WANANCHI KAMA HAWAMTAKI RAIS WANAFANYAJE?

 



Adeladius Makwega – Mbagala

 

Julai 7, 2026 ilikuwa ni siku iliyopangwa kwa maandamano ya amani, ambayo vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania viliyaharamisha (viliyapiga marufuku maandamano haya kwa sababu wanazozifahamu wao).

Mwanakwetu, siku hii, alifanya mawasiliano na jamaa zake kadhaa tangu saa 12 ya asubuhi hadi saa sita mchana, ambapo kwa maeneo ya Dar es Salaam na maeneo mengi ya Tanzania ilionekana kulikuwa na hali ya usalama.

 

“Yaani nimepita pale Kimara naenda kazini; pale ni polisi, wanajeshi na magari yao ya kutisha mengi. Hivi Tanzania tutaishi hivi hadi lini? Nipo kazini, ngoja nikanunue vitafunio ninywe chai yangu, nitakupigia simu baadaye.”

 

Haya ni maneno ambayo Mwanakwetu aliyasikia kutoka kwa mdau mmoja aliyeongea naye.

 

Mwanakwetu aliachana na ndugu huyo huku hoja ya kwenda kununua vitafunio na kunywa chai ikamtia hamu na yeye kwenda kunywa chai katika mkahawa mmoja. Akiwa hapo, akanywa chai, wali, dagaa na maharage, kisha akalipa shilingi 10,000 na kurudishiwa shilingi 8,000: noti tatu za shilingi 1,000 na noti moja ya shilingi 5,000. Baada ya hapo akaenda kuweka muda wa maongezi kwenye simu yake.

 

Njiani kulikuwa na bodaboda wengi wamepaki wakisubiri abiria. Vijana wale walikuwa wanalalamika kuwa wateja hawapo.

 

Kijana mmoja akauliza,

“Hivi kama sisi wananchi hatumtaki Rais, tunafanyaje?”

 

Mwanakwetu akafika dukani, akatoa noti ya shilingi 5,000 ili awekewe muda wa maongezi, huku wale vijana wa bodaboda wakiendelea kujiuliza maswali na kujibizana.

Mwanakwetu akaitaja namba 0665887831. Kijana wa dukani akasoma jina likatokea “MAGRETH.” Mwanakwetu akasema hapana. Kijana akaanza tena kutuma pesa; Mwanakwetu akaitaja tena namba ileile. Kijana akasema jina “Francis Makwega,” kisha akarudi akasema “Adeodatus, nimepatia kulitamka au nimekosea?” Mwanakwetu akacheka kisha akasema, “Linatakwa ADELADIUS.”

Mwanakwetu alikuwa anapata huduma dukani, lakini akili yake ilikuwa katika mjadala wa wale vijana wa bodaboda.

 

Kijana mmoja akasema,

“Unapoteza muda kutuuliza sisi, muulize ChatGPT, atakupa majibu.”

 

Mwanakwetu anawekewa muda wa maongezi.

Kwa wale vijana wa bodaboda, maneno haya yanasikika:

“ChatGPT anasema:

Kwa Tanzania, kuna taratibu za kikatiba na kidemokrasia zinazoweza kufuatwa ikiwa wananchi hawaridhiki na Rais:

 

Mosi, uchaguzi mkuu — Wananchi wanaweza kutumia haki yao ya kupiga kura kumchagua kiongozi mwingine katika uchaguzi ujao. Hili hufanyika kila baada ya miaka mitano.”

 

Vijana wale wakajibu,

 

“Hili hapana.”

 

“Pili, uwajibikaji kupitia Bunge — Bunge lina mamlaka ya kuisimamia serikali. Kwa hali maalum, linaweza kuanzisha mchakato wa kumwondoa Rais madarakani (impeachment) ikiwa kuna ukiukwaji mkubwa wa Katiba au sheria.”


(Vijana Wakajibu: “Hili wabunge wetu hawawezi.”)

 

“Tatu, mahakama — Masuala ya kikatiba yanaweza kupelekwa mahakamani ikiwa kuna madai ya kuvunjwa kwa Katiba au sheria.”


(Vijana Wakajibu: “Kwa mahakama za Bongo, uwongo; labda mahakama za Jamhuri ya Kenya.”)

 

“Nne, maoni ya umma na maandamano ya amani — Wananchi wanaweza kueleza kutoridhika kwao kupitia njia za amani na zinazofuata sheria, kama vile maandamano ya amani au kutoa maoni yao hadharani.”


(Vijana Wakajibu: “Mbona haya maandamano wameyaharamisha? Hao wote ni wale wale.”)

 

“Ni muhimu kufuata njia za kisheria na za amani ili kudumisha utulivu na demokrasia.”

 

Mwanakwetu akawekewa muda wa maongezi, kisha akamuuliza kijana wa dukani, “Hivi, una njugu mawe?” Kijana akajibu hana. Mama mmoja kando alitabasamu kusikia Mwanakwetu anaulizia njugu mawe akihisi Mwanakwetu hajui kupika kande.

 

Hapo ChatGPT alikuwa amemaliza kujibu, na Mwanakwetu akarudi nyumbani kwake, akaamua kuyaweka haya yote katika makala haya.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kumbuka, haya ni makala ya muhtasari wa hali ilivyokuwa tangu asubuhi ya Julai 7, 2026 hadi saa sita mchana, kama ilivyokusanywa na Mwanakwetu.

 

Mwanakwetu, upo?

 

Kumbuka:

 

“Hivi wananchi, kama hatumtaki Rais, Wanafanyaje?”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257












 

0/Post a Comment/Comments