Adeladius Makwega – MBAGALA
Julai 27, 2026
Mwanakwetu alizungumza na kada mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu mambo kadhaa. Hata hivyo, hoja kuu iliyokuwa mezani ilikuwa juu ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na misimamo yake isiyoyumba.
Ndugu huyu alianza kwa kusema:
“Wao wana ajenda yao. Hawajui kuwa yeye amesimama imara katika ajenda ya uzalendo na utaifa kwanza.
Wanachochanganyikiwa nacho ni kile wanachokiona tu; hawajui kuwa moyo wa mtu ni kichaka.

Kitu cha pili ambacho hawakifahamu ni kuwa Dkt. Nchimbi ni mtu sahihi sana — lakini siyo sahihi kwao, siyo sahihi kwa ajenda zao. Hao wenye ajenda zao wamejichanganya, wakidhani wanaweza kufanya kama walivyoweza kufanya kwa Dkt. Philip Mpango, mtangulizi wa Dkt. Nchimbi. Hapa wamelamba galasa, hapa wamekula wa chuya.”
Mwanakwetu akamjibu ndugu huyu kwamba, kwa sasa, Dkt. Emmanuel Nchimbi ana kundi kubwa la watu wanaokubaliana na msimamo wake.
Kwa mtu asiye makini, anaweza kujikuta akihangaika kutaka kujua: Je, Dkt. Nchimbi anawasiliana na nani? Anaongea na nani, na kuhusu nini? Ni nani anayechochea haya?
Maswali haya ni ya kipuuzi ikiwa mtu atahangaika kuyafuatilia. Hata ukichunguza mawasiliano ya simu ya kiongozi huyu, bado huo utakuwa upotevu wa muda.
Kutoka kwake hadharani ni ishara ya uamuzi wenye busara kubwa. Inaonekana ameona hilo, na sasa ameamua kuweka msimamo wake wazi.

Ni kana kwamba anawaambia wapinzani wake wanaomuita “Yuda”:
“Msimamo wangu hampaswi kuutafuta kwa tochi — upo wazi. Acheni kuutafuta kwa kurunzi. Katiba Mpya ndiyo habari ya mjini.”
Mwanakwetu akasema-Jamaa wananuna, mapovu yanawatoka, jasho kali linawaandama, hakuna manukato wala ubani wa kuficha hili.
Ndugu huyu akaongeza:
“Ukitaka kujua kuwa msimamo wa Dkt. Nchimbi unaungwa mkono na kundi kubwa, angalia kauli za Jaji Joseph Warioba, na Dkt. Anna Tibajuka. Tazama anachosema Askofu Dkt. Bagonza. Soma makala za Askofu Emmaus Bandakile Mwamakulya. Msikilize Maria Sarungi. Hata Mange Kimambi — anasema nini? Soma maoni mitandaoni, pia sikiliza maoni mitaani/vijijini, jibu unalo.
Usipokuwa makini, utadhani kundi hili linakutana mahali fulani kwa siri. Lakini ukweli ni kwamba, hawakutani — mawazo yao tu ndiyo yanafanana kwa mshangao mkubwa.”
Mwanakwetu akamwambia ndugu huyu kuwa jambo hili linashangaza, hasa ukizingatia kuwa hata Humphrey Polepole aliwahi kumpinga Dkt. Nchimbi waziwazi lakini Dkt Nchimbi anakuja na taswira nyingine kabisa kama mkongwe wa siasa za Tanzania.
Akaongeza mfano wa Biblia, akisema hali hii inafanana na ile ya Yesu na wanafunzi wake:
Matendo ya Mitume 4:13
“Walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, wakatambua ya kuwa walikuwa pamoja na Yesu.”
Hii inaonyesha kuwa wanafunzi walitambulika kwa sababu walifanana na Yesu — katika ujasiri, maneno, na matendo yao.
Hali ndiyo ilivyo sasa nchini Tanzania.
Baadaye, Mwanakwetu aliagana na ndugu huyo, na akaamua kuyaandika mawazo haya kama yalivyo.
Akiwa peke yake, alijisemea:
“Awali, waliosema walionekana mithili ya ‘tumbili’ wakiongea, walidharauliwa na kuonekana hawana maana. Baadhi ya wanachama wa CCM waliwadharau. Lakini sasa mambo yamebadilika — yale waliyoyadharau yanawauma, wanakaribia kukata tamaa, donge limewakaa, hawana pa kujificha.
Ngwengwe (nyani mkubwa) ametoka msituni — sasa yuko hadharani, anazungumza waziwazi.”
Kwa kifupi, kati ya viongozi wa CCM walio hai na wenye ushawishi mkubwa kwa sasa, Dkt. Emmanuel Nchimbi anaonekana kuwa kinara.
Ni miongoni mwa wanachama wachache walioshiriki vikao vingi vya Kamati Kuu ya CCM Taifa kuliko wengine wengi. Anapozungumza — ni nani anayeweza kujibu hoja zake kwa uzito uleule? Ni nani anayeweza kujitokeza hadharani kwa ujasiri huo? Wanaojitokeza kubweka ni vinyangarika tu — hawana hoja, hawana majibu.
Mwanakwetu anakubaliana na hoja ya Katiba Mpya kama alivyosisitiza Dkt. Nchimbi. Hata hivyo, anaamini kuwa kabla ya yote, haki lazima itendeke kwa wale waliodhulumiwa, ili taifa liingie kwenye mchakato wa Katiba Mpya likiwa limepona majeraha.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Mosi, Hoja juu ya usalama wa Dkt. Nchimbi,
Msimamo wazi na usioyumba wa Dkt. Nchimbi katika masuala ya kitaifa unahitaji
kulindwa kwa kiwango cha juu, kwani anaonekana kuwa kiongozi anayebeba
matarajio ya kundi kubwa la wananchi. Katika mazingira ambapo kuna upinzani
mkali wa kisiasa ndani ya nchi, shinikizo la kimataifa na kimtazamo, ni muhimu
kuhakikisha usalama wa hoja zake na wa kisiasa na hata usalama binafsi
unadumishwa ili asiathiriwe na shinikizo au vitisho vinavyoweza kudhoofisha
utekelezaji wa majukumu yake ya kitaifa.
Pili, Hoja juu ya haki
Kabla ya taifa kuingia kikamilifu katika mchakato wa Katiba Mpya, haki kwa
waliodhulumiwa ni jambo la msingi lisiloweza kupuuzwa. Mwanakwetu anaonesha
wazi kuwa kuna majeraha ya kijamii na kisiasa ambayo yanahitaji kushughulikiwa
kwanza. Haki ikitendeka, itaweka msingi wa maridhiano na umoja wa kitaifa,
jambo litakalofanya mchakato wa Katiba Mpya kuwa wa haki, shirikishi na wenye
kukubalika na wengi. Katiba Mpya siyo mali ya Viongozi, siyo mali ya CCM , siyo
hoja ya ilani , siyo hoja ya upinzani hii ni hoja ya Watanzania wote .
Tatu, Hoja juu ya Katiba Mpya
Msimamo wa Dkt. Nchimbi kuhusu Katiba Mpya unaonekana kuwa ni ajenda kuu ya
kitaifa inayohitaji kupewa kipaumbele. Katiba Mpya inapaswa kuwa chombo cha
kuimarisha demokrasia, kulinda haki za wananchi, na kuweka misingi imara ya
uongozi bora. Kauli yake ya kuifanya Katiba Mpya kuwa “habari ya mjini”
inaashiria umuhimu wake katika kuleta mabadiliko chanya yanayohitajika nchini.
Nne Hoja juu ya wanaompinga Dkt. Nchimbi
Wanaompinga Dkt. Nchimbi wanaonekana kuchanganyikiwa kutokana na kutofautiana
kwa ajenda zao na msimamo wake wa uzalendo na utaifa. Upinzani wao haujajengwa
katika hoja nzito bali katika mitazamo ya maslahi binafsi au ya makundi. Hali
hii inaonekana wazi ambapo inaelezwa kuwa wengi wao hawana majibu ya hoja zake
bali huishia kushambulia bila msingi thabiti, jambo linalozidi kuimarisha
nafasi yake mbele ya umma.
Mwanakwetu upo — kumbuka.
“Ngwenge Ametoka Msituni,Wenye Mishale Kaeni kwa Tahadhari.”
Nakutakia siku njema.
Mawasiliano:
📞 0717 649 257
.gif)


.gif)
.gif)




Post a Comment