ZIARA ZA VIONGOZI: KAMBI ZA JANDO NA UNYAGO?

 



Adeladius Makwega, Mbagala

 

Aprili 4, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, amehitimisha ziara yake ya siku kadhaa wilayani Bunda, ambayo alianza pale wilayani Serengeti, mkoani Mara, Julai 1, 2026.

Katika ziara hii, mambo kadhaa yamefanyika, ikiwamo kero mbalimbali kupewa nafasi ya kupazwa sauti mbele ya kiongozi huyu na mbele ya umma wa Watanzania.

 

Mwanakwetu, kwa muda wote, alikuwa akifuatilia ziara hii hatua kwa hatua kwa jicho makini, huku kukiwa na mambo kadhaa aliyoyabaini.

 

Mojawapo ya mambo aliyoyaona Mwanakwetu ni kuwa tangu awali, viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifanya ziara katika maeneo kadhaa ya taifa hili, lakini kumeonekana hakuna ufuatiliaji wa kero zinazotolewa na wananchi baada ya kusikilizwa.

 

 

“Mhe. Waziri Mkuu, jambo hili pia nililisema kwa Waziri Mkuu aliyekutangulia, lakini halikufanyiwa kazi…”

 

Masikio ya Mheshimiwa Mwigulu Nchemba yalikumbana na sentensi hiyo.

 

Wapo wanaoamini kuwa mambo ni yale yale, kwa kuwa hata kama jambo liliwasilishwa kwa Waziri Mkuu aliyetangulia, Ofisi ya Waziri Mkuu siyo kambi ya jando na unyago iliyojengwa kwa majani mabichi kuwahifadhi vijana walio kambini kwa siku chache tu, ambapo zoezi la tohara likimalizika, kambi inavunjwa.

 

Kwa hakika, hii ni ofisi yenye muendelezo wa watumishi na nyaraka tele. Mwanakwetu anaamini kuwa wale wote wanaoambatana na Waziri Mkuu kutoka Dodoma wanawajibika kuyafanyia kazi mambo yote yaliyotajwa katika malalamiko.

Kwa kutazama, yapo mambo ambayo yanaingia katika sekta kadhaa na wizara nyingine tele, ambapo Waziri Mkuu anaweza kuhoji popote na kuagiza utekelezaji wake kwa mamlaka yake, ambapo ngazi ya mikoa ni vigumu kuhoji.

 

Katika ziara hizi za Waziri Mkuu, wapo wanaohoji kuwa inawezekana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba mwenyewe anatumia ziara hizi kujijengea umaarufu wa kisiasa kutokana na hali ya sasa ya siasa za Tanzania zilivyo njia panda.

 

Hili Mwanakwetu hawezi kulikataa, maana historia ya Tanzania inadokeza kuwa Mawaziri Wakuu wengi, hata walipomaliza majukumu yao ya Uwaziri Mkuu, ndoto za Urais ziliibuka. Mathalani, mwaka 1995, John Samuel Malecela na Cleopa David Msuya waliingiza majina katika mchakato huo. Hata miaka iliyofuata, Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda, shauku zao za kuutaka urais zilionekana kwa kuchukua fomu za kutia nia kwa nafasi hiyo.

 

Katika hili, ndugu yangu Mheshimiwa Kassim Majaliwa hayumo, na pengine hii inatokana na mizengwe ya CCM kupitisha jina la mgombea urais mapema mwaka 2025; vinginevyo, Kassim Majaliwa huyu Mmakonde wa Kusini mwa Tanzania angekuwa mmoja wao.

 

Mwanakwetu anaamini kuwa Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba hawezi kukwepa hili.

 

Jambo la kushtua ni moja tu: je, Marais wanapokuwa wanafanya kazi na Mawaziri Wakuu wao, wanaongea nini?

 

Mwanakwetu anaamini kuwa inawezekana kukawa na unafiki na hata kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa, kuwa:

 

“Wewe chukua fomu za Urais, nipo na wewe ili kuyakamilisha mambo tuliyoyaanza na wewe.”

 

Haya yanaweza kuwa hivyo kutokana na hoja kuwa haiwezekani Waziri Mkuu achukue fomu ya kutia nia katika chama cha siasa, kisha jina la mhusika likatwe. Maana yake, wewe Rais na Waziri wako Mkuu hamkufanya kitu. Kibaya zaidi ni pale ambapo hata Makamu wa Rais anaonekana anachukua fomu ya Urais, kisha waziri wa kawaida anapitishwa—hiki ni kichekesho.

 

Mwanakwetu anaona kuwa inawezekana kukawa na unafiki miongoni mwa viongozi wakuu kwa kuambiana mambo ambayo siyo ya kweli. Hili linafanyika ili Waziri Mkuu afanye kazi kwa ari kubwa, akitambua kuwa Rais anamuunga mkono, na hivyo kutafuta kuungwa mkono kwa wananchi. Hapa ndipo hoja za ziara tele zinaibuka.

 

Mwanakwetu, katika makala haya, anaamini kuwa hoja ya ziara za viongozi wakuu kitaifa ni muhimu sana, ili waende mashinani, kuwapa nguvu viongozi wa ngazi ya mikoa, wilaya, halmashauri, majimbo, tarafa, kata, vijiji na mitaa, na pia kuona hali halisi ya maisha ya wananchi.

 

Katika ziara hizo, ni vizuri viongozi wote wa ngazi za juu—Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu (pamoja na Naibu Waziri Mkuu)—wakawa wanafanya ziara nchi nzima kwa wakati mmoja, ili kutoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao, huku wakiwapa nguvu viongozi wa mashinani, siyo kwenda kuwatisha, kuwatimua na kuwatumbua; hoja iwe kuwaongezea nguvu.

 

Kwa hoja ya viongozi hao, na kama ziarani yupo Naibu Waziri Mkuu, kunakuwa na viongozi wa ngazi za juu wengine wanne wakigawana mikoa mingine. Hapo, baada ya muda mfupi, nchi nzima inakuwa imepata nafasi ya kusikilizwa, na zoezi hili linaweza kufanyika kila mwezi wa tatu wa robo ya mwaka.

Kero zinasikilizwa, zinatatuliwa na kumbukumbu zinakusanywa vizuri. Hapa maagizo yote yanafuatiliwa, na kila jambo, kwa kumbukumbu, ndani ya miezi miwili liwe limefanyika. Viongozi wakuu wakienda katika ziara ya robo ya pili, wanakuwa na nyaraka za kero na maagizo yaliyopita katika eneo husika. Mathalani, kama Mkoa wa Tanga alienda Naibu Waziri Mkuu wakati wa robo ya kwanza, basi katika robo ya pili anaweza kwenda Waziri Mkuu; au kama alikwenda Rais wa Zanzibar robo ya kwanza, basi robo ya pili anakwenda Rais wa Jamhuri ya Muungano.

 

Hapa, Rais wa Zanzibar, kwa kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri, atekeleze majukumu katika ziara hizi bila kujali anatoka upande upi, na pia hapa ndipo unaibuka umuhimu wa nafasi ya Naibu Waziri Mkuu.

 

Kama hili litafanyika vizuri, jamii ya Watanzania itakuwa na nafasi ya kuwapima hawa viongozi—tangu Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na hata Naibu Waziri Mkuu—namna wanavyofanya kazi na uwezo wao wa kushughulikia mambo ya taifa hili.

Kama hili linafanyika, viongozi wababaishaji, matapeli na mawakala wa baadhi ya watu hawawezi kupenya.

 

Mwanakwetu, upo?

Leo hii, msomaji wangu, nilitamani kutafakari na wewe haya yaliyomo katika makala haya kutokana na ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Julai 1–4, 2026, mkoani Mara.

 

Vinginevyo, ziara za viongozi zitakuwa sawa na kambi za jando na unyago.

 

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257










 

 

0/Post a Comment/Comments