Sauti ya Kwanza Kuisikia Leo Hii

 




Adeladius Makwega – Bunda, Mara, Tanzania

 

“Leo ulipoamka asubuhi, ni sauti ipi ya kwanza uliyoisikia?”

 

Mjomba Mwanakwetu aliuliza swali hili kwa baadhi ya Watanzania.

 

“Mimi nilisikia sauti ya kuku, ambapo jogoo wangu aliwika ‘kokorikooooo’.”


— Haya ni majibu ya Leonard Lameck.

 

“Leo mimi sikusikia sauti yoyote ile.”


— Haya ni majibu ya Issa Mbombwe.

 

“Mimi nilisikia sauti ya ndege, ambao kwa hakika ndiyo walioniamsha, kisha nikasikia kuku na ng’ombe.”
— Haya ni majibu ya Rebecca Mdodo.

 

“Mimi nilisikia sauti ya ng’ombe, kisha nikasikia sauti ya bodaboda.”


— Haya ni majibu ya Prisca Blaise.

 

Msomaji wangu, haya ni baadhi ya majibu yaliyotokana na swali ambalo Mwanakwetu aliuliza kwa Watanzania watano aliokutana nao Alhamisi, Julai 9, 2026, mkoani Mara.

 

Kwa kuyatazama majibu haya, ni wazi kuwa wengi wa waliohojiwa walitaja sauti za wanyama kama kuku, mbuzi na ng’ombe—wanyama wanaofugwa kwa wingi mkoani Mara.

 

Nina hakika hata wewe, msomaji wangu, ukiulizwa swali hili leo: ulipoamka asubuhi, ni sauti ipi ya kwanza uliyoisikia?


Bila shaka unayo majibu—tafakari majibu lako.

 

Iwapo kati ya watu watano, wanne wanasema walisikia sauti za ndege, kuku, mbuzi au ng’ombe, inaashiria kuwa wanaishi karibu na mifugo hiyo.

Huu ndio uhalisia wa maisha ya vijijini na hata baadhi ya maeneo ya mtaani, ambapo mifugo imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya mwanadamu.

 

Swali la kujiuliza ni hili:

 

“Je, katika ofisi za umma, kuna jitihada zinazoonesha uhalisia huu wa jamii inayoishi karibu na mifugo?”

 

Kwa hakika, mkoani Mara kuna juhudi mbalimbali zinazofanywa—ikiwemo utoaji wa chanjo kwa mifugo, upatikanaji wa malisho bora, na uboreshaji wa mifumo ya biashara ya wanyama.

“Kwa sasa tunafanya usajili wa wadau wa nyama na maziwa, mathalani mabucha, ili wawe na leseni za biashara zao. Leseni ya bucha inapolipiwa kwa mara ya kwanza ni shilingi 70,000 (dola 28 za Kimarekani), na inapohuhishwa ni shilingi 50,000 (dola 20 za Kimarekani).”

 

Haya ni maelezo ya Mathias Lusheleja, Afisa Mifugo Mkoa wa Mara, kuhusu shughuli za serikali katika sekta ya biashara ya wanyama.

 

“Pia tunasajili minada na machinjio ya kila halmashauri. Usajili huu unafanywa kupitia wakurugenzi watendaji, ambao ndio wasimamizi wa minada na machinjio katika maeneo mengi. Gharama ya usajili mpya ni shilingi 120,000 (dola 48 za Kimarekani), na ya kuhuhisha ni shilingi 100,000 (dola 40 za Kimarekani).”

 

Aidha, Ndugu Lusheleja aliongeza kuwa kuna usajili wa wafanyabiashara wanaonunua mifugo ndani ya halmashauri moja, ambapo kibali hulipiwa shilingi 60,000 (dola 24 za Kimarekani kwa mwaka). Kwa wale wanaonunua mifugo katika zaidi ya halmashauri moja, hulipa kibali cha shilingi 300,000 (dola 120 za Kimarekani kwa mwaka).

 

Mwanakwetu aliuliza: je, usajili huu una manufaa gani kwa jamii?

Akijibu swali hilo, Ndugu Lusheleja alisema kuwa usajili huo unasaidia kuongeza mapato ya taifa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, kulinda usalama wa walaji, kupunguza usumbufu kwa wadau, na pia kutekeleza matakwa ya kisheria.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kumbe hata usajili wa wanyama na malipo ya Leseni ya shughuli za wanyama pia unakuza ustawi wa binadamu katika maboresho ya maisha yake katika miradi minginehasa upatikanaji wa rasilimali fedha zinazotumika kuboresha elimu, afya, miundombinu na kadhalika hakika mifugo ipo jirani zaidi ya binadamu.

 

Msomaji wangu kumbuka jibu hili:

“Leo mimi sikusikia sauti yoyote ile.”

 

Mwanakwetu anaamini kuwa hata ndugu Issa Mbombwe yule mdau mmoja aliyesema maneno haya kila siku inyaokwenda kwa Mungu anasikia sauti ya mifugo katika sekta za elimu, afya ,barabara hata anapopanda bodaboda zinazopita katika barabara zetu zilizojengwa kwa fedha za mifugo yetu.


Mwanakwetu, upo? Kumbuka:

 

“Sauti ya Kwanza Kuisikia Leo Hii.”

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 









 

0/Post a Comment/Comments