UJI WA MGONJWA ULIOLIWA NJIANI WAFIKA OFISINI

 


Adeladius Makwega


Musoma, Mara – Tanzania

 

Mkutano wa hadhara katika Kitongoji cha Rwakikoro, Kijiji cha Chirorwe, Wilaya ya Musoma, ulianza kama mikutano mingine ya kawaida ya kusikiliza kero za wananchi. Lakini ulipofika wakati wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi kuzungumza, hali ilibadilika. Wananchi wakasogea mbele, wengine wakatulia kimya, wakisubiri kusikia msimamo wa Serikali.

 

Na kweli, haukuchukua muda.

Kanali Mtambi alisema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote wa umma anayeshindwa kuwahudumia wananchi, akisisitiza kuwa uzembe hautaendelea kupewa nafasi katika Mkoa wa Mara.

 

Lakini kilichowafanya wananchi kutikisa vichwa na wengine kucheka kwa sauti ni mfano alioutoa kuhusu kukatika kwa huduma ya maji.

 

"Haiwezekani maji yakakatika kwa siku tatu, hospitali ikose maji, wananchi wapate tabu, halafu ukiuliza unaambiwa LUKU imeisha! Serikali ishindwe kununua umeme wa shilingi 150,000? Huu ni utani! Hili haliwezekani. Lazima tukuchukulie hatua."

 

Kauli hiyo ilizua vicheko na makofi, lakini ujumbe wake ulikuwa mzito—watumishi wa umma wanapaswa kuwajibika bila kusubiri kusukumwa.

 

Kana kwamba hiyo haitoshi, Mkuu wa Mkoa akaongeza mfano mwingine uliowafanya wengi kutabasamu huku wakitafakari.

 

"Mtumishi asiyetimiza wajibu wake ni sawa na mtu aliyeagizwa kumpelekea mgonjwa uji hospitalini, lakini akaunywa njiani. Halafu akiulizwa kwa nini mgonjwa hajapata uji, anasema, 'Mgonjwa akinywa uji anatapika kisha wewe unanenepa kwa uji wa mgonjwa!'"

 

Wananchi walicheka, lakini wengi walionekana kuelewa ujumbe uliokuwa umefichwa katika ucheshi huo—kwamba visingizio haviwezi kuchukua nafasi ya uwajibikaji.

 

Mbali na onyo hilo, Kanali Mtambi aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea kuwa karibu nao kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

 

Alikumbusha kuwa hivi karibuni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alifanya ziara katika Wilaya ya Musoma Vijijini. Huku yeye mwenyewe akieleza kuwa, kwa majuma mawili mfululizo, amekuwa akifanya ziara katika Kata ya Suguti kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

 

Na kabla hajafika kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa alikuwa ametembelea ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha uchenjuaji wa dhahabu chenye thamani ya takribani shilingi bilioni 14, ambacho kimefikia hatua za mwisho za ukamilishaji. Pia alikagua machimbo mbalimbali ya dhahabu ili kujionea maendeleo ya sekta hiyo na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea kwa kuzingatia sheria, usalama na manufaa kwa wananchi.

 

Mwisho wa siku, wananchi waliondoka na mambo mawili makubwa ya kukumbuka. La kwanza, Serikali imeweka msisitizo mkubwa kwenye uwajibikaji wa watumishi wa umma. La pili, kama tatizo ni LUKU ya shilingi 150,000, basi kisingizio hicho hakitakuwa tiketi ya kuendelea kubaki ofisini bila kuwajibika.

 

Swali likabaki: Makala haya yaitweje?

  • Uji wa Mgonjwa Ulioliwa Njiani Wafika Ofisini
  • Mgonjwa Akinywa Uji Anatapika
  • LUKU Ikiisha na Kazi Imeisha
  • Kutoka LUKU Hadi Uji wa Mgonjwa

Mjomba Mwanakwetu amechagua:

"Uji wa Mgonjwa Ulioliwa Njiani Wafika Ofisini."

 

Nakutakia siku njema.

 

Adeladius Makwega


Barua pepe: makwadeladius@gmail.com


Simu: 0717 649 257

 

 













 

0/Post a Comment/Comments