ZIWA VICTORIA NALIHAMISHIA MBAGALA

 

Adeladius Makwega – Musoma & Bunda, Mara, Tanzania.

 

Julai 4, 2026 ilianza kwa taswira ya kipekee: safari ya wanahabari waliokuwa katika ziara ya Waziri Mkuu, wakitoka Musoma Mjini kuelekea Musoma Vijijini—safari iliyobeba simulizi, uchunguzi na tafakuri nzito juu ya maisha ya wananchi.

 

Kwa mujibu wa utafiti wa Mwanakwetu, ilibainika kuwa kulikuwa na makundi matatu ya wanahabari: kwanza, wale waliokuwa na Waziri Mkuu kutoka Dodoma; pili, wanahabari wenyeji kutoka Mara; na ndani yake, wanahabari waliokuwa wanahudumu moja kwa moja katika maeneo husika ya majimbo ya uchaguzi.

 

Kundi la wanahabari kutoka Musoma Mjini walifika Musoma Vijijini katika eneo la mradi uliokuwa unafunguliwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba.

 

Hapa ilikuwa katika Kijiji cha Ujamaa Kasoma, kilicho jirani kabisa na ukingo wa Ziwa Victoria—ziwa kubwa, lakini simulizi yake siku hiyo ilikuwa ndogo kuliko matarajio ya walioishi kando yake. Wanahabari hawa walipofika waliamua kwanza kutafuta kifungua kinywa. Walifika mahali palipo na maduka na mikahawa majira ya saa moja na nusu asubuhi, na safari ya habari ikaanza kwa kikombe cha chai.

 

“Nilifika katika mkahawa mmoja unaoendeshwa na Mama Loveness na kuagiza chai na wali. Hili lilifanyika ili mwili wangu uwe na nguvu, maana kupata nafasi ya kula katika ziara za viongozi ni ngumu; nikila wali au ugali, mambo yanakuwa mazuri hadi jua linazama, labda nitakunywa maji na soda ili kukazia siku. Nilipouliza kuna nini, Mama Loveness alisema wali upo, lakini tatizo ni mboga.

 

‘Hapa mboga niliyonayo ni maharage tu, maana samaki na dagaa hatuendi ziwani kwa wiki ya pili sasa, kutokana na madai ya uvuvi haramu; hapa kuna zuio la kuvua kwa sasa.’

 

Mimi niliomba wali na maharage. Mama Loveness alinipa wali na maharage huku nikimnanga, ‘Mbona mnanipa maharage kidogo? Nyie Wajita na Wakwaya mna shida gani? Ndivyo mnavyowapa wanaume zenu mboga kidogo?’

(Mama Loveness akawa anacheka tu.)

 

Niliendelea kuongea, ‘Wewe Mama Loveness, wiki mbili tu mmezuiwa kuvua samaki, hamna hata dagaa za wageni! Majumbani kwenu hakuna hata dagaa wa akiba? Kama hili halitoshi, basi mgekuwa hata na fulu (hawa ni dagaa wa hadhi ya chini ambao inadaiwa walipandikizwa Ziwa Victoria ili wawe chakula cha samaki wengine, na mtu anayekula fulu huonekana kuwa fukara wa mwisho).’

Niliendelea kuongea na mama huyu, ‘Yaani hapa, Mama Loveness, huna samaki, huna dagaa na hata fulu huna? Wenzenu Wagogo, mvua hunyesha mara moja tu kwa mwaka, yaani masika hadi masika, lakini msimu wa kiangazi ambao ni mrefu, kila nyumba ya mama wa Kigogo utakutana na mboga za majani zilizoanikwa na kukausha vizuri, na kuwekwa katika mitungi na vibuyu pamoja na mafuta ya samli.’

 

Mama Loveness alijibu kuwa kwa sasa kupata samaki ni gharama; labda dagaa wachache kwa bei nafuu, tena Musoma Mjini, siyo huku vijijini.

 

Kweli, hadi tamati nilikula wali na maharage, japokuwa nilikuwa hatua chache tu kutoka ukingo wa Ziwa Victoria—mahali ambapo ungetarajia wingi wa samaki, lakini ukweli ukawa tofauti.

 

‘Hili Ziwa Victoria itabidi tulihamishie kwetu Mbagala.’

 

Mama Loveness akawa anacheka huku akiuliza, ‘Sasa wewe, baba Mswahili, kwenu Mbagala au Dodoma?’

Nikamjibu, ‘Mimi kwetu ni Mbagala, na pia kwetu ni Dodoma.’”

 

Kutoka mkahawani, wanahabari walirejea katika eneo la mradi ambapo Jengo la Utawala la Shule ya Msingi Kasoma lilifunguliwa na Waziri Mkuu—ishara ya maendeleo, lakini pia kivuli cha changamoto kinabaki.

 

Msafara wa Waziri Mkuu uliendelea hadi Suguti, ambako mkutano wa hadhara ulifanyika.

 

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu, Suguti ni eneo alikozaliwa Antony Mtaka, kiongozi aliyewahi kuhudumu katika mikoa kadhaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Hapa ndipo wananchi walipozungumza—kwa ujasiri na weledi. Hoja zao zilijikita zaidi katika madini ya dhahabu, rasilimali iliyopo Musoma Vijijini, lakini yenye maswali mengi kuliko majibu. Changamoto kubwa ilikuwa madhara ya uchimbaji na namna wananchi wanavyonufaika na utajiri huo.

 

Katika maeneo yote aliyopita Waziri Mkuu, malalamiko yalitolewa dhidi ya watu mbalimbali. Lakini Suguti kulikuwa na tukio la kipekee: diwani mmoja alilalamikiwa na mama mmoja kutoka Geita kuhusu mgogoro wa fedha za uchimbaji wa dhahabu.

 

Diwani alisimama hadharani na kukiri kupokea shilingi milioni 10, akisema alirudisha sehemu ya fedha hizo. Aliahidi kukamilisha kurejesha fedha zote ndani ya mwezi mmoja—ahadi iliyosikika kama ushindi mdogo wa haki.

 

“Mheshimiwa Diwani, umeonesha uungwana mkubwa kwa kukiri hili jambo; kwa kukiri kuwa mzee huyu alikulea. Nakushukuru sana, na hata wananchi wa kata unayotoka, nawaombeni endeleeni kumchagua,” alisema Waziri Mkuu.

 

Baadaye, Waziri Mkuu alielekea Bunda Mjini ambako alifanya mkutano wa hadhara. Hapa, siasa zilichukua nafasi yake. Alitumia muda mwingi kulizungumzia suala la Mheshimiwa Easter Bulaya, akisisitiza kuwa bado ni mwana CCM na wananchi wanapaswa kumuamini. Alikumbusha kuwa hata mwaka 2020, watia nia wengi walioshinda kura za maoni hawakurudishwa majina yao—akitoa muktadha wa maamuzi ya chama.

 

Baadaye, Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake ya Mkoa wa Mara.

Mwanakwetu anasema nini leo?

 

Taswira ya siasa ya Bunda ilionesha hali ya mashaka, kiasi cha Waziri Mkuu kutoa maagizo hadharani kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. Ilionekana wazi kuwa viongozi wa kitaifa wanajaribu kuwashawishi wananchi kuwaamini wabunge hawa.

 

Ikumbukwe kuwa Easter Matiko na Easter Bulaya walikuwa miongoni mwa wabunge 18 wa CHADEMA walioingia Bungeni mwaka wa 2020 katika muktadha tata wa kisiasa.

 

Katika mkutano huo, mwandishi alishuhudia tukio la kawaida lakini lenye ujumbe: alipatwa na usingizi, akaangusha simu, na alipoamka akasikia sauti kutoka nyuma yake:

 

“Sisi ni wana CCM, Easter Bulaya na hata Easter Matiko ni dada zetu wa damu; hivi nani anaweza kuja hapa mbele akaanza kunielezea habari ya tabia njema ya dada yangu—alivyo mwema—zaidi ya mimi kaka yake? Hawa ni ndugu zetu; lazima wajitathmini, na huu mgogoro upo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); sisi wanachama tunalalamika.”

 

Hapo ndipo kiini cha mjadala kilipo: ndani au nje ya chama? Uwajibikaji au ulinzi wa kisiasa?

 

Wapo wanaoamini kuwa wakubwa ndani ya CCM walikosea—na kama ni kweli, basi swali linabaki: kwa nini ni vigumu kukiri hadharani?

 

Mwanakwetu anajiuliza: kama kuna hitilafu hii, je, nani anaweza kuitatua?

Na zaidi ya hapo, jambo la pili linaibuka—utamaduni wa usuluhishi. Mama kutoka Geita anasafiri hadi Musoma Vijijini kudai haki yake ya shilingi milioni 10. Je, hii si ishara kuwa wananchi wanatafuta haki nje ya mifumo rasmi?

 

Je, Mahakama ya Tanzania inajifunza nini? Je, inaaminika? Je, bado ni kimbilio la wananchi? Na je, historia—kama ule uamuzi wa kuufuta uchifu mwaka 1962—inaendelea kuathiri namna tunavyotatua migogoro leo?

 

Kwa hakika, haya ni zaidi ya simulizi; ni kioo cha jamii.

 

Haya ni makala ya muhtasari wa siku ya mwisho ya ziara ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, mkoani Mara, Julai 4, 2026.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:


“Ziwa Victoria nalihamishia Mbagala.”

Nakutakia siku njema.

Mawasiliano:
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257











 








 





0/Post a Comment/Comments