.gif)
Adeladius Makwega – MBAGALA
Julai 31, 2026, MwAnAkWeTu wa Mbagala alikuwa jijini Dodoma tangu mapema ya siku hii hadi saa 7:21 ya mchana. Ufuatao ni muhtasari wa simulizi alizokutana nazo katika mkoa huu ambao ndipo alipozaliwa miaka 52 iliyopita.
Saa 6:56 mchana alishuka katika basi, stendi ya mabasi ya kijijini Chamwino Ikulu, katika basi linalofanya safari zake Makole–Chamwino Ikulu–Makole. Mara baada ya kushuka basini, macho yake yalikutana na Msikiti wa Abubakari bin Zuberi, ambapo katika geti la akinamama walionekana mabinti kadhaa waliovalia sare za shule wakiingia msikitini kusali Salaat Ijumaa.
Spika za msikiti huu zilikuwa zinanadi maneno haya:
“…Amma baadi, ndugu zangu Waislamu, haya ninawausia nyinyi na nafsi yangu…”
Wanafunzi hawa mabinti walikuwa wa shule za msingi wakiwa mbele na wa sekondari wakiwa nyuma.
Hawa wa sekondari walikuwa wamevaa sketi za rangi kama kijani na juu walivaa hijabu. Sketi zao za shule zilikuwa fupi. Nyuma ya hawa mabinti wa sekondari, kijana mmoja mwenye umri wa miaka takribani 32/33 aliwatazama kisha akawaambia:
“Hoyaa, embu acheni mambo yenu, acheni kukaa uchi, vaeni nguo, vaeni vizuri.”
Taswira iliyopamba macho ya MwAnAkWeTu ilikuwa khanga na vitenge kadhaa vilivyoangukia magotini mwao kutoka makwapani, kisha wakajifunga na kuingia geti la wanawake la msikiti huu.
Binafsi, nikavuka barabara na mbele kidogo nikakutana na mama mmoja wa Kigogo, kalewa pombe chakali, huku akiniita na kunikimbilia:
“Makwega! Makwega, Makwega! Muwaha auuya! (Mkubwa amerudi!). Muwaha auuya! Muwaha auuya? Mkubwa kumbe umaerudi?”
Huyu mama alinisogelea akaniambia:
“Mbona nyumba zako zinakufa, miti yako imekufa, migomba yako imekufa, miwa yako imekufa, miembe yako imekufa? Tukasema sasa na mwenyewe utakuwa umekufa…”
Nikamjibu huyu mama kuwa bado nipo hai, na hata baadhi ya mimea yangu ipo hai. Kama mimea yangu ingekufa yote, tambueni kuwa na mimi na nyinyi tungekuwa tumekufa, maana miti ni uhai.
Mama huyu akaniomba shilingi 1,000 ya ugimbi (pombe), kisha tukaagana naye.
Awali, MwAnAkWeTu alikutana na taswira mbili:
.gif)
Kwanza, alikuwa anakwenda Ofisi ya Rais – Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Akaangalia ramani lakini hakuweza kufahamu
ilipo ofisi hii. Akaangalia tovuti ya taasisi hii nayo ikawa inatoa maelekezo
lakini ni vigumu kujua ilipo. Hivyo basi, akamtafuta dereva wa Bolt, naye
akaanza kuitafuta katika Google Map bila kufanikiwa.
Kijana huyu anayefahamika kama Yusuph, dereva wa Bolt wa Dodoma (anayepatikana kwa simu 0704393491), alisema:
“Mzee, hii ofisi yenyewe inaitwa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Sasa huko kuna
mambo yetu muhimu sana, kama vile mikataba ya madini na mambo nyeti. Huko ni
ngumu kufika. Ebu mpigie simu mtu mwingine atuongoze. Lakini kabla ya kwenda,
kwani mzee unakwenda kufanya nini? Au huko kuna baibe (mrembo) anafanya kazi
huko?”
Nikacheka kisha nikamjibu kuwa mambo ya baibe nimeshastaafu, mimi ni mzee. Kijana huyu akasema:
“Hapana, wazee nyinyi ni hatari sana, maana mkihonga mnahonga vizuri—tangu
viwanja, magari na magorofa. Sasa sisi vijana hatuna uwezo huo.”
MwAnAkWeTu akacheka sana, kisha akampigia simu Afisa Usafirishaji, Gideon Chilongani, naye akatoa maelekezo haya:
“Ukifika Martin Luther School, tembea kidogo kwa ndani, utakuta jengo la TMDA;
kisha ofisi inayofuata ndiyo Ofisi ya Rais – Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.”
Nikamwambia Yusuph, akasema sawa, na akaniambia kuwa kumbe pale sasa malipo yake ni shilingi 5,000 (= dola mbili za Kimarekani). Akapewa pesa hiyo na kunifikisha ofisi hii.
Hapa nilihudumiwa na dada mmoja mwenye maswali ya uchokozi, ambaye nadhani ndiye mkubwa, huku wenzake wakiwa si wachokozi—walikuwa wakarimu na wachangamfu.
Nilipomaliza huduma hii, ndipo nikapanda basi lile la Makole–Chamwino–Makole, na hapo ndipo nikakutana na visa vya mabinti msikitini na kile cha “Muwaha Auuya!”
Kumbuka, huu ni muhtasari wa simulizi zangu kwa siku ya Julai 31, 2026 hapa Dodoma nchini Tanzania.
Je, msomaji wangu unajifunza nini katika visa hivi?
Simulizi hizi zinatupa mafunzo kadhaa muhimu ya kijamii, kiutamaduni na kimaisha:
Kwanza, maadili na mavazi ya heshima—tunaona mjadala kuhusu uvaaji wa mabinti na namna jamii inavyotazama suala la staha, hasa katika maeneo ya ibada.
Pili, hali halisi ya jamii—kupitia yule mama mlevi, tunaona changamoto za maisha kama umaskini, ulevi, na namna watu wanavyochanganya ukweli na hisia katika mazungumzo, huku hoja ya utunzaji mazingira ikitajwa.
Tatu, mtazamo wa vizazi tofauti—maongezi kati ya MwAnAkWeTu na kijana wa Bolt yanaonesha tofauti ya fikra kati ya vijana na wazee kuhusu maisha, mafanikio, na mahusiano.
Nne, changamoto za mifumo na huduma za umma—ugumu wa kuipata ofisi kwa kutumia ramani au tovuti unaonesha mapungufu katika upatikanaji wa taarifa na huduma, huku makala sasa yanasaidia kumuelekeza mtu ilipo taasisi hii.
Tano, uhusiano wa kibinadamu na mawasiliano—kutoka msikitini hadi barabarani na ofisini, simulizi zinaonyesha jinsi mawasiliano ya moja kwa moja yanavyobeba maana, hisia, na wakati mwingine migongano.
Kwa ujumla, tunajifunza kuwa maisha ya kila siku yanamafunzo mengi—kuhusu maadili, uhalisia wa jamii, na umuhimu wa kuelewana kati ya watu wa mitazamo tofauti.
Mwanakwetu upo? Kumbuka.
“Muwaha Auuya!”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)
Post a Comment