Ufalme wa Mungu si Hadithi: Unaonekana Kwenye Maisha Halisi!

 


 

Adeladius Makwega – Musoma MARA TANZANIA.

 

Tafakari ya Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa, kama ilivyotayarishwa na Padri Bonaventura Maro, imejikita katika “Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni,” ikisisitiza umuhimu wa kuweka vipaumbele vya kiroho mbele ya mambo ya kidunia. Kupitia simulizi ya Mfalme Sulemani, inaonesha hekima ya kuchagua kilicho bora zaidi mbele ya Mungu. Sulemani aliomba hekima badala ya mali au utukufu, akitambua kuwa uongozi bora unahitaji moyo wa kusikiliza na kupambanua mema na mabaya. Hivyo, waamini wanahimizwa kujiuliza vipaumbele vyao katika sala na maisha yao kwa ujumla, wakitafuta yale yanayowasaidia kupata uzima wa milele badala ya mafanikio ya muda mfupi.

 

Aidha, tafakari hii inaeleza umuhimu wa kuongozwa na Mungu katika maisha ya kila siku. Inasisitiza kuwa moyo msikivu unaofuata sheria ya Mungu humwezesha mtu kufanya maamuzi sahihi hata katikati ya changamoto. Kwa mfano wa Sulemani, inaonekana wazi kuwa mafanikio yanatokana na kumweka Mungu mbele kama mshauri mkuu. Waamini wanahimizwa kudumisha maisha ya sala na shukrani, kwani moyo wa shukrani humsaidia mtu kutambua neema alizonazo tayari badala ya kulalamika au kutamani zaidi.

 

Katika Injili, mifano ya hazina iliyofichwa, lulu ya thamani na wavu inaeleza kuwa Ufalme wa Mungu ni hazina ya thamani kuu inayopaswa kutafutwa kwa juhudi zote. Wale wanaoutambua wanapaswa kuwa tayari kuacha yote yanayowazuia ili kuupata. Hata hivyo, Ufalme huo unawakaribisha wote, lakini kila mtu anawajibika kufanya uchaguzi binafsi na kuishi kwa haki. Padri Maro anafunga jalada la tafakari yake kwa kuhimiza waamini kuendelea kujifunza na kushiriki Injili, huku wakitafuta kumjua Mungu zaidi ili hatimaye wapate uzima wa milele.

Kwa upande wake, Kardinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimwenguni anayeshughulikia Uinjilishaji wa Watu, anatoa utangulizi wa Dominika hii kwa kusema:

 

“Katika Injili, Yesu anaufananisha Ufalme wa Mungu na hazina iliyofichwa shambani, mfanyabiashara anayetafuta lulu nzuri, na wavu uliotupwa baharini unaokusanya samaki wa kila aina. Hii ndiyo hitimisho la mafundisho ya Yesu katika sura ya 13 ya Injili ya Mtakatifu Mathayo.

 

Ufalme wa Mungu ni wa thamani kubwa kama hazina na lulu ya thamani. Ili kuupata, inafaa mtu awe tayari kuacha au kupoteza kila kitu, kama yule mtu katika mfano alivyofanya. Aliuza kila kitu alichokuwa nacho ili kununua shamba lenye hazina iliyofichwa. Vivyo hivyo kwa mfanyabiashara, aliuza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua ile lulu ya thamani kubwa aliyokuwa ameipata.

Kisha mfano wa mwisho unatukumbusha ule tuliousikia wiki iliyopita: siku ya hukumu itakapofika, Mungu atawatenganisha watu kama samaki waliokusanywa—wema na wabaya, wenye haki na wasio haki. Kuwa sehemu ya Ufalme wa Mungu kunahitaji neema na ujasiri wa kuchagua lililo muhimu zaidi.”

Katika Dominika hii, Mwanakwetu alisali katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma, na akiwa njiani kurudi anapoishi alikutana na taswira tatu:

 

Kisa cha kwanza:


Mama mmoja mtu mzima, aliyekuwa anatembea kwa tabu, alikuwa anatoka kanisani huku akiwa ameshikwa mkono na baba mmoja ambaye sura zao zilifanana mithili ya kaka na dada. Mkono wa kushoto wa mama huyu ulikuwa na mkongojo. Alitoka nje, akaketi kando ya sakafu ya duka la parokia, kisha pikipiki ikaja na kumbeba yeye pamoja na binti mmoja ambaye huenda ndiye anayemsaidia, na wakaondoka kuelekea nyumbani kwao.

 

Kisa cha pili:


Mwanakwetu alitembea kwa dakika tano, akapita eneo la zizi la ng’ombe ambapo mama mmoja alikuwa anakamua maziwa. Zizini kulikuwa na takribani ng’ombe 60 pamoja na watu wengine kadhaa. Mama huyu alimkaripia binti yake akisema:


“Tunapokuja zizini hatuji kucheza. Kila mtu ana majukumu yake. Mimi ninakamua ng’ombe maziwa, wewe unafanya usafi wa zizi, mwingine anawawekea ng’ombe pumba, na mwenzenu wa kuwachunga anakwenda kuchunga tukishamaliza kazi za awali. Hivyo nasema kila mmoja atimize jukumu lake ili mambo yaende vizuri. Hapa nyumbani kwangu sitaki mchezo. Kama mnataka utani, kafanyeni mkiwa na nyumba zenu; hapa ni nyumbani kwangu.”

 

Kisa cha tatu:


Mwanakwetu aliendelea na safari yake, akakutana na akina mama wawili wakiongea.

Mmoja alisema:


“Bosi wake amepelekewa pesa jana, amekataa. Anasema haya mauzo siyo ya kawaida; yeye anajua duka lake linaingiza shilingi 350,000/= kwa siku. Inawezekanaje tangu aondoke apewe 150,000/=?”

Mama mwingine akauliza kwa lafudhi ya Kijita:

 

“Kwani huyo bosi hajui mauzo yanapungua?”


Yule wa kwanza akajibu:

“Anajua kama yanapungua, lakini yakipungua ni labda 310,000/=, siyo nusu ya mauzo ipungue.”

Mwanakwetu akapishana nao, kisha akafika anapoishi na ndipo akayatayarisha makala haya.

Je, visa hivi vinafanana vipi na masomo ya Dominika hii?


Visa hivi vina uhusiano mkubwa na mafundisho ya Dominika ya 17 ya Mwaka A, yanayozungumzia thamani ya Ufalme wa Mungu na umuhimu wa kuweka vipaumbele sahihi maishani.

Kisa cha kwanza (Mama mzee kutoka kanisani):


Kisa hiki kinaonesha thamani ya imani na kujitoa kwa Mungu licha ya udhaifu wa kimwili. Mama yule, ingawa ana matatizo ya kutembea, bado anahakikisha anahudhuria ibada na kushiriki maisha ya kiroho. Hii inafanana na Injili inayosisitiza kuwa Ufalme wa Mungu ni hazina ya thamani ambayo mtu anapaswa kuitafuta kwa juhudi zote. Mama huyu anaonyesha kuwa hata katika hali ngumu, mtu anaweza kuchagua kumweka Mungu mbele, akionesha kwamba mambo ya kiroho yana thamani zaidi kuliko raha za mwili.

Kisa cha pili (Mama anayewasimamia watoto zizini):


Hapa tunaona somo la uwajibikaji na kupanga vipaumbele. Mama anasisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kutimiza jukumu lake bila uzembe. Hii inafanana na mafundisho ya Injili kuhusu kujitoa kikamilifu katika kutafuta “lulu ya thamani,” yaani Ufalme wa Mungu. Kama ilivyo kwa mfanyabiashara aliyekuwa tayari kuacha yote ili kupata lulu, vivyo hivyo maisha yanahitaji nidhamu, uwajibikaji na juhudi ili kufikia malengo ya maana, hasa yale ya kiroho

Kisa cha tatu (Mazungumzo kuhusu biashara na uaminifu):


Kisa hiki kinaonesha changamoto ya haki na uaminifu katika maisha ya kila siku. Tofauti ya mauzo inaleta mashaka ya uaminifu, jambo linalohusiana na mfano wa wavu unaokusanya samaki wema na wabaya. Injili inatukumbusha kuwa mwisho wa yote kutakuwa na hukumu ambapo haki na udanganyifu vitatenganishwa. Hivyo, kisa hiki kinafundisha umuhimu wa kuishi kwa uadilifu, kwani kuwa sehemu ya Ufalme wa Mungu kunahitaji kuchagua mema na kuishi kwa haki kila siku.

 

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Ufalme wa Mungu si Hadithi: Unaonekana Kwenye Maisha Halisi!”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257












0/Post a Comment/Comments