UKWELI KWANZA KATIBA MPYA BAADAYE

 


Katiba Mpya Siyo Baba Huyo Katoka Ruanda na Mkungu wa ndizi 




ADELADIUS MAKWEGA – MBAGALA

 

“Mwalimu, shikamoo! Vipi Musoma, kwema? Umemsikiliza Makamu wa Rais? Je, Katiba Mpya itaweza kweli kubadilisha upepo wa kisiasa nchini?”

 

Haya si maswali mepesi. Ni maswali yanayobeba uzito wa taifa. Ni maswali yanayogusa kiini cha uongozi, haki na mustakabali wa Tanzania. Na yalipotamkwa na Mtweve Kayanda—mwanafunzi wa zamani wa Mwanakwetu—yalikuwa si salamu tu, bali ni kilio cha kizazi kinachotaka majibu.

Ni kizazi kilichochoka kusubiri.

Ni kizazi kinachotaka mabadiliko ya kweli.

 

Mwanakwetu aliposikia maneno hayo, hakuyachukulia kama mazungumzo ya kawaida. Alitambua kuwa huu ni mjadala mpana zaidi—mjadala wa mustakabali wa taifa. Mjadala wa Katiba. Mjadala wa haki.

 

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Ibara ya 47–50), Makamu wa Rais si kiongozi wa kupamba jukwaa. Ni mhimili wa dola. Ni msaidizi mkuu wa Rais. Ni daraja la Muungano. Ni kiongozi anayeweza kushika usukani wa taifa wakati wowote.

 

Na si hilo tu—amepewa dhamana ya kusimamia Muungano na Mazingira. Haya si majukumu ya kawaida. Haya ni maeneo nyeti yanayogusa uhai wa taifa—umoja wake na uendelevu wake.

 

Ndipo tunaposikia kauli ya Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, akisisitiza umuhimu wa Katiba Mpya.

 

Je, hii ni kauli ya kisiasa ya kupita? Au ni sauti ya mfumo unaotambua kuwa umefika mwisho wake?

 

Mwanakwetu alijibu bila kuyumba:

 

“Hii si kauli ya kubahatisha. Hii ni ishara. Ni ujumbe kutoka ndani ya mfumo wenyewe kwamba kuna hitaji la mabadiliko ya kimsingi. Katiba Mpya si anasa—ni takwa la lazima la kihistoria.”

 

Lakini hapa ndipo mjadala unakuwa mzito zaidi.

Je, tunaweza kujenga Katiba Mpya juu ya msingi uliojaa majeraha?

Je, tunaweza kuandika mustakabali mpya huku tukifumbia macho yaliyopita?

 

Mwanakwetu anasema—hapana.

Anasema wazi, kwa sauti isiyotikiswa:

Hakuna Katiba Mpya bila haki. Hakuna mageuzi bila uwajibikaji.

 

Na anataja masharti ya msingi:

Mosi, ukweli kuhusu mauaji ya raia tangu mwaka 2015 lazima ujulikane. Waliotoa amri, waliotekeleza, na waliolinda uovu huo—wawajibishwe. Taifa haliwezi kuendelea juu ya damu ya wasio na hatia.

 

Pili, utekaji wa raia lazima uwekwe wazi. Hofu haiwezi kuwa chombo cha utawala. Nchi haiwezi kuwa salama ikiwa raia wake wanaishi kwa wasiwasi.

 

Tatu, waliotekwa na kuuawa wanapaswa kupata haki ya mwisho—ukweli ujulikane. Ni nani aliyepanga? Ni nani aliyefadhili? Kama mali za umma zilitumika, basi wahusika wanapaswa kulipa kwa mali zao zote.

Nne, waliopotea bila maelezo—taifa linadai majibu. Familia zinadai haki. Hii si siasa—hii ni utu.

Na zaidi ya yote, Mwanakwetu ananyoosha kidole kwenye mfumo:

 

Vyombo vya dola haviwezi kuwa juu ya sheria. Viongozi wake lazima wawajibike.

Na wale waliotumia sheria kama silaha ya kisiasa—waliobambikia watu kesi, walioweka vizuizini wapinzani—wanapaswa kuwajibishwa bila huruma.

 

Kisha Mwanakwetu anafunga mjadala kwa maneno yanayogonga moyo wa taifa:

 

“Katiba Mpya si karatasi. Ni mapatano mapya ya taifa. Lakini haiwezi kuzaliwa kwenye kivuli cha hofu, damu na ukimya. Lazima kwanza tuwe na ujasiri wa kukiri makosa, kurejesha haki, na kuwajibisha wahusika. Ndipo Katiba Mpya itakuwa na uhalali wa kuongoza kizazi kijacho.”

 

Kwa kuhitimisha niseme mambo manne:

Kwanza, Katiba Mpya ni Deni la Taifa, Sio Zawadi ya Wanasiasa


Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa Katiba Mpya si fadhila ya viongozi wala ahadi ya kampeni—ni haki ya msingi ya wananchi. Ni deni la kihistoria ambalo taifa linapaswa kulilipa kwa vizazi vilivyopita, vilivyopo na vijavyo. Hakuna taifa linaloweza kujenga mustakabali imara kwa kuendelea kushikilia mfumo unaolalamikiwa na wananchi wake. Hivyo basi, shinikizo la Katiba Mpya halipaswi kuwa la wanasiasa pekee, bali liwe sauti ya kila Mtanzania—mkulima, mfanyakazi, mwanafunzi na mfanyabiashara. Hii ni vita ya haki, si mjadala wa kisiasa tu.

 

Pili: Mabadiliko ya Kweli Yanahitaji Ujasiri wa Taifa Zima siyo CHADEMA , Siyo Tundu Lissu, siyo waliofiwa na ndugu zao tangu mwaka wa 2015 na siyo wale waliopata vilema vya kudumu bali wote waliosalama maana kinyume chake yaliyowakuta waliotangulia ni zamu wa walio salama.


Safari ya kuelekea Katiba Mpya si ya maneno matupu, bali ni ya maamuzi magumu. Inahitaji ujasiri wa viongozi kukubali makosa, na ujasiri wa wananchi kudai haki zao bila woga. Taifa lisipochukua hatua sasa, historia haitalisamehe. Huu ni wakati wa kusimama, kusema ukweli, na kuchagua mwelekeo mpya. Katiba Mpya haitakuja kwa kelele pekee—itatokana na dhamira ya pamoja ya Watanzania wote kuikomboa nchi yao kutoka mifumo isiyokidhi matarajio yao.

 

Tatu, Katiba Mpya haipaswi kuwa kichaka cha kuwaficha waovu wala kificho cha kufunika maovu yaliyotendeka; badala yake, inapaswa kuwa mwanga unaofichua ukweli na kuimarisha haki. Taifa haliwezi kujenga mfumo mpya wa uongozi kwa msingi wa ukimya, hofu au kulindana. Ikiwa Katiba Mpya itatumika kama njia ya kusahau au kufumbia macho makosa ya zamani, basi haitakuwa suluhisho bali mwendelezo wa matatizo yale yale kwa sura mpya. Hivyo, kabla ya kuandika Katiba Mpya, lazima kuwe na ujasiri wa kuwataja, kuwachunguza na kuwawajibisha wote waliotenda uovu, ili Katiba hiyo iwe chombo cha haki, si kinga ya dhuluma.

 

Nne, Hii si hoja ya mtu mmoja. Hii ni sauti ya taifa linaloamka. Ni sauti ya Watanzania wanaosema—imetosha. Swali si tena kama Katiba Mpya inahitajika.Swali ni: je, tuna ujasiri wa kuifikia?

Mwanakwetu yupo. Na historia inaandika.

Nakutakia siku njema.

Kumbuka:

“Ukweli Kwanza, Katiba Mpya Baadaye.”

ADELADIUS MAKWEGA


Barua pepe: makwadeladius@gmail.com


Simu: 071
7 649 257

 

 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments