Adeladius Makwega – Serengeti, Mara, Tanzania
Wakulima wa Mkoa wa Mara wametakiwa kuzingatia kalenda za mazao ya biashara, hususan zao la tumbaku, ili kuongeza tija, kuboresha kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa Julai 10, 2026, wilayani Serengeti na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mheshimiwa Alfa Haule, alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, katika mkutano wa WAMACU unaowakutanisha wadau wa zao la tumbaku mkoani hapa.
Akizungumza katika mkutano huo, mheshimiwa Haule alisisitiza kuwa sekta ya kilimo ni mhimili muhimu wa uchumi, unaogusa moja kwa moja maisha ya wananchi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taifa.
“Sekta ya kilimo ni chanzo kikubwa cha mapato. Ina uwezo wa kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja, kaya, kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla. Ni wajibu wa wananchi kuongeza juhudi katika sekta hii huku serikali ikiendelea kuwapa ushirikiano,” alisema Haule.
Aidha, aliwataka wakulima kuzingatia miongozo ya kilimo na kufuata ratiba rasmi za uzalishaji na uuzaji wa mazao ili kuepuka hasara pamoja na vitendo vya utoroshaji wa mazao.
“Naomba kwa hisani yenu, wana WAMACU wote na wakulima kwa ujumla, muhakikishe mnafuata miongozo ya kilimo cha tumbaku na mazao mengine, ikiwamo kalenda za mazao hayo. Hii itasaidia kupata tija na kuzuia waharifu wanaotorosha mazao,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Bi. Angelina Marko, alieleza changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, akibainisha kuwa baadhi ya vyama vya ushirika vimepokea fedha lakini havijawalipa wakulima kutokana na madeni waliyonayo katika taasisi za kifedha.
“Ni muhimu vyama vya msingi kuhakikisha vinawalipa wakulima kwa wakati ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima na kurejesha imani ya wakulima kwa vyama vyao,” alisema mheshimiwa Marko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAMACU, ndugu Mwamanyi Range, aliipongeza Bodi ya Tumbaku kwa kusogeza huduma karibu na wakulima wa Mara, hatua iliyopunguza umbali wa kupata huduma hizo kutoka Tabora hadi Serengeti.
“Awali huduma hizi zilipatikana Tabora umbali wa takribani kilomita 550. Sasa zipo hapa Serengeti, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima wetu,” alisema Range.
Akihamasisha wakulima kuongeza juhudi katika kilimo cha tumbaku, Range alieleza kuwa Mkoa wa Mara una uwezo mkubwa wa uzalishaji lakini bado haujatumika kikamilifu.
“Kwa nini Tabora inatajwa kuwa kinara wa tumbaku wakati Tarime kila zao linamea vizuri? Ni wakati wa wana Mara kuamka, kujituma na kutumia fursa hii ipasavyo chini ya WAMACU,” alisisitiza.
Naye Meneja wa Mkoa wa Tumbaku Serengeti, Sostenese Kikwelele, alisema kuwa Bodi ya Tumbaku imefungua ofisi wilayani humo ili kuongeza uzalishaji na kusogeza huduma karibu na wakulima.
“Lengo letu ni kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni tatu hadi kufikia milioni kumi. Hii inawezekana iwapo wadau wote katika mnyororo wa thamani ya tumbaku watashirikiana kwa karibu,” alisema Kikwelele.
Kwa mujibu wa takwimu, hadi mapema Julai 2026, Mkoa wa Tumbaku Serengeti unazalisha kilo 2,650,846 za tumbaku, huku matarajio yakiwa kufikia kilo 10,526,758 ifikapo mwaka 2030.
Kwa mawasiliano:
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257
.gif)

















.gif)
Post a Comment