraka sana kuhusu idadi ya wanachuo walioacha vyuo au kufeli katika kila taasisi ya elimu ya juu nchini Tanzania kwa mwaka wa masomo 2025/2026 idadi ifahamike, uchambuzi ufanyike haraka maana kisa hiki ni kengele ya hatari juu ya elimu yetu.

 

Kisa cha wanafunzi hawa wa chuo kikuu ni muhimu kuangaliwa kwa kina. Kiwe pia kengele ya hatari kwa vyombo vya ushauri vya mamlaka ya uteuzi za Wizara ya Elimu na Katibu Mkuu wa Wizara husika, ili kuwa na kiu ya kujua hali ilivyo katika taasisi zetu za elimu mwaka mmoja baada ya wanafunzi kudahiliwa chuoni.

 

Ufuatiliaji huo unaweza kuongeza umakini katika malezi na ustawi wa vijana wetu, kuanzia ngazi ya chuo kikuu hadi kwa wazazi na walezi, TCU, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Wizara husika.

 

Mwanakwetu anashauri utafiti mdogo ufanyike ili kupata taarifa halisi za hali ilivyo nchi nzima na kujua ukubwa halisi wa tatizo kama lipo.

 

Na kama ni kweli wale wanafunzi ambao wameacha vyuo kutokana na changamoto mbalimbali, nashauri waelekezwe kuripoti katika ofisi za Wakuu wa Wilaya, kisha wasaidiwe kurejea vyuoni haraka.

 

Hili ni kundi muhimu sana, na changamoto zao zinapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka. Wanaweza kurejeshwa chuoni kwa utaratibu maalumu wakati wenzao wakiwa likizo.

 

Kuhusu suala hili la mtu yeyote “kuiona mbingu”, Mwanakwetu analiacha kama lilivyo.

Mungu mwenyewe ndiye atakayeamua.

 

Maana hata Mwanakwetu yupo katika jitihada za kuitafuta mbingu. Hoja hii imebakizwa kama ilivyo katika makala haya ili kuupa uhai zaidi mjadala kuhusu elimu ya vyuo vikuu na mustakabali wa vijana wetu maana Mwanakwetu kama mzazi limemgusa.

 

Mwanakwetu, upo? Kumbuka:

“ATI HAWEZI KUIONA MBINGU.”

Nakutakia siku njema.


✉️ makwadeladius@gmail.com


📞 0717649257

 


















0/Post a Comment/Comments