.gif)
Adeladius Makwega – Serengeti & Tarime, Mara, Tanzania
Ilikuwa ni majira ya asubuhi ya Julai Mosi, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba (MB), alishuka katika Kiwanja cha Ndege cha Soronera kilichopo katika Mbuga ya Serengeti, mkoani Mara, ili kuanza rasmi ziara ya siku kadhaa ndani ya mkoa huu aliozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mjadala wa wanahabari wa Mkoa wa Mara waliobahatika kushiriki ziara hii kwa siku ya kwanza ulikuwa ni namna wananchi watakavyouliza maswali kwa Waziri Mkuu na namna majibu yatakavyokuwa.
Mazingira ya Mbuga ya Serengeti yalikuwa ya baridi kali, huku kukiwa na watalii wengi na magari ya utalii yakitapakaa katika njia mbalimbali za mbuga hii. Ndege ndogo zilikuwa zikitua na kuruka katika kiwanja hiki, na watu wa rangi tofauti walionekana katika uwanja huu mdogo mithili ya uwanja mkubwa wa ndege kama ule wa Amsterdam, Uholanzi.
Waziri Mkuu alishuka na kupokelewa na viongozi kadhaa, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Ziara ilianza rasmi katika mradi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, ambapo taarifa ilisomwa na Waziri Mkuu kukagua jengo hilo, kisha akaelekea katika Uwanja wa Sokoine wilayani Serengeti.
Baada ya kuzungumza na wananchi wa Serengeti, ziara ilihamia Wilaya ya Tarime katika Jimbo la Tarime Vijijini. Waziri Mkuu alipiga hodi katika mji wa Nyamongo, ambapo kwanza alizungumza na wananchi wa eneo hili lenye utajiri wa madini ya dhahabu, kama alivyofanya Serengeti, kisha kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali.
Katika maeneo yote mawili, yaani Serengeti na Nyamongo, ilipofanyika mikutano hii ya Julai Mosi, 2026, wananchi walipewa nafasi ya kuuliza maswali kwa njia mbili. Kwanza, kupitia meza maalum ya Dawati la Kero, ambapo hoja zao zilisikilizwa na kujibiwa moja kwa moja na mawaziri husika. Pili, Waziri Mkuu alitoa nafasi ya kuulizwa maswali ya moja kwa moja, akijibu changamoto za binafsi, za vikundi na hata migogoro mbalimbali.
Miongoni mwa waliozungumza ni Mwajuma Wambura, aliyelalamikia kuondolewa katika eneo linalotarajiwa kujengwa Uwanja wa Ndege wa Serengeti, huku akiomba Serikali itenge maeneo ya kuhamishia makaburi yaliyopo tangu mwaka 1990.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali inaruhusiwa kisheria kuchukua maeneo na kuyabadilishia matumizi, lakini kila mwananchi aliyepo kihalali atalipwa fidia stahiki, kwani dhamira ya Serikali si kumdhulumu mtu.
Miongoni mwa waliopata nafasi pia ni msichana aliyejitambulisha kama Easter Marwa, aliyehitimu kidato cha nne kwa daraja la tatu, akiomba msaada wa kielimu. Waziri Mkuu aliahidi kumsaidia na kumsomesha hadi Chuo Kikuu.
Kisa cha kusikitisha kilikuwa cha kijana aliyejitambulisha kama Ghati Chacha Magebe, aliyesema alipigwa risasi mwaka 2014 akiwa mdogo wakati akichunga mifugo ya familia yake, kufuatia mgogoro kati ya askari na raia karibu na mgodi wa North Mara.
Alitibiwa Musoma Mjini kwa msaada wa mgodi huo. Baadaye mgodi ulitaka kumpa fidia ya shilingi milioni 13, lakini familia yake ilikataa kwa madai kuwa fidia hiyo ilikuwa ndogo. Baadaye alitibiwa katika Hospitali ya Bugando. Baada ya kupona, aliomba fidia ili aweze kusoma VETA, lakini kwa miaka 12 sasa suala hilo halijapatiwa ufumbuzi.
Waziri Mkuu aliagiza Naibu Waziri wa Madini, uongozi wa mgodi wa North Mara, kijana husika pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime wakutane mara moja kujadili suala hilo na kuhakikisha analipwa fidia stahiki bila kuchelewa.
Katika wilaya zote mbili Serengeti na Tarime, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wa kufanya ziara hii, akisisitiza kuwa ,
“Heri mgeni aje ili mwenyeji apone.” Kanali Mtambi aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo, ndugu Gerald Musabila Kusaya
.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Mwanakwetu ameshuhudia Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba, akitoa nafasi kwa wananchi kutoa hoja zao na kujibu maswali yao kwa ufanisi, licha ya muda kuwa mfupi. Wananchi walipendekeza muda wa maswali uongezwe, na mawaziri washughulikie baadhi ya hoja katika makundi kupitia Dawati la Kero ili kumpa Waziri Mkuu nafasi ya kupokea maswali mengi zaidi ya moja kwa moja.
Hoja nyingine iliyojitokeza Nyamongo ni kuhusu matumizi ya kipaza sauti. Wananchi walipendekeza kipaza sauti kisiwe kinashikwa na mtu bali kiwekwe kwenye stendi, ili mwananchi aongee kwa uhuru bila usumbufu wakati anatoa hoja zake kwa Waziri Mkuu. Pendekezo hili lilitokana na tukio la mvutano kati ya mshika kipaza sauti na mwananchi aliyekuwa akieleza kisa chake cha kupigwa risasi. Katika hali hiyo, mwananchi huyo alisema:
“Naomba niongee, kwa sababu naongea na mkubwa, acha niongee.”
Waziri Mkuu akisema Ongea kwa uhuru unaongea na mimi.
Hitimisho
Mwanakwetu anapongeza hatua ya Waziri Mkuu ya kutoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha hoja zao kwa uhuru na kuzishughulikia kwa weledi mkubwa.
Msomaji wangu haya ni makala ya muhtasari wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, katika Wilaya ya Serengeti na eneo la Nyamongo, Tarime Vijijini, Julai Mosi, 2026.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Naomba niongee, kwa sababu naongea na mkubwa, acha niongee.”
Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257









.gif)
Post a Comment